JUMANNE JUMA LA 34
MASIFU YA JIONI
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
Kabla haijaisha
Siku yetu, Ee Bwana
Sisi twakuomba Wewe:
Kwa huo wako upendo
Endelea kutulinda
Watu wako tulo hapa.
Tupe usiku wa leo
Usingizi mtulivu,
Uziimarishe upya
Nguvu zetu imarisha;
Mng'ao wako ufute
Giza lote la adui.
Hamu ya mioyo yetu
Wewe Bwana kukupenda,
Utulinde basi sisi
Tuwapo usingizini,
Ili kukipambazuka
Masifu tukuimbie.
Sifa yote iwe kwako
Kwako, Ee Kristo,'
Meponya watu na kifo-
Ili nawe washiriki
Upendo wake Babako,
Kuishi katika Roho.
ANT. I: Hamwezi kutumikia Mungu na mali.
Zab.49 Upumbavu wa kutegemea mali
Itakuwa vigumu sana kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa mbinguni (Mt.19:23)
I
Enyi watu wote, sikilizeni jambo hili!*
Tegeni masikio, nyote mnaoishi duniani;
wote, wakubwa kwa wadogo,*
matajiri na fukara.
Maneno yangu yatakuwa mazito mazito;*
mimi nitasema maneno ya hekima.
Nitategea sikio nisikilize mithali,*
na kufafanua maana yake kwa muziki wa kinubi.
Mimi siogopi wakati wa hatari,*
wakati nizungukwapo na adui;
watu waovu wategemeao mali zao,*
na kujisifia wingi wa utajiri wao.
Hakika binadamu hawezi kujikomboa mwenyewe;*
hawezi kumlipa Mungu gharama ya maisha yake,
maana fidia ya maisha ni kubwa mno.*
Hawezi kutoa kitu chochote kinachotosha,
kimwezeshe aendelee kuishi,*
asipate kuonja kaburi.
Wote wajua kwamba hata wenye hekima hufa,/
wapumbavu, hali kadhalika na watu wajinga.*
Wote huwaachia wengine mali zao.
Makaburi ni makao yao hata milele;/
ni makao yao vizazi hata vizazi;*
ingawa hapo awali walikuwa wamemiliki ardhi.
Binadamu hatadumu katika fahari yake;*
atakufa tu kama mnyama.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Hamwezi kutumikia Mungu na mali.
ANT. II: Jiwekeeni hazina yenu mbinguni, asema Bwana.
II
Hayo ndiyo yawapatayo wanaojiamini kipumbavu,*
ndio mwisho wa wale wanaojivunia mali zao.
Watakufa tu kama kondoo,*
kifo kitakuwa mchungaji wao.
Waadilifu wataona fahari juu ya waovu,/
miili yao itakapokuwa ikioza huko kuzimu,*
mbali na nyumba zilizokuwa zao wenyewe.
Lakini mimi, Mungu atanisalimisha;*
ataniokoa na nguvu za kuzimu.
Usihangaike ukiona mtu anatajirika,*
wala mali yake ikiongezeka, zaidi na zaidi.
Atakapokufa hatachukua chochote,*
mali haitashuka kuzimu pamoja naye.
Ajapojikuza katika maisha haya,*
na kusifiwa kwa sababu ya kufanikiwa,
atajiunga tu na wazee wake huko kuzimu,*
ambako giza linatawala milele.
Binadamu hatadumu katika fahari yake.*
atakufa tu kama mnyama.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. II: Jiwekeeni hazina yenu mbinguni, asema Bwana.
ANT. III: Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kupokea utukufu na heshima.
WIMBO: Ufu.4:11;5:9,10,12 Wimbo wa waliookolewa
Wewe ni Bwana na Mungu wetu,*
unastahili utukufu na heshima na nguvu;
maana wewe uliumba vitu vyote,/
na kwa matakwa yako*
kila kitu kimepewa uhai na uzima.
Wewe unastahili kukitwaa hicho kitabu*
na kuivunja mihuri yake,
kwa sababu wewe umechinjwa,/
na kwa damu yako umemnunulia Mungu*
watu kutoka katika kila kabila, lugha, jamaa na taifa.
Wewe umewafanya wawe ufalme wa makuhani/
wamtumikie Mungu wetu,*
nao watatawala duniani.
Mwanakondoo aliyechinjwa*
anastahili kupokea
uwezo, utajiri, hekima,*
nguvu, heshima, utukufu na sifa.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kupokea utukufu na heshima.
SOMO: Rom.3:23-25a
Watu wote wametenda dhambi, na wametindikiwa utukufu wa Mungu. Lakini kwa zawadi ya neema
ya Mungu, watu wote hufanywa wawe na uhusiano mwema naye kwa njia ya Kristo Yesu
anayewakomboa. Mungu alimtoa yeye kusudi, kwa damu yake, awe njia ya kuwaondolea watu
dhambi zao kwa imani yao kwake.
KIITIKIZANO
K. Utanijalia utimilifu wa furaha mbele yako, Ee Bwana. (W. Warudie)
K. Nitafurahi milele kuumeni kwako.
W. Mbele yako, Ee Bwana.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Utanijalia...
Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Tutendee makuu, Ee Bwana, kwa kuwa u mwenye nguvu, na jina lako ni Takatifu.
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.
Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.
Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,
kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Tutendee makuu, Ee Bwana, kwa kuwa u mwenye nguvu, na jina lako ni Takatifu.
MAOMBI
Kristo ni mchungaji wa kondoo wake: huwapenda na kuwatunza watu wake. Tuweke matumaini yetu kwake, na tuseme:
W. Bwana, twakuomba ututunze.
Kristo Bwana wetu, wewe ni mchungaji wa milele,
- uwalinde Askofu wetu F..., na wachungaji wote wa Kanisa lako. (W.)
Uwe na wale wanaoteswa kwa sababu ya imani yao, na wale wanaokosa huduma za Kanisa:
- Mchungaji Mwema, uwatunze hao katika mateso na dhiki yao. (W.)
Uwaponye wagonjwa;
- uwalishe wenye njaa. (W.)
Tunawaombea wale wanaotunga sheria na kuzitumia:
- Bwana, uwajalie hekima, busara na ufahamu. (W.)
Uwakusanye kondoo wako uliokufa kwa ajili yao:
- uwaingize nyumbani mwa Baba yao, wote waliokufa katika amani yako. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Kufuatana na mafundisho ya Bwana wetu, kwa imani na
matumaini tunasali: Baba Yetu...
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Ee Bwana Mungu, mchana ni wako na usiku ni mali yako: Ujalie, Jua la Haki liangaze daima
mioyoni mwetu, ili hatimaye tuufikie mwanga wako wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana
wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.