Generic placeholder image

JUMANNE JUMA LA 16 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Baba wa milele, Mungu wa pendo,
Ambaye kwa vumbi ulituumba,
Tugeuze kwa neema ya Roho,
Tutie thamani tulio duni.

Utuandae kwa siku ya siku.
Atakapokuja Kristo kwa enzi
Kutugeuza tena toka vumbi
Na miili yetu kuing'arisha.

E Mungu, hujaonwa, hujaguswa,
Viumbe vyote vyakudhihirisha;
Mbegu ya utukufu ndani mwetu
Itachanua tutapokuona.

ANT. I: Kwa kuwa mwajua anachotaka Mungu, ishini kadiri ya matakwa yake, nanyi mtabarikiwa.

Zab.119:137-144 XVIII Sheria ya Mungu ni adili
Ee Mungu, wewe ni mwadilifu;*
na hukumu zako ni za adili.

Kanuni ulizoweka*
ni za haki na sawa.

Ndani mwangu nawaka hasira kama moto,*
maana adui zangu hawajali maagizo yako.

Ahadi yako ni hakika kabisa,*
nami mtumishi wako naipenda.

Mimi ni mdogo, nadharauliwa;*
hata hivyo sisahau kanuni zako.

Uadilifu wako wadumu milele;*
sheria yako ni ya kweli.

Taabu na huzuni vimenipata,*
lakini maagizo yako yaniletea furaha.

Maagizo yako ni ya haki daima;*
unijalie maarifa nipate kuishi.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Kwa kuwa mwajua anachotaka Mungu, ishini kadiri ya matakwa yake, nanyi mtabarikiwa.

ANT. II: Ee Bwana, maombi yangu na yafike mbele yako.

Zab.88 Kilio cha msaada
Huu ndio wakati wenu hasa, ndio wakati wa utawala wa giza (Lk.22:53)

I
Ee Mungu, Mungu mwokozi wangu,/
ninalia mchana kutwa,*
usiku nakulalamikia.

Sala yangu ikufikie;*
usikilize kilio changu.

Maafa mengi yamenipata,*
hata niko karibu kufa.

Niko sawa na wote wanaokufa;*
nguvu zangu zote zimeniishia.

Nimesahauliwa kati ya wafu,*
kama waliouawa, waliomo kaburini;

wale ambao huwakumbuki tena,*
ambao wametengwa na ulinzi wako.

Umenitupa katika kina cha kaburi;*
katika sehemu za giza na kina kikuu.

Hasira yako imenilemea;*
umenisonga kwa mawimbi yako yote.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Ee Bwana, maombi yangu na yafike mbele yako.

ANT. III: Ee Bwana, nakusihi unisaidie: usinifiche uso wako.

II
Umenitenga na rafiki zangu,/
umenifanya kuwa chukizo kwao.*
Nimefungwa ndani, wala siwezi kutoroka;

macho yangu yamevimba kwa huzuni./
Kila siku nakulilia, Ee Mungu;*
nakunyoshea mikono yangu.

Wafu hawafaidiki kwa miujiza yako!*
Mizimu haifufuki na kukusifu!

Je, upendo wako mkuu unatajwa kaburini,*
au uaminifu wako kwenye makao ya wafu?

Je, miujiza yako inajulikana humo gizani,*
au wema wako kwa hao waliosahauliwa?

Mimi lakini, nakulilia, Ee Mungu;*
kila asubuhi nakuletea ombi langu.

Kwa nini, Ee Mungu, wanitupilia mbali?*
Kwa nini umegeukia mbali nami?

Nimeteseka na kukaribia kifo tangu ujana wangu;*
niko hoi kabisa, nateseka kwa mapigo yako.

Hasira yako kali imeniwakia:*
mashambulio yako ya kutisha yananiangamiza.

Yananizunguka kama mafuriko mchana kutwa;*
yananizingira yote kwa pamoja.

Umenitenga na rafiki na wenzangu wote;*
giza ndilo lililonibakia, sina mwingine.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Ee Bwana, nakusihi unisaidie: usinifiche uso wako.

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: 1Yoh.3:17-18
Mtu akiwa na mali za hapa duniani, halafu akamwona ndugu yake ana shida, lakini akawa na moyo mgumu bila kumwonea huruma, anawezaje kusema kwamba anampenda Mungu? Watoto wangu, upendo wetu usiwe maneno matupu, bali uwe upendo wa kweli na wa vitendo.

K. Heri mtu yule aliye na huruma na fadhili.
W. Atakumbukwa milele.

SALA:
Tuombe: Mungu Mwenyezi wa milele, uliyewapelekea mitume Roho wako Mtakatifu saa hii, umtume kwetu Roho huyo huyo wa upendo, ili tuweze kukushuhudia kiaminifu mbele ya watu wote. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Adhuhuri: Kum.30:11,14
Maagizo haya nikuagizayo leo, si mazito mno kwako, wala si mbali. Lakini neno li karibu nawe sana, li katika kinywa chako na moyo wako, upate kulifanya.

K. Neno lako, Ee Bwana, laimulikia miguu yangu.
W. Lanionesha njia inipasayo kupita.

SALA:
Tuombe: Ee Mungu Mwenyezi, uliyemfumbulia Petro mpango wako wa kuwakomboa watu wote, twakuomba uzipokee kazi zetu, ili kwa neema yako, ziendeleze kusudi lako jema la ukombozi. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Isa.55:10-11
Kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye, mbegu, na mtu alaye, chakula; ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.

K. Bwana amepeleka neno lake duniani.
W. Amri zake zaenea upesi.

SALA:
Tuombe: Mungu Mwenyezi, tunakumbuka jinsi ulivyomtuma malaika wako kwa akida Kornelio kumwonesha njia ya wokovu. Ifungue mioyo yetu tupate kuushughulikia wokovu wa dunia kwa ari zaidi, ili Kanisa lako litufikishe sisi na watu wote mbele yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.