Generic placeholder image

JUMAPILI JUMA LA 13 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
E Bwana Mbarikiwa,
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.

Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.

Ee fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;
Na yote yanafanyika
Kadiri unavyotaka.

Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu
Milele inayodumu

ANT. I: Ni heri kumkimbilia Bwana; maana fadhili zake ni za milele, aleluya.

Zab.118 Sala ya shukrani
Huyu ndiye lile jiwe mlilokataa ninyi waashi, ambalo sasa limekuwa jiwe kuu la msingi (mate.4:11)

I
Mshukuruni Mungu, kwa kuwa ni mwema,*
kwa maana upendo wake mkuu ni wa milele.

Watu wa Israeli waseme:*
"Upendo wake mkuu ni wa milele."

Wazao wa Aroni waseme:*
"Upendo wake mkuu ni wa milele."

Wote wamchao Mungu waseme:*
"Upendo wake mkuu ni wa milele."

Katika taabu yangu nilimlilia Mungu,*
naye akanisikiliza na kuniokoa.

Mungu yuko nami, siogopi kitu;*
mwanadamu atanifanya nini?

Mungu yuko nami, ananisaidia;*
nami nitashuhudia kushindwa kwa adui zangu.

Ni afadhali kumtumainia Mungu,*
kuliko kumtegemea mwanadamu.

Ni afadhali kumtumainia Mungu,*
kuliko kuwategemea viongozi wa dunia.

Watu wote wasiomjua Mungu walinizingira,*
lakini kwa nguvu ya Mungu nikawapondaponda.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Ni heri kumkimbilia Bwana; maana fadhili zake ni za milele, aleluya.

ANT. II: Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu, aleluya.

II
Walinizunguka kila upande,*
lakini kwa nguvu ya Mungu nikawapondaponda.

Walinivamia kwa wingi kama nyuki,/
lakini wakateketea kama kichaka motoni;*
kwangu nguvu ya Mungu nikawapondaponda.

Nilishambuliwa mno karibu nishindwe,*
lakini Mungu alinisaidia.

Mungu hunijalia nguvu na uhodari;*
yeye mwenyewe ameniokoa.

Sikilizeni sauti za furaha na ushindi/
katika mahema ya watu waadilifu;*
"Mkono wa Mungu umetenda mambo ya ajabu!

Mkono wa Mungu umeleta ushindi!*
Mkono wa Mungu umetenda mambo ya ajabu!"

Sitakufa, bali nitaishi,*
na kutangaza matendo ya Mungu.

Mungu ameniadhibu sana,*
lakini hakuniacha nife.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu, aleluya.

ANT. III: Nitakushukuru, Bwana, kwa kuwa umenijibu, aleluya.

III
Nifungulie milango ya Hekalu;*
nitaingia na kumshukuru Mungu!

Huu ndio mlango wa Mungu,*
ambao waadilifu waweza kupitia.

Nakushukuru, Ee Mungu, kwa kunisikiliza;*
kwa sababu wewe umeniokoa.

Jiwe walilolikataa waashi,*
limekuwa jiwe kuu la msingi.

Jambo hili limefanywa na Mungu;*
nalo ni jambo la ajabu mno kwetu.

Hii ndiyo siku aliyoifanya Mungu;*
basi, tushangilie na kufurahi.

Utuokoe, Ee Mungu, utuokoe!*
Ee Mungu, tunakusihi, utupe fanaka!

Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Mungu!*
Twakubariki toka nyumbani mwa Mungu.

Mungu ni Mungu, naye ni mwema kwetu./
Shikeni matawi mikononi, anzeni sherehe,*
mkiandamana mpaka madhabahuni.

Ndiwe, Mungu wangu, ninakushukuru*
ninakutukuza, Ee Mungu wangu.

Mshukuruni Mungu kwa kuwa ni mwema,*
kwa maana upendo wake mkuu ni wa milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Nitakushukuru, Bwana, kwa kuwa umenijibu, aleluya.

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: 1Yoh.1:16
Sisi tunajua na tunaamini upendo alio nao Mungu kwetu sisi. Mungu ni upendo, na kila mtu aishiye katika upendo, anaishi katika muungano na Mungu, na Mungu anaishi katika muungano naye.

K. Uelekeze moyo wangu kwenye utashi wako, Ee Mungu.
W. Unihuishe kwa neno lako.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Adhuhuri: Gal.6:8
Apandaye katika tamaa za kidunia, atavuna humo uharibifu; lakini akipanda katika Roho, atavuna kutoka kwa Roho uzima wa milele.

K. Ee Bwana, neno lako lasimama imara hata milele.
W. Ukweli wako wadumu kizazi hata kizazi.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Gal.6:9-10
Basi, tusichoke kutenda mema; maana tusipolegea tutavuna mavuno kwa wakati wake. Kwa hiyo, basi, tukiwa bado na wakati, tuwatendee watu wote mema, na hasa ndugu wa imani yetu.

K. Nimekuita kwa moyo wangu wote; Ee Bwana, unisikie.
W. Nami nitazishika amri zako

SALA:
Tuombe: Bwana Mungu, kwa kuwa umetufanya tuwe watoto wa nuru kwa neema uliyotujalia: usiruhusu mafundisho ya uwongo yatutie giza akilini, ila ujalie nuru yako iangaze ndani mwetu, nasi tuishi daima katika mwanga wa ukweli. Tunaomba hayo kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.