JUMANNE JUMA 1 LA KWARESIMA
MASOMO

SOMO 1: Isa.55:10-11
Bwana asema: kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula; ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.34:3-6,15-18
1. Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
Nalimtafuta Bwana akanijibu,
Akaniponya na hofu zangu zote.

(K) Wenye haki, Bwana anawaponya na taabu zao zote.

2. Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
Wala nyuso zao hazitaona haya.
Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
Akamwokoa na taabu zake zote. (K)

3. Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki,
Na masikio yake hukielekea kilio chao.
Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya,
Aliondoe kumbukumbu lao duniani. (K)

4. Walilia, naye Bwana akasikia,
Akawaponya na taabu zao zote.
Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo,
Na waliopondeka roho huwaokoa. (K)

SHANGILIO: Zab.95:8
Leo msifanye migumu mioyo yenu, lakini msikie sauti yake Bwana.

INJILI: Mt.6:7-15
Siku ile Yesu aliwaambia wafuasi wake: mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi. Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba. Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni. Utupe leo riziki yetu. Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu. Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. [Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.] Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.

MAOMBI
Ndugu zangu, Yesu Kristo anatukataza tusifanye mambo mema kwa ajili ya sifa za watu, tupate kupendwa au kulipwa nao. Kwa hiyo, tumwombe msaada wake. Ee Bwana Yesu twakuomba:

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uzidi kulijalia Kanisa lako wachungaji wenye bidii ya kulitangaza neno lako na wote wanaolisikia neno lako walitendee kazi kwa kuliishi kiaminifu. Ee Bwana.

2. Utujalie imani thabiti katika nia yako njema ya kutukomboa kwa njia ya mateso, ili nasi tukawatendee wenzetu wanaohitaji majitoleo yetu. Ee Bwana.

3. Usituache tushawishike kutenda kinyume cha matakwa yako; na utulinde dhidi ya wote wenye kutudhuru. Ee Bwana.

4. Uwasamehe makosa yao ndugu zetu marehemu, ili wastahili kushiriki utukufu wako huko mbinguni. Ee Bwana.

Tunaomba hayo kwako wewe unayeishi na kutawala daima na milele. Amina.