JUMAPILI YA 14 MWAKA B
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.48:9-10
Tumezitafakari fadhili zako, ee Mungu, katikati ya hekalu lako. Kama lilivyo jina lako, ee Mungu, ndivyo na sifa yako hata miisho ya dunia. Mkono wako wa kuume umejaa haki.

KOLEKTA:
Ee Mungu, kwa njia ya unyenyekevu wa Mwanao umeuinua ulimwengu uliokuwa umeanguka. Uwajalie waamini wako furaha takatifu ili, hao uliowaondoa katika utumwa wa dhambi, wapate kuifikia furaha ya milele. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Eze.2:2-5
Bwana aliposema nami, roho ikaniingia, ikanisimamisha; nikamsikia yeye aliyesema nami. Akaniambia, Mwanadamu, nakutuma kwa wana wa Israeli, kwa mataifa wanaoasi, walioniasi mimi, wao na baba zao wamekosa juu yangu, naam, hata hivi leo. Na hao wana nyuso zisizo na haya, na mioyo yao ni migumu. Mimi nakutuma kwa hao; nawe utawaambia, Bwana Mungu asema hivi. Nao, kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia, (maana ndio nyumba ya kuasi hao), hata hivyo watajua ya kuwa nabii amekuwako miongoni mwao.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.123(K)2
1. Nimekuinulia macho yangu,
Wewe uketiye mbinguni.
Kama vile macho ya watumishi
Kwa mkono wa bwana zao.

(K) Macho yetu humwelekea Bwana, Mungu wetu.

2. Kama macho ya mjakazi
Kwa mkono wa bibi yake;
Hivyo macho yetu humwelekea Bwana, Mungu wetu.
Hata atakapoturehemu. (K)

3. Uturehemu, Ee Bwana, uturehemu sisi,
Kwa maana tumeshiba dharau.
Nafsi zetu zimeshiba mzaha wa wenye raha,
Na dharau ya wenye kiburi. (K)

SOMO 2:2Kor.12:7-10
Makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili; mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.

SHANGILIO: Yn.14:23
Aleluya, aleluya!
Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake.
Aleluya!

INJILI: Mk.6:1-6
Yesu alitoka, akafika mpaka nchi ya kwao, wanafunzi wake wakamfuata. Na ilipokuwa sabato, alianza kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia wakashangaa, wakisema, Huyu ameyapata wapi haya? na, Ni hekima gani hii aliyopewa huyu? Na, Ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake? Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake. Yesu akawaambia, Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake. Wala hakuweza kufanya mwujiza wo wote huko; isipokuwa aliweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache akawaponya. Akastaajabu kwa sababu ya kutokuamini kwao.

Nasadiki husemwa.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunaomba sadaka tunayotoa kwa heshima ya jina lako itutakase, na ituwezeshe kutenda siku kwa siku kadiri ya uzima wa mbinguni. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.34:8
Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema; heri mtu yule anayemtumaini.

Au:
Mt.11:28

Bwana asema: Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, sisi tulioshibishwa na sadaka kubwa namna hii, tunakuomba utujalie kuitunza zawadi hiyo iletayo wokovu, wala tusiache kamwe kukusifu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.