Generic placeholder image

JUMAPILI JUMA LA 14 LA MWAKA
MASIFU YA JIONI II

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya

UTENZI tazama pia AU
Ee Mungu twasifu lako jina;
Bwana wa wote twakusujudia!
Vyote duniani enzi vyakiri
Na vyote mbinguni vyakuabudu.
Milki yako haina mipaka,
Ni wa milele wako utawala.

Sikilizeni! Utenzi wa mbingu!
Malaika waimba kwa sauti;
Makerubi na pia Maserafi
Kwa sauti tamu hujaza mbingu
Waimba na kusifu bila mwisho:
Mtakatifu 'takatifu Bwana.

Mtakatifu Baba, pia Mwana,
Mtakatifu Roho, E Utatu.
U Mmoja tu katika udhati
Mungu usiyegawanyika katu;
Twakuabudu tukipiga goti,
Wakati hilo fumbo twaungama.

E Bwana waokoe watu wako
Waliozungukwa na majaribu;
Tusaidie twepe dhambi leo
Situache kamwe tuvurugike.
Loo, tumaini langu ni kwako,
Bwana usiniache peke yangu.

AU

Msifu Mfalme wa mbinguni,
ee roho yangu;
Miguuni pake peleka ushuru wako;
Amenikomboa na kuniponya,
Kanitia nguvu, kanisamehe;
Nani basi kama mimi apaswa kuimba?
Msifu Yeye! Msifu Yeye!
Msifu Yeye! Msifu Yeye!
Msifu Mfalme wa milele.

Msifu kwa hisani aloonyesha
Kwa baba zetu mahangaikoni;.
Msifu Yeye asobadilika milele,
Si mwepesi wa kukaripia
Ni mwepesi wa kubariki;
Msifu Yeye! Msifu Yeye!
Msifu Yeye! Msifu Yeye!
Katika uaminifu wake ni Mkuu.

Atutunza na kuturehemu kama baba;
Udhaifu wetu aujua vema,
Kwa upole anatuchukua
Na kutujaza matumaini,
Hutuokoa na adui zetu wote;
Msifu Yeye! Msifu Yeye!
Msifu Yeye! Msifu Yeye!
Kama huruma yake ilivyoenea.

Enyi malaika tusaidieni,
Na tusaidieni kumuabudu Yeye;
Ninyi mwamwona Yeye uso kwa uso;
Jua na mwezi mbele zake inameni,
Vyote vilivyoko wakati wote angani.
Msifuni Yeye! Msifuni Yeye!
Msifuni Yeye! Msifuni Yeye!
Pamoja nasi msifuni Mungu Mhisani.

ANT. I: Kristo, Bwana, ndiye kuhani milele, kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki, aleluya.

Zab.110:1-5,7 Kutawazwa kwa mfalme mteule
Kristo sharti atawale mpaka Mungu atakapowashinda adui zake na kuwaweka chini ya miguu yake (Kor.15:25)

Mungu amemwambia bwana wangu,*
"Keti upande wangu wa kulia,

Mpaka niwafanye maadui zako,*
kama kibao cha kuegemea miguu yako."

Toka Sion Mungu ataeneza enzi yako.*
Asema: "Tawala juu ya adui zako!"

Watu wako watajitolea,*
siku utakapopambana na adui.

Vijana wako watakujia kwenye milima mitakatifu,*
kama vile umande wa asubuhi.

Mungu ameapa, wala hataghairi:/
"Kwamba wewe ni kuhani milele,*
kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki."

Mungu yuko upande wako wa kulia;*
atakapokasirika, atawaponda wafalme.

Njiani mfalme atakunywa maji ya kijito;*
kwa hiyo atainua kichwa juu kwa ushindi.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Kristo, Bwana, ndiye kuhani milele, kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki, aleluya.

ANT. II: Mungu wetu yuko mbinguni: hufanya cho chote apendacho, aleluya.

Zab.115 Mungu mmoja wa kweli
Mmemgeukia Mungu, mkaziacha sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai na wa kweli (1Tes.1:9)

Sio sisi, Ee Mungu, sio sisi;/
bali wewe peke yako utukuzwe,*
kwa ajili ya upendo wako mkuu na uaminifu wako.

Kwa nini mataifa yanatuuliza:*
"Mungu wenu yuko wapi?"

Mungu wetu yuko mbinguni;*
yote anayotaka huyafanya.

Miungu yao imefanywa kwa fedha na dhahabu;*
imetengenezwa kwa mikono ya wanadamu.

Ina vinywa lakini haisemi;*
ina macho lakini haioni.

Ina masikio lakini haisikii;*
ina pua lakini hainusi.

Ina mikono lakini haipapasi;/
ina miguu lakini haitembei.*
Haiwezi kamwe kutoa sauti.

Wote wanaoitengeneza wanafanana nayo,*
kadhalika na wote walio na imani nayo.

Enyi watu wa Israeli mtumainieni Mungu;*
yeye ni msaidizi wenu na ngao yenu.

Enyi wazao wa Aroni mtumainieni Mungu;*
yeye ni msaidizi wenu na mlinzi wenu.

Enyi mnaomcha Mungu mtumainieni Mungu;*
yeye ni msaidizi wenu na mlinzi wenu.

Mungu anatukumbuka, na atatubariki;/
atawabariki watu wa Israeli,*
atawabariki wazao wa Aron.

Atawabariki wote wamchao,*
atawabariki wazao wa Aron.

Mungu awajalieni watoto;*
awajalie ninyi na wazao wenu!

Mbarikiwe na Mungu,*
aliyeumba mbingu na dunia.

Mbingu ni mali yake Mungu,*
bali dunia amewapa wanadamu.

Sio wafu wanaomsifu Mungu,*
wala ye yote aliyeshuka kuzimuni.

Basi ni sisi tutakaomsifu Mungu,*
sasa na hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Mungu wetu yuko mbinguni: hufanya cho chote apendacho, aleluya.

ANT. III: Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote, wakubwa kwa wadogo, aleluya.

WIMBO: Ufu.19:1,2,5-7 Arusi ya Mwana-kondoo

Aleluya.
Wokovu, utukufu na nguvu ni mali yake Mungu wetu!*
(W. Aleluya)
Maana hukumu yake ni ya kweli na ya haki.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Msifuni Mungu enyi watumishi wake wote,*
(W. Aleluya)
Nanyi nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Bwana, Mungu wetu Mwenyezi , ni Mfalme!*
(W. Aleluya)
Tufurahi na kushangilia; tumtukuze.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Wakati wa arusi ya Mwana-kondoo umefika,*
(W. Aleluya)
Na bibi arusi yuko tayari.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Atukuzwe Baba na Mwana, na Roho Mtakatifu,*
(W. Aleluya)
Kama mwanzo na sasa na siku zote, na milele. Amina.*
W. Aleluya (aleluya).

Ant. III: Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote, wakubwa kwa wadogo, aleluya.

SOMO: 2Tes.2:13-14
Tunapaswa kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu ninyi ndugu, ninyi mnaopendwa na Bwana. Kwa maana Mungu amewateua tangu mwanzo mpate kuokolewa kwa nguvu ya Roho, mfanywe watu wake watakatifu kwa imani yenu katika ukweli. Mungu aliwaitieni jambo hili kwa njia ya Habari Njema tuliyowahubirieni; aliwaiteni mpate kupokea sehemu yenu katika utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo.

KIITIKIZANO
K. Bwana Mungu wetu ni Mwenyezi, uwezo wake ni mkuu. (W. Warudie)
K. Hekima yake haina mipaka.
W. Uwezo wake ni mkuu.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Mavuno ni mengi, lakini wafanyakazi ni wachache. Mwombeni Bwana ambaye mavuno ni yake, awatume wafanyakazi wakakusanye mavuno yake.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Mavuno ni mengi, lakini wafanyakazi ni wachache. Mwombeni Bwana ambaye mavuno ni yake, awatume wafanyakazi wakakusanye mavuno yake.

MAOMBI
Yesu Kristo anatuita kushiriki utukufu wake. Pamoja naye tumwombe Baba yetu wa mbinguni.
W. Baba, kwa huruma yako yasikie maombi yetu.

Tunayaombea mataifa yote:
- ili yatafute njia zenye kufikia amani; ili yaheshimu haki na uhuru wa binadamu kila mahali; ili kwa upendo yapate kugawanya rasilmali ya dunia. (W.)

Tunaliombea Kanisa:
- ili viongozi wake walihubiri kiaminifu neno lako, ili waamini wote wawe imara katika imani na matumaini, na kwa njia ya upendo wa Kanisa kwa wote, Wewe utambulike. (W.)

Uwe nasi katika familia zetu na katika jumuiya hii:
- ili katika wenzetu wote tukuone Wewe. (W.)

Tunajiombea wenyewe:
- ili kwa kazi zetu tuweze kuwatumikia wenzetu. (W.)

Tunawaombea waamini marehemu:
- ili kwa huruma yako wapumzike kwa amani. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, ulimwengu wetu ulipokuwa umeanguka na kuwa magofu, wewe uliujenga upya juu ya msingi wa mateso na kifo cha Mwanao; utupatie neema ya kufurahia kuondokana kwetu na dhambi, uhuru ambao Mwanao alijipatia kwa ajili yetu, na utufikishe kwenye furaha ya milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.