Generic placeholder image

JUMAPILI JUMA LA 14 LA MWAKA
MASIFU YA JIONI I

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya

UTENZI
Atukuzwe Bwana Mungu wetu!
Mbingu na ziimbe kwa furaha;
Dunia iimbe mbele yake
Nyimbo zake za heshima kuu!
Yatangazwe matendo makuu;
Usifiwe wake utukufu;
Sauti zote na zipalizwe
Kwa Mungu Mfalme mtukufu!

Vyote viishivyo na kupumua
Vishukuru kwa nyimbo za dhati;
Vitu vyote vimwimbie Yeye
Astahiliye sifa zote!
Tangazeni upendo wa Baba,
Katupatia Mungu Mwanae;
Msifuni Roho tulompata
Aliye mmojawao milele.

ANT. I: Ee Bwana, neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu, aleluya.

Zab.119:105-112 XIV Sheria ya Mungu ni mwanga
Hii ndiyo amri yangu: pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda ninyi (Yoh.15:12)

Neno lako ni taa ya kuniongoza,*
na mwanga katika njia yangu.

Nimeapa na kuthibitisha kiapo changu,*
kwamba nitashika maagizo yako maadilifu.

Ee Mungu, ninateseka mno;*
unipe uhai kama ulivyoahidi.

Ee Mungu, upokee sala yangu ya shukrani;*
na unifundishe maagizo yako.

Maisha yangu yamo hatarini daima,*
lakini siisahau sheria yako.

Waovu wamenitegea mtego kuninasa,*
lakini sikiuki amri zako.

Maagizo yako ni rasilimali yangu daima;*
naam, ni furaha ya moyo wangu.

Nimekusudia kwa moyo wote*
kutimiza kanuni zako milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Ee Bwana, neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu, aleluya.

ANT. II: Ee Bwana, utanionesha furaha kamili mbele yako, aleluya.

Zab.16 Kuomba usalama
Mungu alimfufua Yesu, akamwokoa kutoka katika maumivu ya kifo (Mate.2:24)

Unilinde, Ee Mungu;*
nakimbilia usalama kwako.

Nimemwambia Mungu: “Wewe ni Bwana wangu;*
mema yote niliyo nayo yatoka kwako."

Ni bora sana hao watakatifu walioko nchini;*
kukaa nao ndiyo furaha yangu.

Lakini wanaokimbilia miungu mingine,*
wanajizidishia taabu wao wenyewe.

Damu ya matambiko sitawatolea kamwe;*
na majina ya miungu hiyo sitayataja kamwe.

Ee Mungu, wewe peke yako, ndiwe tegemeo langu;/
wewe wanipa mahitaji yangu yote;*
maisha yangu yamo mikononi mwako.

Umenipimia sehemu nzuri sana;*
naam, kila ulichonipa ni kizuri sana.

Nitamtukuza Mungu kwa kuniongoza,*
na usiku dhamiri yangu yanionya.

Namweka Mungu mbele yangu daima,*
yuko karibu nami, wala sitatikisika.

Kwa hiyo nafurahi na kushangilia,*
nami nitakaa salama salimini,

kwani wanikinga na nguvu za kuzimu,*
wala humwachi mpendwa wako apotee huko ahera.

Utanionesha njia ya kufikia uzima;/
kuwako kwako kwanijaza furaha,*
uwezo wako waniletea raha daima.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Ee Bwana, utanionesha furaha kamili mbele yako, aleluya.

ANT. III: Kila kiumbe, mbinguni na duniani, kilipigie goti jina la Yesu, aleluya.

WIMBO: Filp.2:6-11 Kristo, mtumishi wa Mungu
Yesu, kwa asili,*
alikuwa daima Mungu;

lakini hakufikiri kwamba/
kule kuwa sawa na Mungu*
ni kitu cha kung'ang'ania kwa nguvu.

Bali, kwa hiari yake mwenyewe,*
aliachilia hayo yote,

akajitwalia hali ya mtumishi/
akawa sawa na wanadamu,*
akaonekana kama wanadamu.

Alijinyenyekeza na kutii mpaka kufa,*
hata kufa msalabani.

Kwa sababu hiyo*
Mungu alimkweza juu kabisa,

akampa jina lililo kuu zaidi*
kuliko majina yote.

Ili kwa heshima ya jina la Yesu,/
viumbe vyote mbinguni, duniani na kuzimu,*
vipige magoti mbele yake;

Na kila mtu akiri/
Kwamba Yesu Kristo ni Bwana,*
kwa utukufu wa Mungu Baba.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Kila kiumbe, mbinguni na duniani, kilipigie goti jina la Yesu, aleluya.

SOMO: Kol.1:3-6a
Daima tunamshukuru Mungu, Baba ya Bwana wetu Yesu Kristo, wakati tunapowaombea. Maana tumesikia juu ya imani yenu katika Kristo Yesu, na juu ya mapendo yenu kwa watu wote wa Mungu. Wakati ujumbe ule wa kweli, yaani ile Habari Njema, ulipowafikieni kwa mara ya kwanza mlipata kusikia juu ya lile tumaini linalopatikana kwake. Kwa sababu hiyo imani na mapendo yenu yanategemea jambo lile mnalotumainia, ambalo mmewekewa salama mbinguni. Injili inazidi kuzaa matunda nakuenea ulimwenguni kote, kama vile ilivyofanya kwenu ninyi.

KIITIKIZANO
K. Tangu mawio ya jua hata machweo yake, jina la Bwana litukuzwe. (W. Warudie)
K. Utukufu wake u juu ya mbingu.
W. Jina la Bwana litukuzwe.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Tangu...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Nira yangu ni rahisi kuchukua, na mzigo wangu ni mwepesi, asema Bwana.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana.
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Nira yangu ni rahisi kuchukua, na mzigo wangu ni mwepesi, asema Bwana.

MAOMBI
Mungu, Baba yetu, kwa mapendo makubwa hutuongoza mbele kuelekea kwenye siku ya furaha, tutakapoingia katika pumziko lake.
W. Matumaini yetu yote ni kwako, Ee Bwana Mungu.

Tunawaombea Papa wetu F..., na Askofu wetu F...:
- uwaongoze na uwabariki katika kazi zao. (W.)

Uwasaidie wagonjwa wayavumilie mateso yao pamoja na Kristo,
- ili wapate katika Kristo ukamilifu wa maisha na mapendo. (W.)

Kristo hakuwa na mahali pa kulaza kichwa chake:
- utuwezeshe sisi kutambua shida na haja za wale wasio na maskani. (W.)

Uwabariki wakulima wote:
- utujalie tuyapokee kwa shukrani mazao ya nchi. (W.)

Baba, uwahurumie wale waliofariki dunia wakiwa katika amani ya Kristo:
- uwaingize katika makao uliyokwisha watayarishia. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, ulimwengu wetu ulipokuwa umeanguka na kuwa magofu, wewe uliujenga upya juu ya msingi wa mateso na kifo cha Mwanao; utupatie neema ya kufurahia kuondokana kwetu na dhambi, uhuru ambao Mwanao alijipatia kwa ajili yetu, na utufikishe kwenye furaha ya milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.