JUMANNE JUMA LA 2 MAJILIO
MASIFU YA ASUBUHI
K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.
ANTIFONA YA MWALIKO:
Tumwabudu Bwana, mfalme atakayekuja.
(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)
Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)
Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)
Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)
Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)
Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)
UTENZI
Sikieni sauti ya mjumbe
'Kristo yu karibu', yasema,
'Tupieni mbali za giza ndoto,
Na mkaribisheni Kristo,
Yeye aliye nuru ya mchana!'
Roho iloshikana na dunia
Iamshwe na hilo onyo kali;
Yesu Kristo ni lake jua,
Liondoalo ulegevu wote,
Asubuhi uwinguni hung'aa.
Basi na atakapokuja tena
Kwa utukufu na vitisho vingi,
Na kuifunika hofu dunia,
Na atokee katika mawingu
Aje na kuwa wetu mtetezi.
ANT. I: Ee Bwana, niletee nuru yako na kweli yako.
Zab.43 Sala ya mkimbizi yaendelea
Mimi ni mwanga, nami nimekuja ulimwenguni ili wote wanaoniamini wasibaki gizani
(Yoh.12:46)
Uwe upande wangu, Ee Mungu;*
unitetee haki zangu;
unikinge na watu wanaokuchukia,*
watu waongo na waovu.
Wewe Mungu wangu, uliye nguvu yangu,*
kwa nini umenitupilia mbali?
Mbona naendelea kuteseka,*
nikisumbuliwa na adui zangu?
Upeleke mwanga wako na ukweli wako,*
vipate kuniongoza na kunipeleka kwako;
mpaka kwenye mlima wako mtakatifu, kwenye makao yako.*
Hapo, Ee Mungu, nitakwenda madhabahuni pako;
nitakuja kwako, Ee Mungu, asili ya furaha yangu.*
Nitakusifu kwa kinubi, Ee Mungu, Mungu wangu.
Mbona ninahuzunika hivyo moyoni?*
Kwa nini nahangaika hivyo?
Nitamtumainia Mungu!*
Nitamsifu tena Mungu, mwokozi wangu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Ee Bwana, niletee nuru yako na kweli yako.
ANT. II: Bwana, uje kutusaidia siku zote za maisha yetu.
WIMBO: Isa.38:10-14,17-20 Kihoro cha mgonjwa mahututi; furaha ya aliyepona.
Nalisema, Katika usitawi wa siku zangu/
nitakwenda kuingia malango ya kuzimu;*
Nimenyimwa mabaki ya miaka yangu.
Nalisema, Sitamwona BWANA, yeye BWANA,*
katika nchi ya walio hai;
Sitamwona mwanadamu tena*
pamoja na hao wakaao duniani.
Kao langu limeondolewa kabisa,*
limechukuliwa kama hema ya mchungaji;
Nimekunja maisha yangu kama mfumaji;*
atanikatilia mbali na kitanda cha mfumi;
Naliomboleza usiku kucha;/
kama simba ameivunja mifupa yangu yote;*
Tangu mchana hata usiku wananimaliza.
Kama mbayuwayu au korongo ndivyo nilivyolia;/
Naliomboleza kama hua;*
macho yangu yamedhoofu kwa kutazama juu;
Ee BWANA, nimeonewa,*
na uwe mdhamini wangu.
Tazama; nalikuwa na uchungu mwingi*
kwa ajili ya amani yangu;
Lakini kwa kunipenda/
umeniokoa na shimo la uharibifu;*
Kwa maana umezitupa dhambi zangu zote nyuma yako.
Kwa kuwa kuzimu hakuwezi kukusifu;*
mauti haiwezi kukuadhimisha;
Wale washukao shimoni*
hawawezi kuitarajia kweli yako.
Aliye hai, naam, aliye hai, /
ndiye atakayekusifu, kama mimi leo;*
Baba atawajulisha watoto kweli yako.
BWANA yu tayari kunipa wokovu.*
Basi, kwa vinubi tutaziimba nyimbo zangu,
Siku zote za maisha yetu*
Nyumbani mwa BWANA.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. II: Bwana, uje kutusaidia siku zote za maisha yetu.
ANT. III: Ee Bwana, wastahili sifa zetu Sion.
Zab.65 Wimbo wa shukrani
Sion ieleweke kuwa ni mji wa Mungu (Origen)
Wastahili sifa, Ee Mungu, katika Sion;*
nasi tutakutimizia nadhiri zetu,
maana wewe wasikiliza sala zetu.*
Watu wote watakujia na kukiri dhambi zao:
dhambi zetu zinapotulemea,*
wewe watuondolea.
Heri uliowachagua wakae patakatifu pako,/
Sisi tutashiba kwa mema ya nyumba yako;*
kwa baraka za Hekalu lako takatifu.
Kwa matendo ya ajabu, Ee Mungu, mkombozi wetu,*
wewe watusikiliza na kutupatia ushindi.
Duniani kote na kupita bahari za mbali,*
watu wakutumainia wewe.
Wewe umejawa nguvu tele tele:*
kwa nguvu yako waisimika milima mahali pake,
watuliza mshindo wa bahari na wa mawimbi yake,*
wakomesha ghasia za watu.
Ulimwengu wote washangazwa na matendo yako./
Wasababisha furaha kila mahali,*
toka mashariki hata magharibi.
Wewe waitunza nchi kwa kuinyeshea mvua,/
waijalia rutuba na kuisitawisha;*
mito yake waijaza maji ya mbinguni,
waifanikisha nchi na kuipatia mavuno.*
Hivi ndivyo ufanyavyo:
Mashamba wayanyeshea mvua kwa wingi,*
na kuyalowanisha kwa maji;
ardhi wailainisha kwa manyunyu,*
na kuibariki mimea ichipue.
Wautunukia mwaka wote mema yako,*
kila ulipopitia pamejaa fanaka.
Mbuga za majani zimejaa mifugo,*
milima nayo imejawa furaha.
Malisho yamejaa kondoo,/
mabonde yamefunikwa kwa ngano.*
Kila kitu kinashangilia kwa furaha.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Ee Bwana, wastahili sifa zetu Sion.
SOMO: Mwa.49:10
Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, wala mfanyasheria kati ya miguu yake, hata atakapokuja
Yeye, mwenye milki, ambaye mataifa watamtii.
KIITIKIZANO
K. Utukufu wa Bwana utakung'aria, Ee Yerusalemu. Kama jua Bwana atachomoza juu yako. (W. Warudie)
K. Utukufu wake utajitokeza katikati yako.
W. Kama jua Bwana atachomoza juu yako.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Utukufu wa Bwana...
Ant. Wimbo wa Zakaria
Furahi na ushangilie, ewe binti Sion. Tazama, nakuja kukaa kati yako, asema Bwana.
WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.
Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.
Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,
kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.
Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.
Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,
ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.
Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,
utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;
kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.
Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,
na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Furahi na ushangilie, ewe binti Sion. Tazama, nakuja kukaa kati yako, asema Bwana.
MAOMBI
Katika ulimwengu uliogawanywa kwa woga na uroho, Kanisa humwita tena Mwokozi wake.
W. Bwana Yesu, utujie kwa upendo.
Utusaidie tuweze kuonesha majuto yetu,
- kwa mwenendo mpya wa maisha. (W.)
Tunapowatangazia wengine nguvu yako ya kuokoa,
- sisi wenyewe tusipoteze wokovu wetu. (W.)
Uiwezeshe dunia yetu kujaa na kufurika neema ya ujio wako:
- utujalie tupate kufurahia utimilifu wa furaha yako. (W.)
Utuwezeshe kuishi kikamilifu hapa duniani,
- na kuyabadili maisha yetu kwa tumaini la utukufu ujao. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Bwana utukumbuke katika utawala wako, kwa kuwa kwa
kufuata mafundisho yako tunasali: Baba Yetu...
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Bwana Mungu, dunia nzima imeuona wokovu wako. Utupe neema ya kungoja kwa furaha siku tukufu ya
kuzaliwa kwake Mwokozi wetu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi
na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.