Generic placeholder image

JUMAPILI JUMA LA 16 LA MWAKA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Sisi ni watu wake Bwana, kundi linaloongozwa kwa mkono wake: njooni, tumwabudu, aleluya.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI angalia pia AU
Leo ninalipokea
Jina tukufu la Utatu,
Kwa kulitaja hilo jina,
Nafsi tatu Mungu Mmoja,
Mungu Mmoja Nafsi tatu.

Leo najinyenyekeza,
Uweza wa Mungu uniongoze,
Jicho lake liniangalie,
Nguvu zake zidumu nami,
Sikio lake linisikilize.

Hekima ya Mungu wangu inifunze,
Mkono wake unioneshe njia
Yake ngao mimi na inikinge;
Linisemeshe neno la Mungu,
Majeshi yake ya mbinguni yanilinde.

Leo ninalipokea
Jina tukufu la Utatu,
Kwa kulitaja hilo jina,
Nafsi tatu Mungu Mmoja,
Mungu Mmoja Nafsi tatu.

U Muumba wa vitu vyote
Ndiwe Mungu milele milele,
Baba, Roho, Mwana:
Usifiwe Bwana wa wokovu wangu,
Wokovu ulo katika Kristo Bwana.

AU:

Watu wote mwishio duniani,
Kwa shangwe kuu Bwana mwimbieni;
Na kwa furaha mtumikieni,
Sifa yake Bwana itangazeni,
Njooni mbele yake, furahini.

Bwana ni Mungu kweli, mnajua;
Bila ya sisi kumsaidia
Bwana Mungu sote ametuumba;
Sisi ni watu wake, atulisha;
Katufanya kuwa kondoo wake.

Kwani, Bwana Mungu wetu ni mwema:
Milele huruma yake yakini;
Kweli zake zimekuwa thabiti,
Na thabiti daima zitabaki,
Kweli zake zitadumu imara.

Sifa nao utukufu milele
Kutoka kwa watu na malaika
Zimwendee Baba na pia Mwana
Na Roho Mtakatifu pamoja,
Mungu anayeabudiwa pote.

ANT. I: Mshukuruni Bwana, kwa kuwa fadhili zake kuu hazina mwisho, aleluya.

Zab.118 Sala ya shukrani
Huyu ndiye lile Jiwe mlilolikataa ninyi waashi, ambalo sasa limekuwa jiwe kuu la msingi (Mate.4:11)

Mshukuruni Mungu, kwa kuwa ni mwema,*
kwa maana upendo wake mkuu ni wa milele.

Watu wa Israeli waseme:*
"Upendo wake mkuu ni wa milele.“

Wazao wa Aroni waseme:*
“Upendo wake mkuu ni wa milele."

Wote wamchao Mungu waseme:*
"Upendo wake mkuu ni wa milele."

Katika taabu yangu nilimlilia Mungu,*
naye akanisikiliza na kuniokoa.

Mungu yuko nami, siogopi kitu;*
mwanadamu atanifanya nini?

Mungu yuko nami, ananisaidia;*
nami nitashuhudia kushindwa kwa adui zangu.

Ni afadhali kumtumainia Mungu,*
kuliko kumtegemea mwanadamu.

Ni afadhali kumtumainia Mungu,*
kuliko kuwategemea viongozi wa dunia.

Watu wote wasiomjua Mungu walinizingira,*
lakini kwa nguvu ya Mungu nikawapondaponda.

Walinizunguka kila upande,*
lakini kwa nguvu ya Mungu nikawapondaponda.

Walinivamia kwa wingi kama nyuki,/
lakini wakateketea kama kichaka motoni;*
kwa nguvu ya Mungu nikawapondaponda.

Nilishambuliwa mno karibu nishindwe*
lakini Mungu alinisaidia.

Mungu hunijalia nguvu na uhodari;*
yeye mwenyewe ameniokoa.

Sikilizeni sauti za furaha na ushindi/
katika mahema ya watu waadilifu;*
"Mkono wa Mungu umetenda mambo ya ajabu!

Mkono wa Mungu umeleta ushindi!*
Mkono wa Mungu umetenda mambo ya ajabu!"

Sitakufa, bali nitaishi,*
na kutangaza matendo ya Mungu.

Mungu ameniadhibu sana,*
lakini hakuniacha nife.

Nifungulie milango ya Hekalu;*
nitaingia na kumshukuru Mungu!

Huu ndio mlango wa Mungu,*
ambao waadilifu waweza kuupitia.

Nakushukuru, Ee Mungu, kwa kunisikiliza;*
kwa sababu wewe umeniokoa.

Jiwe walilolikataa waashi,*
limekuwa jiwe kuu la msingi.

Jambo hili limefanywa na Mungu;*
nalo ni jambo la ajabu mno kwetu.

Hi ndiyo siku aliyoifanya Mungu;*
basi, tushangilie na kufurahi.

Utuokoe, Ee Mungu, utuokoe!*
Ee Mungu, tunakusihi, utupe fanaka!

Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Mungu!*
Twakubariki kutoka nyumbani mwa Mungu.

Mungu ni Mungu, naye ni mwema kwetu./
Shikeni matawi mikononi, anzeni sherehe,*
mkiandamana mpaka madhabahuni.

Ndiwe Mungu wangu, ninakushukuru*
ninakutukuza, Ee Mungu wangu.

Mshukuruni Mungu kwa kuwa ni mwema,*
kwa maana upendo wake mkuu ni wa milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Mshukuruni Bwana, kwa kuwa fadhili zake kuu hazina mwisho, aleluya.

ANT. II: Aleluya, viumbe vyote vya Bwana, msifuni Bwana, aleluya.

WIMBO: Dan.3:52-56 Kila kiumbe kimsifu Bwana
Mwumba astahili sifa milele (Rom.1:25)

Umehimidiwa, Ee Bwana, MUNGU wa baba zetu;*
Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.

Limehimidiwa jina lako takatifu, tukufu;*
Lastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.

Umehimidiwa katika hekalu la fahari yako takatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Umehimidiwa juu ya kiti cha ufalme wako,*
Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.

Umehimidiwa utazamaye vilindi, uketiye juu ya makerubi;*
Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.

Umehimidiwa katika anga la mbinguni*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Tumtukuze Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Umehimidiwa katika anga la mbinguni,*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Aleluya, viumbe vyote vya Bwana, msifuni Bwana, aleluya.

ANT. III: Kila kitu chenye uhai, na kimsifu Bwana, aleluya.

Zab.150 Zaburi ya kumsifu Mungu
Msifuni Mungu rohoni mwenu, msifuni kwa mioyo yenu, yaani: mtukuzeni Mungu kwa roho na kwa mwili (Hesychius)

Msifuni Mungu Hekaluni mwake;*
msifuni kwa ajili ya enzi yake mbinguni.

Msifuni kwa ajili ya matendo yake makuu;*
msifuni kwa ajili ya utukufu wake mkuu.

Msifuni kwa mlio wa tarumbeta;*
msifuni kwa zeze na kinubi!

Msifuni kwa ngoma na michezo;*
msifuni kwa filimbi na bango!

Msifuni kwa kupiga matoazi;/
msifuni kwa kuvumisha matoazi.*
Kila kiumbe chenye uhai na kimsifu Mungu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Kila kitu chenye uhai, na kimsifu Bwana, aleluya.

SOMO: 2Tim.2:8,11-13
Mkumbuke Yesu Kristo aliyefufuliwa kutoka wafu, aliyekuwa wa ukoo wa Daudi, kama isemavyo Injili ninayoihubiri. Usemi huu ni wa kweli: "Ikiwa tulikufa pamoja naye, tutaishi pia pamoja naye. Tukiendelea kuvumilia, tutatawala pia pamoja naye. Tukimkana, naye pia atatukana. Tukikosa kuwa waaminifu, Yeye hubaki mwaminifu daima, maana yeye hawezi kujikana mwenyewe."

KIITIKIZANO
K. Tunakushukuru, Ee Mungu, na tunaomba msaada kwa jina lako. (W. Warudie)
K. Tunasimulia matendo yako ya ajabu.
W. Na tunaomba msaada kwa jina lako.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Tunakushukuru...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Yesu aliwaona watu, makundi kwa makundi, akawaonea huruma kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Yesu aliwaona watu, makundi kwa makundi, akawaonea huruma kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji.

MAOMBI
Utukufu, enzi, nguvu na uwezo viwe kwa Mungu Mmoja, Mwokozi wetu, kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu, daima na milele.
W. Tunakusifu, Ee Mungu: twakiri ya kuwa wewe ndiwe Bwana.

Tunakutukuza, Bwana, Mwumba wa ulimwengu. Sisi tulikuwa wakosefu tuliohitaji neema yako:
- hata hivyo, ulitupa mwito tukujue na tukutumikie katika maisha yetu. (W.)

Mwanao ametuonesha njia.
- Tunapozifuata nyayo zake, utusaidie tusiiache njia hiyo iongozayo kwenye uzima. (W.)

Tunaadhimisha leo ufufuko wa Mwanao:
- katika mateso na starehe, tunaomba ufufuko huo utupatie furaha ya kweli. (W.)

Ee Bwana, utujalie moyo wa sala na shukrani:
- utuwezeshe kukushukuru daima na popote. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana, utufadhili sisi tunaokutumikia, na kwa wema wako, utuongezee neema zako: ili, tukiwa na moyo wa imani, matumaini na mapendo, tuweze daima kuwa macho, na kuendelea kuzishika amri zako. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.