Generic placeholder image

JUMANNE JUMA LA 16 LA MWAKA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Bwana ni Mungu Mwenyezi: njooni, tumwabudu.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Usiku umekwisha sasa,
Na sisi twakusifu Baba,
Tumesimama mbele yako,
Wakakamavu tupo macho;
Sala, fikara twatolea,
Twakuabudu kwa kuimba.

Ewe mfalme wa vyote,
Kwa makao yako twandae;
Tuondolee udhaifu,
Tupatie afya na nguvu;
Tuingize mbinguni kwako,
Watakatifu wafurahiko.

Ee Baba, Roho na Mwana,
Mtakatifu sana sana,
E Utatu Mtakatifu,
Tupatie wako wokovu;
Ni wako utukufu wote,
Ung'arao na kuvuma kote.

ANT. I: Ee Bwana, nitakuimbia, na nitatembea katika njia ya ukamilifu.

Zab.101 Mwongozo wa mfalme
Mkinipenda, mtazishika amri zangu (Yoh.14:15)

Utenzi wangu kuhusu uaminifu na haki;*
ninauimba kwa heshima yako, Ee Mungu.

Mwenendo wangu utakuwa bila dosari.*
Je, utakuja kwangu lini?

Nyumbani mwangu nitaishi bila hatia;*
chochote kiovu, kamwe sitakivumilia.

Mienendo ya wale waliomwasi Mungu naichukia,*
mambo yao hayataambatana nami.

Upotovu wowote ule uwe mbali nami;*
nitaachana kabisa na kila baya.

Nitawakomesha wale wanaowasengenya watu;*
sitawavumilia wenye kiburi na majivuno.

Watu walio waaminifu ndio watakaokuwa wenzangu;*
na watumishi wangu watakuwa wasio na uovu.

Mwongo yeyote hatakaa nyumbani mwangu;*
hakuna mnafiki atakayekaa kwangu.

Siku kwa siku nitawakomesha waovu wote;*
nitawaondoa wabaya wote katika jiji la Mungu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Ee Bwana, nitakuimbia, na nitatembea katika njia ya ukamilifu.

ANT. II: Ee Bwana, usiziondoe kwetu fadhili zako.

WIMBO: Dan.3:26,27,29,30,34-41 Sala ya Azaria katika tanuu
Basi, badilisheni mwenendo wenu mbaya, mkamrudie Mungu ili yeye afute dhambi zenu (Mate.3:19)

Umehimidiwa, Ee Bwana,*
MUNGU wa baba zetu,

na jina lako lastahili*
kusifiwa na kutukuzwa milele.

Wala usilitangue agano lako*
na kutuondolea rehema zako,

kwa ajili ya Abrahamu umpendaye,/
na kwa ajili ya Isaka mtumishi wako,*
na Israeli mtakatifu wako,

Ambao uliwaahidia ya kuwa*
utauzidisha uzao wao

kama nyota mbinguni*
na kama mchanga uliopo pwani.

Maana sisi, Ee BWANA,*
tumekuwa duni kuliko mataifa mengine yote,

na kudhulumiwa leo katika ulimwengu wote*
kwa sababu ya dhambi zetu.

Sasa hakuna mfalme*
wala nabii wala kiongozi;

hakuna dhabihu wala kafara*
wala sadaka wala uvumba;

wala mahali pa kukutolea dhabihu*
na kuona rehema.

Lakini kwa moyo uliovunjika/
na kwa roho nyenyekevu*
tukubaliwe nawe,

na sadaka yetu iwe machoni pako leo/
kama dhabihu za kondoo waume na ng'ombe,*
na kama kondoo wanono elfu kumi.

Nasi tukufuate kwa unyofu,*
maana wanaokutumainia Wewe hawataaibika.

Na sasa tunakufuata kwa moyo wote;*
tunakucha, na kuutafuta uso wako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Ee Bwana, usiziondoe kwetu fadhili zako.

ANT. III: Nitakuimbia wimbo mpya, Ee Mungu.

Zab.144:1-10 Shukrani kwa ushindi
Naweza kuikabili kila hali, kwani Kristo hunipa nguvu (Filp.4:13)

Atukuzwe Mungu, 'mwamba wa usalama wangu,/
aipaye mikono yangu mazoezi ya vita,*
na kuvifunza vidole vyangu mapambano.

Yeye ndiye kinga yangu amini,*
ngome yangu, usalama wangu na mwokozi wangu.

Yeye ni ngao yangu ninayotegemea;*
huyashinda mataifa na kuyaweka chini yangu.

Ee Mungu, mtu ni nini hata umwangalie?*
Mwanadamu ni nini hata umkumbuke?

Binadamu ni kama pumzi tu;*
siku zake ni kama kivuli kipitacho.

Ee Mungu, pasua mbingu ushuke!*
Uiguse milima, nayo itoe moshi!

Lipusha umeme, uwatawanye adui;*
upige mishale yako, uwahangaishe!

Unyoshe mkono wako kutoka juu,*
uniokoe na kuniondoa katika maji haya mengi;

uniopoe katika makucha ya wageni,/
ambao maneno yao yote ni ya uwongo,*
na hushuhudia uwongo kwa kiapo.

Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya;*
nitakupigia kinubi cha nyuzi kumi,

wewe uwapaye wafalme ushindi,*
na kumwokoa Daudi, mtumishi wako!

Uniepushe na upanga wa adui katili;*
uniopoe katika makucha ya wageni,

ambao maneno yao yote ni ya uwongo,*
na hushuhudia uwongo kwa kiapo.

Naam, wana wetu katika ujana wao,*
wawe kama mimea inayokua vizuri.

Binti zetu wawe kama nguzo za pembeni,*
zilizochongwa vizuri ili kupamba Hekalu.

Ghala zetu zijae mazao ya kila aina.*
Kondoo wetu mashambani wazae maelfu na maelfu.

Mifugo yetu iwe na afya na nguvu;/
isitupe mimba wala kuzaa kabla ya wakati.*
Kusiwepo tena udhalimu katika mitaa yetu.

Heri taifa ambalo limejaliwa hayo!*
Heri taifa ambalo Mungu wao ni Mungu!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Nitakuimbia wimbo mpya, Ee Mungu.

SOMO: Isa.55:1
Haya, kila aonaye kiu, njoni majini, Naye asiye na fedha; nunueni mle; Naam, njoni, nunueni divai na maziwa, Bila fedha na bila thamani.

KIITIKIZANO
K. Sikia kilio changu, Ee Bwana, maana nalitumainia neno lako. (W. Warudie)
K. Naamka kabla ya alfajiri na kuomba msaada.
W. Nalitumainia neno lako.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Sikia...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Bwana, utuokoe mikononi mwao wote wanaotuchukia.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Bwana, utuokoe mikononi mwao wote wanaotuchukia.

MAOMBI
Mateso yetu yanatufanya tukubalike; kukubalika kwetu kunatuletea matumaini: na matumaini yetu hayatatudanganya, kwa kuwa tumejazwa Roho Mtakatifu mioyoni mwetu. Kwa njia ya Roho huyo, tuombe:
W. Bwana, uwe nasi katika safari yetu.

Utuwezeshe kutambua kuwa matatizo yetu ni mepesi na ya kupita;
- kwani hayo si kitu, yakilinganishwa na furaha tutakayopata tufikapo mbinguni. (W.)

Uwafariji walio pweke, wasiopendwa na wasio na marafiki;
- uwaoneshe upendo wako, na uwasaidie waweze kuwatunza ndugu zao. (W.)

Utuondolee majivuno, itulize hasira yetu:
- ili tuweze kukufuata kwa upole na unyenyekevu wa moyo. (W.)

Utujalie utimilifu wa Roho wako, ili tuwe wana wako;
- uyafanye mapendo kati yetu yawe ya ukarimu na kweli. (W.)


Sala ya Baba yetu:
K. Bwana utukumbuke katika utawala wako, kwa kuwa kwa kufuata mafundisho yako tunasali: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana, utuongezee imani, ili masifu haya tunayokutolea yazae daima matunda yake yatokayo mbinguni. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.