Generic placeholder image

JUMAPILI JUMA LA 13 LA MWAKA
MASIFU YA JIONI II

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. (Aleluya)

UTENZI tazama pia AU
Sifa kwa Mtakatifu kabisa
Aliye juu na katika kina,
Asemayo mastaajabivu,
Katika yote mkweli kabisa.

Hekima pendevu ya Mungu wetu!
Ingawa dhambi na fedheha pote,
Kaja vitani Adamu wa pili,
Ili kutuoko alikuja.

Ee upendo wa busara yote!
Mwili na damu katika Adamu
Dhidi ya adui vilivyoshindwa,
Na vijitahidi hadi ushindi.

Karama bora kuliko neema,
Mwili na damu vinadhihirisha,
Uwepo hasa wa Mungu mwenyewe,
Na yake dhati, umungu mtupu.

Kwa upendo tele ukawa mtu,
Adui ya watu ukamshinda,
Mateso mawili ulikubali,
Ili binadamu anufaike.

Mosi, kwa faragha bustanini,
Wa aidha juu msalabani;
Ni funzo na himizo kwa nduguzo,
Tupende kuteswa na kufa pia.

Sifa kwa Mtakatifu kabisa,
Aliye juu na katika kina,
Asemayo mastaajabivu,
Katika yote mkweli kabisa.

AU

Mwanzoni Mungu aliumba mbingu,
Pia dunia tupu yenye giza;
Kilindini Rohoye ilivuma
Pumzi ikafanyiza mawimbi.

Kisha Mungu aliumba Mwanga,
Kuja kwa huo kulifuta giza,
Pakawa asubuhi na jioni:
Mwisho wa siku ya kwanza ya Mungu.

Atukuzwe Baba wa ulimwengu,
Na Kristo Mwana wa pekee,
Wao na Roho vyote watawala:
Utatu katika Mungu Mmoja.

ANT. I: Bwana atainyosha kutoka Sion fimbo ya nguvu zake, na atawala milele, Aleluya

Zab.110:1-5,7 Kutawazwa kwa mfalme mteule
Maana Kristo sharti atawale mpaka Mungu atakapowashinda adui zake na kuwaweka chini ya miguu yake (Kor.15:25)

Mungu amemwambia bwana wangu,*
"Keti upande wangu wa kulia,

Mpaka niwafanye maadui zako,*
kama kibao cha kuegemea miguu yako."

Toka Sion Mungu ataeneza enzi yako.*
Asema: "Tawala juu ya adui zako!"

Watu wako watajitolea,*
siku utakapopambana na adui.

Vijana wako watakujia kwenye milima mitakatifu,*
kama vile umande wa asubuhi.

Mungu ameapa, wala hataghairi:/
"Kwamba wewe ni kuhani milele,*
kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki."

Mungu yuko upande wako wa kulia;*
atakapokasirika, atawaponda wafalme.

Njiani mfalme atakunywa maji ya kijito;*
kwa hiyo atainua kichwa juu kwa ushindi.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Bwana atainyosha kutoka Sion fimbo ya nguvu zake, na atawala milele, Aleluya

ANT. II: Dunia ilitetemeka mbele ya uso wa Bwana, aleluya.

Zab.114:1-8 Mungu pamoja na watu wake
Nanyi mliouacha ulimwengu huu, tambueni kuwa mmeokolewa kutoka Misri (Mt. Augustino)

Watu wa Israeli walipoondoka nchini Misri,*
wazao wa Yakobo walipotoka ugenini,

Yuda likawa taifa takatifu la Mungu,*
Israeli ikawa mali yake mwenyewe.

Bahari ya Shamu iliona ikakimbia;*
mto Yordani ukaacha kutiririka!

Milima ilirukaruka kama kondoo dume,*
vilima vikaruka kama wana-kondoo!

Ee bahari, imekuwaje hata ukakimbia?*
Nawe Yordani, kwa nini ukaacha kutiririka?

Enyi milima, mbona mliruka kama kondoo dume?*
Nanyi vilima, imekuwaje mkaruka kama wanakondoo?

Tetemeka, ewe dunia, mbele yake Mungu;*
Naam, mbele ya Mungu wa Yakobo,

anayeugusa mwamba ukawa bwawa la maji,*
nayo majabali yakawa chemchemi za maji.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Dunia ilitetemeka mbele ya uso wa Bwana, aleluya.

ANT. III: Bwana, Mungu Mwenyezi, ni Mfalme wetu, aleluya.

WIMBO: Ufu.19:1,2,5-7 Arusi ya Mwana-kondoo
Aleluya.
Wokovu, utukufu na nguvu ni mali yake Mungu wetu!*
(W. Aleluya)
Maana hukumu yake ni ya kweli na ya haki.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Msifuni Mungu enyi watumishi wake wote,*
(W. Aleluya)
Nanyi nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Bwana, Mungu wetu Mwenyezi , ni Mfalme!*
(W. Aleluya)
Tufurahi na kushangilia; tumtukuze.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Wakati wa arusi ya Mwana-kondoo umefika,*
(W. Aleluya)
Na bibi arusi yuko tayari.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Atukuzwe Baba na Mwana, na Roho Mtakatifu,*
(W. Aleluya)
Kama mwanzo na sasa na siku zote, na milele. Amina.*
W. Aleluya (aleluya).

Ant. III: Bwana, Mungu Mwenyezi, ni Mfalme wetu, aleluya.

SOMO: 2Kor.1:3-4
Atukuzwe Mungu Baba ya Bwana wetu Yesu Kristo, Baba mwenye huruma, na Mungu mwenye kuleta faraja yote. Yeye hutufariji sisi katika taabu zetu zote, ili nasi tupate kuwafariji wengine katika kila taabu kwa faraja hiyo hiyo tunayopokea kutoka kwa Mungu.

KIITIKIZANO
K. Umehimidiwa, Ee Bwana, katika anga la mbinguni. (W. Warudie)
K. Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
W. Katika anga la mbinguni.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Umehimidiwa...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Mwana wa Mtu alikuja, si kuangamiza roho, bali kuziokoa.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Mwana wa Mtu alikuja, si kuangamiza roho, bali kuziokoa.

MAOMBI
Kristo ndiye Kichwa cha mwili wake, yaani Kanisa, na sisi ni viungo vya mwili huo; tumekusanyika jioni hii kuomba kwa jina lake, tukisema:
W. Utawala wako ufike.

Kanisa lako liwe mwanga kwa mataifa, ishara na chanzo cha nguvu yako ya kuwaunganisha watu wote
- Liwaongoze wanadamu katika fumbo la upendo wako. (W.)

Uwaongoze Papa na Maaskofu wote wa Kanisa
- uwajalie umoja, upendo na amani. (W.)

Bwana, uijalie dunia yetu amani,
- ili watu wote waishi kwa utulivu na usalama. (W.)

Utujalie moyo wa huruma kwa maskini, wagonjwa, walio pweke na wasiopendwa,
- maana katika hao tunakutana nawe. (W.)

Uwajalie marehemu ufufuo wa utukufu:
- ili tuungane nao katika furaha ya milele. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, kwa kuwa umetufanya tuwe watoto wa nuru kwa neema uliyotujalia: usiruhusu mafundisho ya uwongo yatutie giza akilini, ila ujalie nuru yako iangaze ndani mwetu, nasi tuishi daima katika mwanga wa ukweli. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.