Generic placeholder image

JUMANNE JUMA LA 2 MAJILIO
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Muumba wa nyota za usiku,
Mwanga wa milele wa taifa,
Mkombozi wetu sisi sote,
Utusikie tukuitapo.

Kwa mwili wa Maria 'likuja,
Tuokoke dhambi na aibu,
Kwa neema yako Mkombozi
Sasa njoo tuponye wadhambi.

Na siku ya hukumu ya mwisho,
Sisi tutakapofufuliwa,
Fika Mkombozi mwenye baraka,
Tupeleke rahani milele.
Irvin Udulutsch OSB

ANT. I: Hamwezi kutumikia Mungu na mali.

Zab.49 Upumbavu wa kutegemea mali
Itakuwa vigumu sana kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa mbinguni (Mt.19:23)

I
Enyi watu wote, sikilizeni jambo hili!*
Tegeni masikio, nyote mnaoishi duniani;

wote, wakubwa kwa wadogo,*
matajiri na fukara.

Maneno yangu yatakuwa mazito mazito;*
mimi nitasema maneno ya hekima.

Nitategea sikio nisikilize mithali,*
na kufafanua maana yake kwa muziki wa kinubi.

Mimi siogopi wakati wa hatari,*
wakati nizungukwapo na adui;

watu waovu wategemeao mali zao,*
na kujisifia wingi wa utajiri wao.

Hakika binadamu hawezi kujikomboa mwenyewe;*
hawezi kumlipa Mungu gharama ya maisha yake,

maana fidia ya maisha ni kubwa mno.*
Hawezi kutoa kitu chochote kinachotosha,

kimwezeshe aendelee kuishi,*
asipate kuonja kaburi.

Wote wajua kwamba hata wenye hekima hufa,/
wapumbavu, hali kadhalika na watu wajinga.*
Wote huwaachia wengine mali zao.

Makaburi ni makao yao hata milele;/
ni makao yao vizazi hata vizazi;*
ingawa hapo awali walikuwa wamemiliki ardhi.

Binadamu hatadumu katika fahari yake;*
atakufa tu kama mnyama.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Hamwezi kutumikia Mungu na mali.

ANT. II: Jiwekeeni hazina yenu mbinguni, asema Bwana.

II
Hayo ndiyo yawapatayo wanaojiamini kipumbavu,*
ndio mwisho wa wale wanaojivunia mali zao.

Watakufa tu kama kondoo,*
kifo kitakuwa mchungaji wao.

Waadilifu wataona fahari juu ya waovu,/
miili yao itakapokuwa ikioza huko kuzimu,*
mbali na nyumba zilizokuwa zao wenyewe.

Lakini mimi, Mungu atanisalimisha;*
ataniokoa na nguvu za kuzimu.

Usihangaike ukiona mtu anatajirika,*
wala mali yake ikiongezeka, zaidi na zaidi.

Atakapokufa hatachukua chochote,*
mali haitashuka kuzimu pamoja naye.

Ajapojikuza katika maisha haya,*
na kusifiwa kwa sababu ya kufanikiwa,

atajiunga tu na wazee wake huko kuzimu,*
ambako giza linatawala milele.

Binadamu hatadumu katika fahari yake.*
atakufa tu kama mnyama.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Jiwekeeni hazina yenu mbinguni, asema Bwana.

ANT. III: Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kupokea utukufu na heshima.

WIMBO: Ufu.4:11;5:9,10,12 Wimbo wa waliookolewa
Wewe ni Bwana na Mungu wetu,*
unastahili utukufu na heshima na nguvu;

maana wewe uliumba vitu vyote,/
na kwa matakwa yako* kila kitu kimepewa uhai na uzima.

Wewe unastahili kukitwaa hicho kitabu*
na kuivunja mihuri yake,

kwa sababu wewe umechinjwa,/
na kwa damu yako umemnunulia Mungu*
watu kutoka katika kila kabila, lugha, jamaa na taifa.

Wewe umewafanya wawe ufalme wa makuhani/
wamtumikie Mungu wetu,*
nao watatawala duniani.

Mwanakondoo aliyechinjwa*
anastahili kupokea

uwezo, utajiri, hekima,*
nguvu, heshima, utukufu na sifa.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kupokea utukufu na heshima.

SOMO: 1Kor.1:7b-9
Mnangojea kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye atawaimarisha ninyi mpaka mwisho, mpate kuonekana bila hatia Siku ile ya Bwana wetu Yesu Kristo. Mungu ni mwaminifu; yeye aliwaita ninyi mwe na umoja na Mwanae Yesu Kristo Bwana wetu.

KIITIKIZANO
K. Bwana, Mungu Mwenyezi, njoo kwetu, utuokoe. (W. Warudie)
K. Utuoneshe uso wa tabasamu, nasi tutakuwa salama.
W. Njoo kwetu, utuokoe.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana, Mungu...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Sauti yalia nyikani: Mtengenezeeni Bwana njia, yanyosheni mapito yake.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Sauti yalia nyikani: Mtengenezeeni Bwana njia, yanyosheni mapito yake.

MAOMBI
Tumwombe Baba yetu atuopoe kutoka dhambini, na atupeleke kwenye uzima mpya.
W. Baba, tunaomba Mwanao atuletee uhuru.

Yohane Mbatizaji alihubiri watu watubu na kugeuza mioyo yao;
- utuondolee ubinafsi. (W.)

Wafarisayo walikataa kuupokea ushuhuda wa Yohane Mbatizaji juu ya ujio wa Mwanao:
- utuondolee woga wa kuukabili ukweli. (W.)

Yohane Mbatizaji alifurahi kumwachia nafasi Mwanao:
- utuondolee majivuno. (W.)

Wafu walitamani kupata uzima wa milele:
- uwaopoe kutoka mautini. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Kufuatana na mafundisho ya Bwana wetu, kwa imani na matumaini tunasali: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, dunia nzima imeuona wokovu wako. Utupe neema ya kungoja kwa furaha siku tukufu ya kuzaliwa kwake Mwokozi wetu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.