JUMAPILI YA 13 MWAKA B MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.47:1
Enyi watu wote, pigeni makofi mpigieni Mungu kelele kwa sauti ya shangwe.

KOLEKTA:
Ee Mungu, umependa kutufanya sisi tuwe wana wa nuru kwa neema uliyotufadhilia. Tunakuomba utujalie ili tusifunikwe na giza la udanganyifu, bali tukae daima peupe katika mwanga wa ukweli. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Hek.1:13-15;2:23-24
Mungu hakuifanyiza mauti, wala haimpendezi walio hai wakipotea. Kwa maana aliviumba vitu vyote ili vipate kuwako, na nguvu za uzazi zilizomo ulimwenguni ni za kuleta siha, wala hakuna ndani yake sumu yo yote ya uharibifu wala ahera haina milki kama ya kifalme hapa duniani; Maana haki yaishi milele. Yaani, Mungu alimwumba mwanadamu ili apate kutokuharibika, kwa mfano wake mwenyewe, ila ulimwengu uliingiwa na mauti kwa husuda kuionja.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.30:1,3-5,10-12
1. Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua,
Wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu.
Umeniinua nafsi yangu,
Ee Bwana, kutoka kuzimu.
Umenihuisha na kunitoa
Miongoni mwao washukao shimoni.

(K) Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua.

2. Mwimbieni Bwana zaburi,
Enyi watauwa wake.
Na kufanya shukrani.
Kwa kumbukumbu la utakatifu wake.
Maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo,
Katika radhi yake mna uhai.
Huenda kuliko huja kukaa usiku,
Lakini asubuhi huwa furaha. (K)

3. Ee Bwana, usikie, unirehemu,
Bwana, uwe msaidizi wangu.
Uligeuza matanga yangu kuwa machezo;
Ee Bwana, Mungu wangu,
Nitakushukuru milele. (K)

SOMO 2: 2Kor.8:7,9,13-15
Kama mlivyo na wingi wa mambo yote; imani, na usemi, na elimu, na bidii yote, na upendo wenu kwetu sisi; basi vivyo hivyo mpate wingi wa neema hii pia. Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake. Maana sisemi bali mambo yawe sawasawa; wakati huu wa sasa wingi wenu uwafae upungufu wao, ili na wingi wao uwafae ninyi mtakapopungukiwa; ili mambo yawe sawasawa. Kama ilivyoandikwa, aliyekusanya vingi, hakuzidi, wala yeye aliyekusanya vichache hakupungukiwa.

SHANGILIO: Yn.1:12,14
Aleluya, aleluya!
Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu. Wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu.
Aleluya!

INJILI: Mk.5:21-4:
Yesu alipokwisha kuvuka kurudi ng’ambo katika kile chombo, wakamkusanyikia mkutano mkuu; naye alikuwa kando ya bahari. Akaja mtu mmoja katika wakuu wa sinagogi, jina lake Yairo; hata alipomwona, akaanguka miguuni pake, akimsihi sana, akisema, Binti yangu mdogo yu katika kufa; nakuomba uje, uweke mkono wako juu yake, apate kupona, na kuishi. Akaenda pamoja naye. Mkutano mkuu wakamfuata, wakimsonga-songa. Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya; aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake, maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona. Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule. Mara Yesu, hali akifahamu nafsini mwake kwamba nguvu zimemtoka, akageuka kati ya mkutano, akasema, Ni nani aliyenigusa mavazi yangu? Wanafunzi wake wakamwambia, Je! wawaona makutano wanavyokusonga-songa, nawe wasema, Ni nani aliyegusa? Akatazama pande zote ili amwone yule aliyelitenda neno hilo. Na yule mwanamke akaingiwa na hofu na kutetemeka, akijua lililompata, akaja akamwangukia, akamweleza kweli yote. Akamwambia, Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena. Halipokuwa katika kunena, wakaja watu kutoka kwa yule mkuu wa sinagogi, wakisema, Binti yako amekwisha kufa; kwani kuzidi kusumbua mwalimu? Lakini Yesu, alipolisikia lile neno likinenwa, akamwambia mkuu wa sinagogi, Usiogope, amini tu. Wala hakumruhusu mtu afuatane naye, ila Petro, na Yakobo, na Yohane nduguye Yakobo. Wakafika nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi, akaona ghasia, na watu wakilia, wakifanya maombolezo makuu. Alipokwisha kuingia, akawaambia, Mbona mnafanya ghasia na kulia? Kijana hakufa, bali amelala tu. Wakamcheka sana. Naye alipokwisha kuwatoa nje wote, akamtwaa babaye yule kijana na mamaye, na wale walio pamoja naye, akaingia ndani alimokuwamo yule kijana. Akamshika mkono kijana, akamwambia, Tallitha, kumi; tafsiri yake, Msichana, nakuambia, inuka. Mara akasimama yule kijana, akaenda; maana alikuwa amepata umri wa miaka kumi na miwili. Mara wakashangaa mshangao mkuu. Akawaonya sana, mtu asijue habari ile; akaamuru apewe chakula.

Nasadiki husemwa.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Mungu, wewe unapenda kutuletea mapato mazuri ya mafumbo yako. Tunakuomba utujalie ibada za utumishi wetu ziendane na dhabihu hii takatifu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.103:1
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Naam, vyote vilivyo ndani yangu vilihimidi jina lake takatifu.

Au:
Yn 17:20-21

Baba, ninawaombea hao, nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, tunaomba sadaka hii ya kimungu tuliyokutolea na kuila itutie uzima, ili, kwa kuungana nawe siku zote kwa mapendo, tupate kuzaa matunda yenye kudumu daima. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.