Generic placeholder image

JUMAPILI JUMA LA 14 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Njoo Roho Mtakatifu,
Ndani yetu sisi uishi,
Pamoja nawe waje pia
Mungu Baba na Mungu Mwana,
Nazo zako tele neema
Njoo upate tujalia,
Zitufanye watakatifu,
Pia tuwe kitu kimoja.

Imara katika upendo
Na viwe, roho na ulimi,
Yako sifa kuitangaza
Kila mahali duniani,
Na ule upendo jalie-
Ulio mwetu mioyoni-
Mioyo mingine iwashwe
Kutokana na mwako wake.

Ee Mtukufu kabisa
Utatu ulio upendo,
Moyo wake bin-Adamu
Kwa ajili yako 'liumbwa,
Kwako Wewe na iwe sifa
Kwa wimbo usio na mwisho,
Haki yako Wewe pekee
Kwabudiwa hata milele.

ANT. I: Bwana hunilaza katika malisho ya majani mabichi, aleluya.

Zab.23 Mungu mchungaji wetu
Mwana-kondoo atakuwa mchungaji wao, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji ya uzima (Ufu.7:17)

Mungu ni mchungaji wangu;*
sitapungukiwa chochote,

Hunipumzisha kwenye malisho mabichi;/
huniongoza kwenye maji matulivu na safi,*
na kunirudishia nguvu.

Huniongoza katika njia iliyo sawa,*
kwa ajili ya jina lake.

Nijapopita katika giza kuu, sitaogopa,/
kwa kuwa wewe Mungu u pamoja nami;*
fimbo yako na bakora yako vyanilinda.

Waniandalia karamu mbele ya adui zangu;/
umenipaka mafuta kichwani mwangu,*
na kikombe changu wakijaza mpaka kufurika.

Hakika wema wako na upendo wako mkuu,/
vitakuwa pamoja nami maisha yangu yote.*
Nitakaa nyumbani mwako muda wote niishipo.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Bwana hunilaza katika malisho ya majani mabichi, aleluya.

ANT. II: Katika Israeli jina la Mungu ni kuu, aleluya.

Zab.76 Mungu Mshindi
Watamwona Mwana wa Mtu akija juu ya mawingu ya angani (Mt.24:30)

I
Mungu anajulikana katika Yuda;*
jina lake ni kuu katika Israeli.

Hema lake liko huko Salemu;*
makao yake yako huko Sion.

Huko alivunja mishale ya adui;*
alivunja ngao, panga na silaha.

Wewe, Ee Mungu, watukuka mno;/
umejaa fahari kuu unaporudi,*
kutoka milimani ulikowashinda adui.

Washupavu wao wamenyang'anywa nyara zao,/
sasa wanalala usingizi wao wa mwisho,*
ushujaa wao wote haukuwafaa kitu.

Ulipowakemea, Ee Mungu wa Yakobo,*
farasi na wapanda farasi walikufa ganzi.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Katika Israeli jina la Mungu ni kuu, aleluya.

ANT. III: Dunia iliogopa, ikakaa kimya, Mungu aliposimama kuihukumu.

II
Wewe, Ee Mungu, ni wa kutisha mno!*
Nani awezaye kustahimili ukikasirika?

Umejulisha hukumu yako toka mbinguni,*
nayo dunia ikaogopa na kunyamaa;

wakati ulipoinuka, Ee Mungu, kutoa hukumu,*
kuwaokoa wote wanaodhulumiwa duniani.

Ghadhabu ya watu husababisha tu sifa kwako;*
na walioponea huko Emati watafanya sikukuu zako.

Mpeni Mungu, Mungu wenu, yale mliyoahidi;*
enyi mlio karibu, mpeni vipaji Mungu wa kutisha.

Yeye huwanyenyekesha wakuu;*
huwatisha wafalme wa dunia.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Dunia iliogopa, ikakaa kimya, Mungu aliposimama kuihukumu.

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: Rom.5:1-2,5
Sasa, kwa vile tumefanywa kuwa wenye uhusiano mwema na Mungu kwa imani, basi, tunayo amani naye kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa imani yetu yeye ametuweka katika hali hii ya neema ya Mungu ambayo sasa tunaiishi. Basi, tunajivunia tumaini tulilonalo la kuushiriki utukufu wa Mungu. Tumaini hilo haliwezi kutuhadaa, maana Mungu amekwisha miminia mioyoni mwetu mapendo yake kwa njia ya Roho Mtakatifu aliyetujalia.

K. Nitayaimba daima mapendo yako, Ee Bwana.
W. Kinywa changu kitautangaza ukweli wako, kizazi hata kizazi.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Adhuhuri: Rom.8:26
Roho anatusaidia katika udhaifu wetu. Maana hatujui inavyotupasa kuomba; lakini Roho mwenyewe anatuombea kwa Mungu kwa mlio wa huzuni usioelezeka.

K. Ee Bwana, kilio changu kikufikie.
W. Unifundishe kwa neno lako.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: 2Kor.1:21-22
Mungu mwenyewe ndiye mwenye kutuimarisha sisi na ninyi pia katika Kristo, na ndiye anayetuweka wakfu; ndiye aliyetutia muhuri wa kuwa mali yake yeye, na kutujalia Roho mioyoni mwetu kama dhamana ya mambo yote ambayo ametuwekea.

K. Bwana ni nuru yangu na msaada wangu.
W. Naye ni mlinzi wa uhai wangu.

SALA:
Tuombe: Bwana Mungu, ulimwengu wetu ulipokuwa umeanguka na kuwa magofu, wewe uliujenga upya juu ya msingi wa mateso na kifo cha Mwanao; utupatie neema ya kufurahia kuondokana kwetu na dhambi, uhuru ambao Mwanao alijipatia kwa ajili yetu, na utufikishe kwenye furaha ya milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.