Generic placeholder image

JUMANNE JUMA LA 15 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Bwana Mungu na wa vyote Muumba,
Ulimwengu nawe wategemezwa.
Vyote hubadilika na kuoza,
Wewe hapana, wabaki ni Mpya.

Ndiwe faraja na ya mtu kinga,
U Mwamba juu yake wa kujenga,
Ndiwe makao tulivu ya roho,
Yote hutimilika ndani yako.

Asifiwe Baba na Mwana Mungu,
Asifiwe Roho Mtakatifu;.
Na utukuzwe Utatu milele,
Nguvu yetu maisha yetu yote.

ANT. I: Mapendo ni utimilifu wa Torati.

Zab.119:97-104 XIII Kuipenda sheria ya Mungu
Naipenda sana sheria yako.*
Naitafakari mchana kutwa:

Agizo lako liko nami daima,*
lanifanya mwenye hekima zaidi kuliko adui zangu.

Ninaelewa zaidi kuliko walimu wangu wote,*
kwa kuwa nayatafakari maagizo yako.

Nawapita wazee kwa busara yangu,*
kwa sababu nazishika amri zako.

Najizuia kufuata mwenendo wowote mbaya,*
nipate kulizingatia neno lako.

Sikukiuka maagizo yako,*
maana wewe mwenyewe ni mwalimu wangu.

Maagizo yako ni matamu mno kwangu;*
matamu kuliko asali!

Kwa sheria yako napata hekima,*
kwa hiyo nachukia kila mwenendo mbaya.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Mapendo ni utimilifu wa Torati.

ANT. II: Uwakumbuke watu wako, Ee Bwana, uliowachagua zamani za kale.

Zab.74 Ombolezo juu ya kubomolewa Hekalu
Msiwaogope wale wauao mwili (Mt.10:28)

I
Kwa nini, Ee Mungu, umetutupa kabisa?*
Mbona hasira yako inawaka dhidi ya kondoo wako?

Kumbuka jumuiya yako uliyoifanya tangu kale,/
kabila ulilolikomboa liwe mali yako,*
mlima Sion ulioufanya makao yako.

Pita juu ya magofu haya ya kudumu!*
Adui wameharibu kila kitu Hekaluni.

Wamepiga kelele za ushindi Hekaluni mwako!*
Wameweka humo bendera zao za ushindi!

Wanafanana na mtema kuni,*
anayekata miti kwa shoka lake.

Walivunjavunja milango ya Hekalu*
kwa mashoka na nyundo zao.

Walichoma moto patakatifu pako;*
walikufuru mahali pale unapoheshimiwa.

Walipania kutuangamiza sote pamoja;*
walichoma mahali patakatifu nchini kote.

Hamna tena ishara, hatuna tena nabii!*
Hata hatujui yatakuwa hivi hadi lini!

Mpaka lini, Ee Mungu, adui atakutukana?*
Je, watalikufuru jina lako hata milele?

Mbona umelegeza mkono wako?*
Kwa nini wakataa kufanya kitu?

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Uwakumbuke watu wako, Ee Bwana, uliowachagua zamani za kale.

ANT. III: Inuka, Ee Mungu, ujitetee mwenyewe!

II
Wewe, Ee Mungu, u mfalme wetu tangu awali;*
umefanya matendo makuu pote nchini.

Kwa enzi yako kuu uliigawa bahari;*
uliviponda vichwa vya majoka ya bahari.

Wewe uliviponda vichwa vya Lewiyatani;*
ukawapa wanyama wa jangwani mzoga wake.

Wewe umefanya chemchemi na vijito;*
na kuikausha mito mikubwa.

Mchana ni wako na usiku ni wako;*
umeweka mwezi na jua mahali pao.

Wewe umeweka mipaka yote ya dunia;*
umepanga majira ya kiangazi na ya baridi.

Kumbuka, Ee Mungu, madharau ya adui zako;*
taifa pumbavu linalikashifu jina lako.

Usiwatupie wanyama maisha ya wapenzi wako;*
usiwasahau watu wako wanaoteseka.

Ulikumbuke agano lako nasi!*
Nchi imejaa uharamia kila mahali pa giza.

Usiwaache wanaodhulumiwa waaibishwe;*
uwajalie fukara na maskini wakusifu.

Inuka, Ee Mungu, ukajitetee;*
ukumbuke madharau ya kila siku ya wasiokujua.

Usisahau makelele ya adui zako;*
na ghasia za daima za wapinzani wako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Inuka, Ee Mungu, ujitetee mwenyewe!

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: Yer.22:3
Fanyeni hukumu na haki, mkamtoe yeye aliyetekwa katika mikono ya mdhalimu, wala msiwatende mabaya mgeni, wala yatima, wala mjane, wala kuwadhulumu, wala msimwage damu ya mtu asiye na hatia katika mahali hapa.

K. Bwana ataitawala nchi kwa haki.
W. Atawahukumu watu bila upendeleo.

SALA:
Tuombe: Mwenyezi Mungu wa milele, uliyewapelekea mitume Roho wako Mtakatifu saa hii, umtume kwetu Roho huyo huyo wa upendo, ili tuweze kukushuhudia kiaminifu mbele ya watu wote. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Adhuhuri: Kum.15:7-8
Kama akiwapo mtu maskini pamoja nawe, nduguzo mmojawapo, ndani ya malango yako mojawapo, katika nchi yako akupayo BWANA, Mungu wako, usifanye moyo wako kuwa mgumu, wala usimfumbie mkono wako nduguyo maskini; lakini mfumbulie mkono wako kwa kweli, umkopeshe kwa kweli yatoshayo haja yake katika ahitajiayo.

K. Bwana, umezisikiliza sala za maskini.
W. Utawasikiliza na kuwaimarishia mioyo yao.

SALA:
Tuombe: Ee Mungu Mwenyezi, ulimfumbulia Petro mpango wako wa kuwakomboa watu wote, twakuomba uzipokee kazi zetu ili, kwa neema yako, ziendeleze kusudi lako jema la ukombozi. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Mit.22:22-23
Usimnyang'anye maskini, kwa kuwa ni maskini; Wala usimdhulumu mtu mnyonge langoni; Kwa sababu BWANA atawatetea; Naye atawateka uhai wao waliowateka.

K. Bwana atawaokoa fukara, ambao hawana msaada.
W. Atayaokoa maisha ya maskini.

SALA:
Tuombe: Mungu Mwenyezi, tunakumbuka jinsi ulivyomtuma malaika wako kwa akida Kornelio kumwonesha njia ya wokovu. Ifungue mioyo yetu tupate kuushughulikia wokovu wa dunia kwa ari zaidi, ili Kanisa lako litufikishe sisi na watu wote mbele yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.