Generic placeholder image

JUMANNE JUMA LA 16 LA MWAKA
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Kabla haijaisha
Siku yetu, Ee Bwana
Sisi twakuomba Wewe:
Kwa huo wako upendo
Endelea kutulinda
Watu wako tulo hapa.

Tupe usiku wa leo
Usingizi mtulivu,
Uziimarishe upya
Nguvu zetu imarisha;
Mng'ao wako ufute
Giza lote la adui.

Hamu ya mioyo yetu
Wewe Bwana kukupenda,
Utulinde basi sisi
Tuwapo usingizini,
Ili kukipambazuka
Masifu tukuimbie.

Sifa yote iwe kwako
Kwako, Ee Kristo,'
Meponya watu na kifo-
Ili nawe washiriki
Upendo wake Babako,
Kuishi katika Roho.

ANT. I: Nikikusahau wewe, Yerusalemu, mkono wangu wa kuume na unyauke!

Zab.137:1-6 Ombolezo ugenini
Huu utumwa wa kimwili wa watu lazima ueleweke kuwa ni kielelezo cha utumwa wao wa kiroho (Mt.Hilari)

Kando ya mito ya Babuloni, tulikaa,*
tukawa tunalia tulipokumbuka Sion.

Katika miti ya huko nchini,*
tulitundika vinubi vyetu.

Waliotuchukua mateka walitutaka tuwaimbie;/
watesi wetu walitutaka tuwafurahishe:*
"Tuimbieni wimbo juu ya Sion!"

Tutaimbaje wimbo wa kumsifu Mungu*
mbali, katika nchi ya kigeni?

Ewe Yerusalemu, kama nikikusahau,*
basi, mkono wangu wa kulia ukatike!

Nikithamini kitu kingine zaidi kuliko wewe Yerusalemu,/
nisipokukumbuka wewe;*
basi, ulimi wangu uwe mzito, niwe bubu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Nikikusahau wewe, Yerusalemu, mkono wangu wa kuume na unyauke!

ANT. II: Mbele ya malaika nitakusifu, Ee Mungu wangu.

Zab.138 Sala ya shukrani
Wafalme wa dunia watauletea mji mtakatifu utukufu na heshima (Ufu.21:24)

Nakushukuru, Ee Mungu, kwa moyo wangu wote,*
nitaimba sifa zako mbele ya miungu.

Nitasujudu kuelekea Hekalu lako takatifu;/
nitakusifu kwa upendo wako mkuu na uaminifu wako.*
Kwa sababu umekuza ahadi yako na jina lako.

Nilipokulilia ulinisikiliza;*
kwa nguvu yako uliniimarisha.

Ee Mungu, wafalme wote duniani watakusifu,*
kwa sababu wamezisikia ahadi zako.

Wataimba sifa za matendo yako, Ee Mungu,*
kwa maana utukufu wako ni mkuu.

Ee Mungu, ingawa wewe uko juu ya wote,/
wawaangalia kwa wema walio wanyonge;*
nao wenye kiburi hawawezi kufichika kwako.

Nizungukwapo na taabu, wewe wanilinda;/
wanyosha mkono wako dhidi ya adui zangu wakali,*
na kwa nguvu yako kuu wanisalimisha.

Ee Mungu, utatimiza yote uliyoniahidi./
Ee Mungu, upendo wako mkuu ni wa milele.*
Uikamilishe kazi yako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Mbele ya malaika nitakusifu, Ee Mungu wangu.

ANT. III: Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kupokea utukufu na heshima.

WIMBO: Ufu.4:11;5:9,10,12 Wimbo wa waliookolewa
Wewe ni Bwana na Mungu wetu,*
unastahili utukufu na heshima na nguvu;

maana wewe uliumba vitu vyote,/
na kwa matakwa yako* kila kitu kimepewa uhai na uzima.

Wewe unastahili kukitwaa hicho kitabu*
na kuivunja mihuri yake,

kwa sababu wewe umechinjwa,/
na kwa damu yako umemnunulia Mungu*
watu kutoka katika kila kabila, lugha, jamaa na taifa.

Wewe umewafanya wawe ufalme wa makuhani/
wamtumikie Mungu wetu,*
nao watatawala duniani.

Mwanakondoo aliyechinjwa*
anastahili kupokea

uwezo, utajiri, hekima,*
nguvu, heshima, utukufu na sifa.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kupokea utukufu na heshima.

SOMO: Kol.3:16
Ujumbe wa Kristo ukae ndani yenu pamoja na utajiri wake wote. Fundishaneni na kushauriana kwa hekima yote. Imbeni zaburi, nyimbo na tenzi za kiroho; mwimbieni Mungu mioyoni mwenu kwa shukrani.

KIITIKIZANO
K. Utanijalia utimilifu wa furaha mbele yako, Ee Bwana. (W. Warudie)
K. Nitafurahi milele kuumeni kwako.
W. Mbele yako, Ee Bwana.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Utanijalia...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Tutendee makuu, Ee Bwana, kwa kuwa u mwenye nguvu, na jina lako ni Takatifu.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Tutendee makuu, Ee Bwana, kwa kuwa u mwenye nguvu, na jina lako ni Takatifu.

MAOMBI
Kristo alitufundisha kuielekeza mioyo yetu kwenye Utawala wa Mungu na hukumu zake. Katika Utawala huo tutapewa yote tunayohitaji. Tunaposubiri hayo, tuombe:
W. Utawala wako uje, Ee Bwana.

Heri wale wanaotambua kwamba wanamhitaji Mungu:
- utuongoze tukutafute Wewe kwa moyo safi. (W.)

Heri wale wafanyao kazi bila kutazamia malipo; heri wale watesekao kwa ajili ya kutetea haki:
- uwatulize na kuwapunguzia uzito wa mizigo yao. (W.)

Heri walio wapole, wenye huruma na wenye kusamehe;
- maana watasamehewa nawe siku ya mwisho. (W.)

Heri wapatanishi na wapenda amani:
- maana hao ni kweli wana wa Mungu. (W.)

Uwafariji wote wenye uchungu wa kufiwa:
- uwawezeshe kushiriki tumaini la heri ya wale wote waliokufa katika amani ya Kristo. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Kufuatana na mafundisho ya Bwana wetu, kwa imani na matumaini tunasali: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Tunaposali mbele yako, Ee Bwana, tunakuomba, kwa huruma yako, neema ya kutafakari daima mioyoni mwetu yale tunayotangaza kwa vinywa vyetu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.