JUMANNE JUMA 2 LA KWARESIMA
MASOMO
SOMO 1: Isa.1:10,16-20
Lisikieni neno la Bwana, enyi waamuzi wa Sodoma; tegeni masikio msikie sheria ya Mungu wetu,
enyi watu wa Gomora. Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho
yangu; achene kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa;
mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane. Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu
zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera,
zitakuwa kama sufu. Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; bali kama mkikataa na kuasi
mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha Bwana kimenena haya.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.50:8-9,16-17,21,23(K)23
1. Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako,
Na kafara zako ziko mbele yangu daima.
Sitatwaa ng’ombe katika nyumba yako,
Wala beberu katika mazizi yako.
(K) Autengenezaye mwenendo wake, Nitamwonesha wokovu wangu.
2. Una nini wewe kuitangaza sheria yangu,
Na kuliweka agano langu kinywani mwako?
Maana wewe umechukia maonyo,
Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako. (K)
3. Ndivyo ulivyofanya, nami nikanyamaza,
Ukadhani ya kuwa Mimi ni kama wewe,
Atoaye dhabihu za kushukuru, ndiye anayenitukuza.
Naye autengenezaye mwenyendo wake,
Nitamwonesha wokovu wa Mungu. (K)
SHANGILIO: Mt.4:17
Tubuni asema Bwana, kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.
INJILI: Mt.23:1-12
Yesu aliwaambia makutano na wanafunzi wake, akasema, Waandishi na Mafarisayo wameketi katika
kiti cha Musa; basi, yoyote watakayowaambia, myashike, na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo
yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi. Wao hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu
mabegani mwao; wasitake wenyewe kuigusa kwa kidole chao. Tena matendo yao yote huyatenda ili
kutazamwa na watu; kwa kuwa hupanua hirizi zao, huongeza matamvua yao; hupenda viti vya mbele
katika karamu, na kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni, na kuitwa na watu, Rabi.
Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu. Wala msimwite mtu baba
duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni. Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu
ni mmoja, naye ndiye Kristo. Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu. Na yeyote atakayejikweza
atadhiliwa; na yeyote atakayejidhili atakwezwa.
MAOMBI
Ee Mungu uwakwezaye wanyenyekevu na kuwashusha wenye kiburi, twakuomba:
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uzidi kuwapa moyo wa uwajibikaji wahubiri wote wa neno lako, ili wasiache hata mara moja kukemea maovu
ya dunia hii.
2. Watu wote duniani wafungue mioyo na masikio yao wapate kuusikiliza mwaliko wako wa toba hasa katika Kipindi
hiki cha Kwaresima.
3. Umpe kila mmoja wetu tamaa ya kujiosha, kujitakasa na hivi kuondoa uovu bila kuogopa au kujali uzito wa
dhambi zetu.
4. Utuepushe na unafiki wa kifarisayo, ili kila mmoja wetu abebe mzigo wake na kupewa heshima anayostahili
mbele yako.
Ee Mwenyezi Rahimu, twanyenyekea mbele yako; na hivi twakuomba utupokee kama wanafunzi wa Mwalimu mmoja
na watoto wa Baba mmoja. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.