Generic placeholder image

JUMANNE JUMA LA 34
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Njoo Roho Mtakatifu,
Ndani yetu sisi uishi,
Pamoja nawe waje pia
Mungu Baba na Mungu Mwana,
Nazo zako tele neema
Njoo upate tujalia,
Zitufanye watakatifu,
Pia tuwe kitu kimoja.

Imara katika upendo
Na viwe, roho na ulimi,
Yako sifa kuitangaza
Kila mahali duniani,
Na ule upendo jalie-
Ulio mwetu mioyoni-
Mioyo mingine iwashwe
Kutokana na mwako wake.

Ee Mtukufu kabisa
Utatu ulio upendo,
Moyo wake bin-Adamu
Kwa ajili yako 'liumbwa,
Kwako Wewe na iwe sifa
Kwa wimbo usio na mwisho,
Haki yako Wewe pekee
Kwabudiwa hata milele.

ANT. I: Nimezishika amri zako uhamishoni.

Zab.119:49-56 VII Kuwa na imani na sheria ya Mungu
Ukumbuke ahadi yako kwangu mimi mtumishi wako,*
ahadi ambayo imenipa matumaini.

Hata niwapo taabuni napata kitulizo,*
maana ahadi yako yanipa uhai.

Wenye kiburi hunidharau daima,*
lakini mimi sikiuki sheria yako.

Ninapoyakumbuka maagizo yako ya tangu kale,*
nafarijika, Ee Mungu.

Nashikwa na hasira kali,*
nionapo waovu wakivunja sheria zako.

Nikiwa huku ugenini,*
tenzi zangu ni juu ya amri zako.

Usiku ninakukumbuka, Ee Mungu,*
na kuzingatia sheria zako.

Hii ni baraka kubwa kwangu,*
kwamba nazishika amri zako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Nimezishika amri zako uhamishoni.

ANT. II: Bwana ataliokoa taifa lake utumwani, nasi tutashangilia.

Zab.53 Mtu asiyemcha Mungu
Watu wote wametenda dhambi, na wametindikiwa utukufu wa Mungu (Rom.3:23)

Wapumbavu hujisemea: "Hakuna Mungu!"/
Wote wamepotoka, wametenda mambo ya kuchukiza;*
hakuna hata mmoja atendaye jema.

Toka mbinguni Mungu awachungulia wanadamu,/
aone kama kuna yeyote mwenye busara,*
kama kuna mtu yeyote anayemcha Mungu.

Lakini wote wamepotoka,/
wote kwa pamoja wameharibika,*
hakuna atendaye mema, hakuna hata mmoja.

Mungu asema,“Je, hao watendao maovu hawana akili?"*
Wanawamaliza watu wangu,

kama kwamba wanakula mikate;*
tena hawamchi Mungu!"

Hapo, watetemeka kwa hofu,*
hofu ambayo hawajapata kuiona;

maana Mungu ataitawanya mifupa ya adui.*
Hao watashindwa, maana Mungu amewaacha.

Laiti ukombozi wa Israeli*
ungefika kutoka Sion!

Mungu atakapowafanikisha tena watu wake,*
Israeli atafurahi, na Yakobo atashangilia.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana ataliokoa taifa lake utumwani, nasi tutashangilia.

ANT. III: Mungu ni msaidizi wangu; Bwana ndiye anayenitegemeza nafsi yangu.

Zab.54:1-4,6-7 Sala ya kujikinga na maadui
Nabii anaomba ili kwa jina la Bwana aokolewe na uovu wa wale wanaomdhulumu (Kasiani)

Uniokoe, Ee Mungu, kwa jina lako;*
unisalimishe kwa enzi yako.

Uisikie, Ee Mungu, sala yangu;*
uyapokee maneno yangu.

Watu wenye kiburi wananishambulia;/
wakatili wanayawinda maisha yangu,*
watu wasiomjali kamwe Mungu.

Lakini Mungu ni msaada wangu,*
Bwana hutegemeza maisha yangu.

Kwa moyo radhi nitakutolea sadaka;*
nitalisifu jina lako kwa kuwa wewe ni mwema.

Maana umeniokoa katika taabu zangu zote,*
nami nimewaona adui zangu wameshindwa.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Mungu ni msaidizi wangu; Bwana ndiye anayenitegemeza nafsi yangu.

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: 1Kor.12:4-6
Vipaji vya kiroho ni vya namna nyingi, lakini Roho avitoaye hivyo ni mmoja. Kuna namna nyingi za kutumikia, lakini Bwana anayetumikiwa ni mmoja. Kuna namna mbalimbali za kufanya kazi ya huduma, lakini Mungu ni mmoja, anayewezesha kazi zote katika wote.

K. Msaada wa Mungu u karibu na wale wamchao.
W. Utukufu wake utafanya maskani katika nchi yetu.

SALA:
Tuombe: Mwenyezi Mungu wa milele, uliyewapelekea mitume Roho wako Mtakatifu saa hii, umtume kwetu Roho huyo huyo wa upendo, ili tuweze kukushuhudia kiaminifu mbele ya watu wote. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Adhuhuri: 1Kor.12:12-13
Kama vile mwili ulivyo mmoja wenye viungo vingi, na viungo hivyo ingawaje ni vingi hufanya mwili mmoja, ndivyo ilivyo pia kwa Kristo. Maana sisi, tukiwa Wayahudi au watu wa mataifa mengine, watumwa au watu huru, sote tumebatizwa kwa Roho mmoja katika mwili huo mmoja; na sote tukanyweshwa Roho huyo mmoja.

K. Baba Mwenyezi, utudumishe katika uaminifu kwa jina lako.
W. Na utujalie tuwe na umoja.

SALA:
Tuombe: Ee Mungu Mwenyezi, uliyemfumbulia Petro mpango wako wa kuwakomboa watu wote, twakuomba uzipokee kazi zetu ili, kwa neema yako, ziendeleze kusudi lako jema la ukombozi. Kwa Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: 1Kor.12:24b,25-26
Mungu mwenyewe ameuweka mwili katika mpango, akakipa heshima zaidi kiungo kile kilichopungukiwa heshima, ili kusiweko na utengano katika mwili, bali viungo vyote vishughulikiane. Kama kiungo kimoja kinaumia, viungo vyote huumia pamoja nacho. Kiungo kimoja kikisifiwa, viungo vingine vyote hufurahi pamoja nacho.

K. Bwana, Mungu wetu, utukusanye kutoka miongoni mwa mataifa.
W. Ili tulitukuze jina lako takatifu.

SALA:
Tuombe: Mungu Mwenyezi, tunakumbuka jinsi ulivyomtuma malaika wako kwa akida Kornelio kumwonesha njia ya wokovu. Ifungue mioyo yetu tupate kuushughulikia wokovu wa dunia kwa ari zaidi, ili Kanisa lako litufikishe sisi na watu wote mbele yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.