Generic placeholder image

JUMAPILI JUMA LA 13 LA MWAKA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Njooni, tumwimbie Bwana; tumfanyie shangwe Mungu anayetuokoa, Aleluya.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI tazama pia AU
Mungu usiye mipaka
Ndanimo Wewe taishi,
E ufufuo na Mwanga,
Utenzi wa asubuhi
Wewe tunakuimbia,
Unyamavu wa usiku
Sasa tunaumaliza.

Jogoo yule wa kwanza
Anapoanza kuwika,
Na vyote viamkapo
Kutoka usingizini,
Ndipo huchipua upya
Uzima na tumaini,
Na rangi huonekana.

Mwumba wa vyote vilivyo,
Kipimo cha vitu vyote
Na mwisho wa vyote hivyo,
E Mungu msamehevu
Sahau makosa yetu,
Na sikia zetu sala
Kabla hatujakwomba.

Sifa iwe kwako Baba,
Mwana, Roho Mtakatifu,
E Utatu Mtakatifu,
Chemchemi ya neema,
Unayetuita sisi
'Toka utovu wa vyote
Tuje kwako tutulie.

AU

Kristo ni Mwokozi wa dunia,
Awapendaye walio safi,
Kisima cha hekima ya mbingu,
Thibitisho la imani yetu
Hifadhi ya tumaini letu,
Silaha za askari wake,
Bwana wa dunia na mbingu,
Afya yetu tunapoishi,
Uzima wetu tunapokufa.

Chini katika kiza kinene,
Alilala kafungwa mfungwa,
Ilipowadia yake saa,
Alifufuka taji kavaa.
Na sasa, mbinguni kisha paa,
Kiti cha enzi amekalia,
Ambacho kamwe hakukiacha;
Hicho ni mali ya Baba yake,
Hicho ni mali yake mwenyewe.

Utukufu wote kwake Baba,
Ambaye peke Hakuzaliwa;
Heshima yote iwe kwa Yesu,
Pekee aliye Mwana wake;
Pia kwa Roho Mtakatifu;
Utatu ulo Mkamilifu.
Vitu vyote haya na vijibu,
Haya jibuni binadamu:
Amin - iwe hivyo - Amina.

ANT. I: Nitakutafuta mapema asubuhi, Ee Mungu, ili nizione nguvu zako, aleluya.

Zab.63:1-8 Hamu ya kuwa pamoja na Mungu
Mtu aliyeacha matendo ya giza, na amtafute Mungu.

Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu;*
nakutafuta kwa moyo.

Roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu,*
nina kiu nawe kama nchi kavu isiyo na maji.

Nina hamu ya kukuona patakatifuni pako,*
ili nione enzi yako na utukufu wako.

Upendo wako mkuu ni bora kuliko maisha,*
kwa hiyo nitakusifu.

Nitakushukuru maisha yangu yote,*
katika sala nitainua mikono yangu.

Roho yangu itafanya karamu na kushiba vinono;*
kwa shangwe nitaimba sifa zako.

Niwapo kitandani ninakukumbuka,*
usiku kucha ninakufikiria;

maana wewe umenisaidia daima.*
Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia.

Roho yangu inaambatana nawe kabisa,*
mkono wako wa kuume wanitegemeza.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Nitakutafuta mapema asubuhi, Ee Mungu, ili nizione nguvu zako, aleluya.

ANT. II: Katikati ya moto, wale watatu waliimba kwa sauti moja: Atukuzwe Mungu, aleluya.

WIMBO: Dan:3.37-88,56 Kila kiumbe kimsifu Bwana
Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote (Ufu.19:5)

Enyi viumbe vyote vya Bwana, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Malaika za Bwana, mhimidini Bwana;*
Enyi mbingu, mhimidini Bwana.

Maji yote yaliyo juu angani, mhimidini Bwana;*
Mawezo yote ya Bwana, mhimidini Bwana.

Jua na mwezi, mhimidini Bwana;*
Nyota za mbinguni, mhimidini Bwana.

Manyunyu yote na ukungu, mhimidini Bwana;*
Pepo zote, mhimidini Bwana.

Moto na hari, mhimidini Bwana;*
Kipupwe na musimu, mhimidini Bwana.

Umande na sakitu, mhimidini Bwana;*
Jalidi na baridi, mhimidini Bwana.

Barafu na theluji, mhimidini Bwana;*
Usiku na mchana, mhimidini Bwana.

Dunia na imhimidi Bwana;*
Imsifu na kumwadhimisha milele.

Milima na vilima, mhimidini Bwana;*
Mimea yote ya nchi, mhimidini Bwana.

Chemchemi, mhimidini Bwana;*
Bahari na mito, mhimidini Bwana.

Nyangumi na vyote viendavyo majini, mhimidini Bwana;*
Ndege zote za angani, mhimidini Bwana.

Hayawani na wanyama wafugwao, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Wanadamu, mhimidini Bwana;*
Bani Israeli, mhimidini Bwana.

Makuhani wa Bwana, mhimidini Bwana;*
Watumishi wa Bwana, mhimidini Bwana.

Roho na nafsi zao wenye haki, mhimidini Bwana;*
Watakatifu na wanyenyekevu moyoni, mhimidini Bwana.

Enyi Anania, Azaria, na Misaeli, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Tumtukuze Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Umehimidiwa katika anga la mbinguni,*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Ant. II: Katikati ya moto, wale watatu waliimba kwa sauti moja: Atukuzwe Mungu, aleluya.

ANT. III: Wana wa Sion wamshangilie mfalme wao, aleluya.

Zab.149 Wimbo wa ushindi
Wana wa Kanisa, taifa jipya la Mungu, watashangilia katika Kristo, mfalme wao (Hesychius)

Mwimbieni Mungu wimbo mpya,*
msifuni kati ya jamii ya watu wake waaminifu!

Furahi, Ee Israeli, kwa sababu ya Mwumba wako,/
enyi wakazi wa Sion,*
shangilieni kwa sababu ya mfalme wenu.

Lisifuni jina lake kwa michezo,*
mwimbieni kwa ngoma na kinubi.

Mungu amependezwa na watu wake;*
yeye huwapa wanyonge ushindi.

Watu waaminifu wafurahi kwa fahari;*
washangilie hata usiku kucha.

Watangaze daima sifa kuu za Mungu,*
wakiwa na panga zenye makali kuwili mikononi mwao,

ili wawalipe kisasi watu wa mataifa,*
wawaadhibu watu wasiomjua Mungu;

wawafunge wafalme wao kwa minyororo,*
na viongozi wao kwa pingu za chuma.

kusudi watekeleze adhabu iliyoamriwa!*
Hiyo ndiyo fahari ya waaminifu wa Mungu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Wana wa Sion wamshangilie mfalme wao, aleluya.

SOMO: Ufu.7:10,12
Ukombozi wetu watoka kwa Mungu wetu aketiye juu ya kiti cha enzi, na kutoka kwa Mwana-kondoo! Amina! Sifa, utukufu, hekima, shukrani, heshima, uwezo na nguvu viwe kwa Mungu wetu, milele na milele! Amina.

KIITIKIZANO
K. Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai utuhurumie. (W. Warudie)
K. Umeketi mkono wa kuume wa Baba.
W. Utuhurumie
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Wewe...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Yesu akageuka, akamwona yule mwanamke, akamwambia, 'Jipe moyo, binti: imani yako imekuponya,' aleluya.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Yesu akageuka, akamwona yule mwanamke, akamwambia, 'Jipe moyo, binti: imani yako imekuponya,' aleluya.

MAOMBI
Tumwombe Kristo Bwana, jua linalowaangazia watu wote daima.
W. Bwana Mwokozi wetu, utupatie uzima!

Bwana wa jua na nyota, tunakushukuru kwa kutupatia siku mpya;
- nasi tunaadhimisha siku ya ufufuko wako. (W.)

Kwa njia ya Roho wako, utuongoze tutekeleze matakwa yako;
- kwa hekima yako utuelekeze na kutulinda. (W.)

Utujalie tushiriki kwa furaha adhimisho la ekaristi Jumapili ya leo;
- utulishe na kutustawisha kwa neno lako, na kwa mwili wako. (W.)

Kwa mema yote uliyotujalia,
- tunashukuru, Bwana, kwa moyo wote. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, kwa kuwa umetufanya tuwe watoto wa nuru kwa neema uliyotujalia: usiruhusu mafundisho ya uwongo yatutie giza akilini, ila ujalie nuru yako iangaze ndani mwetu, nasi tuishi daima katika mwanga wa ukweli. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.