JUMAPILI YA 15 YA MWAKA B MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.17:15
Bali mimi nikutazame uso wako katika haki, niamkapo nishibishwe kwa sura yako.

KOLEKTA:
Ee Mungu, unawaonesha mwanga wa ukweli wako wale wanaopotea, ili waweze kurudi kwenye njia ya haki. Uwawezeshe wote ambao, kwa imani wanayoungama, wanahesabiwa kuwa Wakristo, wayakatae mambo yanayopingana na jina hilo, na kuyafuata yale yanayopatana nalo. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Amo.7:12-15
Amazia akamwambia Amosi, Ewe mwonaji, nenda zako, ikimbilie nchi ya Yuda, ukale mkate huko, ukatabiri huko; lakini usitabiri tena huku Betheli; kwa maana ni mahali patakatifu pa mfalme, nayo ni nyumba ya kifalme. Ndipo Amosi akajibu akamwambia Amazia, Mimi sikuwa nabii, wala sikuwa mwana wa nabii; bali nalikuwa mchungaji, na mtunza mikuyu; naye Bwana akanitwaa, katika kufuatana na kundi; Bwana akaniambia, Enenda uwatabirie watu wangu Israeli.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.85:8-13(K)8
1. Na nisikie atakavyosema Mungu BWANA,
Maana atawaambia watu wake amani,
Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,
Utukufu ukae katika nchi yetu.

(K) Ee Bwana utuoneshe rehema zako utupe wokovu wako.

2. Fadhili na kweli zimekutana,
Haki na amani zimehusiana.
Kweli imechipuka katika nchi,
Haki imechungulia kutoka mbinguni. (K)

3. Naam, Bwana atatoa kilicho chema,
Na nchi yetu itatoa mazao yake.
Haki itakwenda mbele zake,
Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia. (K)

SOMO 2: Efe.1:3-14
Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo; kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo. Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake. Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa. Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake. Naye alituzidishia hiyo katika hekima yote na ujuzi; akiisha kutujulisha siri ya mapenzi yake, sawasawa na uradhi wake, alioukusudia katika yeye huyo. Yaani, kuleta madaraka ya wakati mkamilifu atavijumlisha vitu vyote katika Kristo, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani pia. Naam, katika yeye huyo; na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake. Nasi katika huyo tupate kuwa sifa ya utukufu wake, sisi tuliotangulia kumwekea Kristo tumaini letu. Nanyi pia katika huyo mmekwisha kulisikia neno la kweli, habari njema za wokovu wenu; tena mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa muhuri na Roho yule wa ahadi aliye Mtakatifu. Ndiye aliye arabuni ya urithi wetu, ili kuleta ukombozi wa milki yake, kuwa sifa ya utukufu wake.

SHANGILIO: Yn.1:12,14
Aleluya, aleluya!
Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; Wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu.
Aleluya!

INJILI: Mk.6:7-13
Yesu aliwaita wale Thenashara, akaanza kuwatuma wawili wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu; akawakataza wasichukue kitu cha njiani isipokuwa fimbo tu; wala mkate, wala mkoba, wala pesa za bindoni; lakini wajifungie viatu; akasema, Msivae kanzu mbili. Akawaambia, Mahali po pote mtakapoingia katika nyumba, kaeni humo hata mtakapotoka mahali pale. Na mahali po pote wasipowakaribisha ninyi wala kuwasikia, mtokapo huko, yakung'uteni mavumbi yaliyo chini ya miguu yenu, kuwa ushuhuda kwao. Wakatoka, wakahubiri kwamba watu watubu. Wakatoa pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza.

Nasadiki husemwa.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, uvitazame vipaji vya Kanisa lako likuombalo, ujalie vipokelewe kwa ajili ya kukuza utakatifu wa waamini. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.84:3-4
Shomoro naye ameona nyumba, na mbayuwayu amejipatia kioto, alipoweka makinda yake, kwenye madhabahu zako, ee Bwana wa majeshi, Mfalme wangu na Mungu wangu. Heri wakaao nyumbani mwako, watakuhimidi daima.

Au:
Yn 6:56

Bwana asema: Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, baada ya kuila sadaka hii, tunakuomba matunda ya wokovu wetu yaongezeke kadiri tunavyoshiriki mara nyingi mafumbo haya. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.