Generic placeholder image

JUMAPILI JUMA LA 14 LA MWAKA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Sisi ni watu wake Bwana, kundi linaloongozwa kwa mkono wake: njooni, tumwabudu, aleluya.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI angalia pia AU
Leo ninalipokea
Jina tukufu la Utatu,
Kwa kulitaja hilo jina,
Nafsi tatu Mungu Mmoja,
Mungu Mmoja Nafsi tatu.

Leo najinyenyekeza,
Uweza wa Mungu uniongoze,
Jicho lake liniangalie,
Nguvu zake zidumu nami,
Sikio lake linisikilize.

Hekima ya Mungu wangu inifunze,
Mkono wake unioneshe njia
Yake ngao mimi na inikinge;
Linisemeshe neno la Mungu,
Majeshi yake ya mbinguni yanilinde.

Leo ninalipokea
Jina tukufu la Utatu,
Kwa kulitaja hilo jina,
Nafsi tatu Mungu Mmoja,
Mungu Mmoja Nafsi tatu.
U Muumba wa vitu vyote
Ndiwe Mungu milele milele,
Baba, Roho, Mwana:
Usifiwe Bwana wa wokovu wangu,
Wokovu ulo katika Kristo Bwana.

AU:

Watu wote mwishio duniani,
Kwa shangwe kuu Bwana mwimbieni;
Na kwa furaha mtumikieni,
Sifa yake Bwana itangazeni,
Njooni mbele yake, furahini.

Bwana ni Mungu kweli, mnajua;
Bila ya sisi kumsaidia
Bwana Mungu sote ametuumba;
Sisi ni watu wake, atulisha;
Katufanya kuwa kondoo wake.

Kwani, Bwana Mungu wetu ni mwema:
Milele huruma yake yakini;
Kweli zake zimekuwa thabiti,
Na thabiti daima zitabaki,
Kweli zake zitadumu imara.

Sifa nao utukufu milele

Kutoka kwa watu na malaika Zimwendee Baba na pia Mwana
Na Roho Mtakatifu pamoja,
Mungu anayeabudiwa pote.

ANT.I: Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana, aleluya.

Zab.118 Sala ya shukrani
Huyu ndiye lile Jiwe mlilolikataa ninyi waashi, ambalo sasa limekuwa jiwe kuu la msingi (Mate.4:11)

Mshukuruni Mungu, kwa kuwa ni mwema,*
kwa maana upendo wake mkuu ni wa milele.

Watu wa Israeli waseme:*
"Upendo wake mkuu ni wa milele.“

Wazao wa Aroni waseme:*
“Upendo wake mkuu ni wa milele."

Wote wamchao Mungu waseme:*
"Upendo wake mkuu ni wa milele."

Katika taabu yangu nilimlilia Mungu,*
naye akanisikiliza na kuniokoa.

Mungu yuko nami, siogopi kitu;*
mwanadamu atanifanya nini?

Mungu yuko nami, ananisaidia;*
nami nitashuhudia kushindwa kwa adui zangu.

Ni afadhali kumtumainia Mungu,*
kuliko kumtegemea mwanadamu.

Ni afadhali kumtumainia Mungu,*
kuliko kuwategemea viongozi wa dunia.

Watu wote wasiomjua Mungu walinizingira,*
lakini kwa nguvu ya Mungu nikawapondaponda.

Walinizunguka kila upande,*
lakini kwa nguvu ya Mungu nikawapondaponda.

Walinivamia kwa wingi kama nyuki,/
lakini wakateketea kama kichaka motoni;*
kwa nguvu ya Mungu nikawapondaponda.

Nilishambuliwa mno karibu nishindwe*
lakini Mungu alinisaidia.

Mungu hunijalia nguvu na uhodari;*
yeye mwenyewe ameniokoa.

Sikilizeni sauti za furaha na ushindi/
katika mahema ya watu waadilifu;*
"Mkono wa Mungu umetenda mambo ya ajabu!

Mkono wa Mungu umeleta ushindi!*
Mkono wa Mungu umetenda mambo ya ajabu!"

Sitakufa, bali nitaishi,*
na kutangaza matendo ya Mungu.

Mungu ameniadhibu sana,*
lakini hakuniacha nife.

Nifungulie milango ya Hekalu;*
nitaingia na kumshukuru Mungu!

Huu ndio mlango wa Mungu,*
ambao waadilifu waweza kuupitia.

Nakushukuru, Ee Mungu, kwa kunisikiliza;*
kwa sababu wewe umeniokoa.

Jiwe walilolikataa waashi,*
limekuwa jiwe kuu la msingi.

Jambo hili limefanywa na Mungu;*
nalo ni jambo la ajabu mno kwetu.

Hi ndiyo siku aliyoifanya Mungu;*
basi, tushangilie na kufurahi.

Utuokoe, Ee Mungu, utuokoe!*
Ee Mungu, tunakusihi, utupe fanaka!

Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Mungu!*
Twakubariki kutoka nyumbani mwa Mungu.

Mungu ni Mungu, naye ni mwema kwetu./
Shikeni matawi mikononi, anzeni sherehe,*
mkiandamana mpaka madhabahuni.

Ndiwe Mungu wangu, ninakushukuru*
ninakutukuza, Ee Mungu wangu.

Mshukuruni Mungu kwa kuwa ni mwema,*
kwa maana upendo wake mkuu ni wa milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana, aleluya.

ANT. II: Tumwimbie Mungu wetu, aleluya.

WIMBO: Dan.3:52-56 Kila kiumbe kimsifu Bwana
Mwumba astahili sifa milele (Rom.1:25)

Umehimidiwa, Ee Bwana, MUNGU wa baba zetu;*
Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.

Limehimidiwa jina lako takatifu, tukufu;*
Lastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.

Umehimidiwa katika hekalu la fahari yako takatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Umehimidiwa juu ya kiti cha ufalme wako,*
Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.

Umehimidiwa utazamaye vilindi, uketiye juu ya makerubi;*
Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.

Umehimidiwa katika anga la mbinguni*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Tumtukuze Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Umehimidiwa katika anga la mbinguni,*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Ant. II: Tumwimbie Mungu wetu, aleluya.

ANT. III: Msifuni Mungu kwa kadiri ya wingi wa ukuu wake, aleluya.

Zab.150 Zaburi ya kumsifu Mungu
Msifuni Mungu rohoni mwenu, msifuni kwa mioyo yenu, yaani: mtukuzeni Mungu kwa roho na kwa mwili (Hesychius)

Msifuni Mungu Hekaluni mwake;*
msifuni kwa ajili ya enzi yake mbinguni.

Msifuni kwa ajili ya matendo yake makuu;*
msifuni kwa ajili ya utukufu wake mkuu.

Msifuni kwa mlio wa tarumbeta;*
msifuni kwa zeze na kinubi!

Msifuni kwa ngoma na michezo;*
msifuni kwa filimbi na bango!

Msifuni kwa kupiga matoazi;/
msifuni kwa kuvumisha matoazi.*
Kila kiumbe chenye uhai na kimsifu Mungu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Msifuni Mungu kwa kadiri ya wingi wa ukuu wake, aleluya.

SOMO: Eze.36:25-27
Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda.

KIITIKIZANO
K. Tunakushukuru, Ee Mungu, na tunaomba msaada kwa jina lako. (W. Warudie)
K. Tunasimulia matendo yako ya ajabu.
W. Na tunaomba msaada kwa jina lako.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Tunakushukuru...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Wengi waliposikia mafundisho ya Yesu, walishangaa wakasema, 'Je, huyu ameyapata wapi hayo? Je, huyu si yule seremala, mwana wa Maria?'

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Wengi waliposikia mafundisho ya Yesu, walishangaa wakasema, 'Je, huyu ameyapata wapi hayo? Je, huyu si yule seremala, mwana wa Maria?'

MAOMBI
Tumshukuru Mwokozi wetu aliyekuja duniani ili Mungu apate kuwa nasi.
W. Bwana, tunakusifu na tunakushukuru.

Tunakukaribisha kwa sifa, wewe uliye nyota ya Mchana, na Tunda la kwanza kutoka katika wafu:
- nasi tufufuke nawe, ili tutembee katika mwanga wa Pasaka. (W.)

Utusaidie siku hii ya mapumziko, tuweze kuona uzuri katika viumbe vyako vyote:
- fungua macho na mioyo yetu, tupate kutambua na kukiri mapendo yako duniani. (W.)

Ee Bwana, sisi familia yako, tunakusanyika mezani pako:
- utusaidie tuweze kuondoa na kusahau magomvi na chuki kati yetu, na utusamehe dhambi zetu. (W.)

Tunaziombea familia zote za Kikristo:
- Roho aziongezee umoja katika imani na mapendo. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, ulimwengu wetu ulipokuwa umeanguka na kuwa magofu, wewe uliujenga upya juu ya msingi wa mateso na kifo cha Mwanao; utupatie neema ya kufurahia kuondokana kwetu na dhambi, uhuru ambao Mwanao alijipatia kwa ajili yetu, na utufikishe kwenye furaha ya milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.