Generic placeholder image

JUMANNE JUMA LA 2 MAJILIO
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Njoo Roho Mtakatifu,
Ndani yetu sisi uishi,
Pamoja nawe waje pia
Mungu Baba na Mungu Mwana,
Nazo zako tele neema
Njoo upate tujalia,
Zitufanye watakatifu,
Pia tuwe kitu kimoja.

Imara katika upendo
Na viwe, roho na ulimi,
Yako sifa kuitangaza
Kila mahali duniani,
Na ule upendo jalie-
Ulio mwetu mioyoni-
Mioyo mingine iwashwe
Kutokana na mwako wake.

Ee Mtukufu kabisa
Utatu ulio upendo,
Moyo wake bin-Adamu
Kwa ajili yako 'liumbwa,
Kwako Wewe na iwe sifa
Kwa wimbo usio na mwisho,
Haki yako Wewe pekee
Kwabudiwa hata milele.

Kabla ya Adhuhuri
ANT.: Manabii walitabiri kwamba Mwokozi atazaliwa na bikira.

Adhuhuri
ANT.: Malaika Gabrieli alimwambia Maria: 'Furahi, wewe uliyependelewa sana! Bwana yu pamoja nawe. Umebarikiwa kuliko wanawake wote.'

Baada ya Adhuhuri
ANT.: Maria alihangaishwa sana na amkio hilo, akajiuliza: 'Salamu hii ina maana gani?' Akawaza: 'Nitamzaa Mfalme bila kupoteza ubikira!'

Zab.119:49-56 VII Kuwa na imani na sheria ya Mungu
Ukumbuke ahadi yako kwangu mimi mtumishi wako,*
ahadi ambayo imenipa matumaini.

Hata niwapo taabuni napata kitulizo,*
maana ahadi yako yanipa uhai.

Wenye kiburi hunidharau daima,*
lakini mimi sikiuki sheria yako.

Ninapoyakumbuka maagizo yako ya tangu kale,*
nafarijika, Ee Mungu.

Nashikwa na hasira kali,*
nionapo waovu wakivunja sheria zako.

Nikiwa huku ugenini,*
tenzi zangu ni juu ya amri zako.

Usiku ninakukumbuka, Ee Mungu,*
na kuzingatia sheria zako.

Hii ni baraka kubwa kwangu,*
kwamba nazishika amri zako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.53 Mtu asiyemcha Mungu
Watu wote wametenda dhambi, na wametindikiwa utukufu wa Mungu (Rom.3:23)

Wapumbavu hujisemea: "Hakuna Mungu!"/
Wote wamepotoka, wametenda mambo ya kuchukiza;*
hakuna hata mmoja atendaye jema.

Toka mbinguni Mungu awachungulia wanadamu,/
aone kama kuna yeyote mwenye busara,*
kama kuna mtu yeyote anayemcha Mungu.

Lakini wote wamepotoka,/
wote kwa pamoja wameharibika,*
hakuna atendaye mema, hakuna hata mmoja.

Mungu asema,“Je, hao watendao maovu hawana akili?"*
Wanawamaliza watu wangu,

kama kwamba wanakula mikate;*
tena hawamchi Mungu!"

Hapo, watetemeka kwa hofu,*
hofu ambayo hawajapata kuiona;

maana Mungu ataitawanya mifupa ya adui.*
Hao watashindwa, maana Mungu amewaacha.

Laiti ukombozi wa Israeli*
ungefika kutoka Sion!

Mungu atakapowafanikisha tena watu wake,*
Israeli atafurahi, na Yakobo atashangilia.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.54:1-4,6-7 Sala ya kujikinga na maadui
Nabii anaomba ili kwa jina la Bwana aokolewe na uovu wa wale wanaomdhulumu (Kasiani)

Uniokoe, Ee Mungu, kwa jina lako;*
unisalimishe kwa enzi yako.

Uisikie, Ee Mungu, sala yangu;*
uyapokee maneno yangu.

Watu wenye kiburi wananishambulia;/
wakatili wanayawinda maisha yangu,*
watu wasiomjali kamwe Mungu.

Lakini Mungu ni msaada wangu,*
Bwana hutegemeza maisha yangu.

Kwa moyo radhi nitakutolea sadaka;*
nitalisifu jina lako kwa kuwa wewe ni mwema.

Maana umeniokoa katika taabu zangu zote,*
nami nimewaona adui zangu wameshindwa.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Kabla ya Adhuhuri
ANT.: Manabii walitabiri kwamba Mwokozi atazaliwa na bikira.

Adhuhuri
ANT.: Malaika Gabrieli alimwambia Maria: 'Furahi, wewe uliyependelewa sana! Bwana yu pamoja nawe. Umebarikiwa kuliko wanawake wote.'

Baada ya Adhuhuri
ANT.: Maria alihangaishwa sana na amkio hilo, akajiuliza: 'Salamu hii ina maana gani?' Akawaza: 'Nitamzaa Mfalme bila kupoteza ubikira!'

MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: Yer.23:5
Tazama siku zinakuja, asema BWANA, nitakapomchipushia Daudi Chipukizi la haki; naye atamiliki mfalme, atatenda kwa hekima, naye atafanya hukumu na haki katika nchi.

K. Mataifa yatalicha jina lako, Bwana.
W. Na wafalme wote wa dunia watatukuza utukufu wako.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Adhuhuri: Yer.23:6
Katika siku zake Yuda ataokolewa, na Israeli atakaa salama; na jina lake atakaloitwa ni hili, BWANA ni haki yetu.

K. Utukumbuke, Ee Bwana, kwa upendo wako ulio nao kwa watu wako.
W. Njoo, utuokoe.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Eze.34:15-16
Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo zangu, nami nitawalaza, asema Bwana MUNGU. Nami nitawatafuta waliopotea, nitawarudisha waliofukuzwa, nitawafunga waliovunjika, nitawatia nguvu wagonjwa; nao wanono na wenye nguvu nitawaharibu; nitawalisha hukumu.

K. Njoo, Ee Bwana, usikawie.
W. Uwafungue watu wako kutoka dhambi zao.

SALA:
Tuombe: Bwana Mungu, dunia nzima imeuona wokovu wako. Utupe neema ya kungoja kwa furaha siku tukufu ya kuzaliwa kwake Mwokozi wetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.