Generic placeholder image

JUMAPILI JUMA LA 16 LA MWAKA
MASIFU YA JIONI I

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya

UTENZI
Atukuzwe Bwana Mungu wetu!
Mbingu na ziimbe kwa furaha;
Dunia iimbe mbele yake
Nyimbo zake za heshima kuu!
Yatangazwe matendo makuu;
Usifiwe wake utukufu;
Sauti zote na zipalizwe
Kwa Mungu Mfalme mtukufu!

Vyote viishivyo na kupumua
Vishukuru kwa nyimbo za dhati;
Vitu vyote vimwimbie Yeye
Astahiliye sifa zote!
Tangazeni upendo wa Baba,
Katupatia Mungu Mwanae;
Msifuni Roho tulompata
Aliye mmojawao milele.

ANT. I: Salini kwa ajili ya amani ya Yerusalemu.

Zab.122 Sifa za Yerusalemu
Mmefika mlimani Sion, kwenye mji wa Mungu aliye hai. Mmefika Yerusalemu, mji wa mbinguni (Ebr.12:22)

Nalifurahi waliponiambia:*
"Twende nyumbani kwa Mungu“

Sasa sisi tumekwisha wasili,*
tumesimama milangoni mwa Yerusalemu!

Yerusalemu, mji uliorekebishwa,*
kwa mpango mzuri na umetengemaa!

Humo ndimo makabila yanafika,/
naam, makabila ya Israeli,*
kumshukuru Mungu kama alivyoagiza.

Humo mna mahakama ya haki,*
mahakama ya kifalme ya Daudi.

Uombeeni Yerusalemu amani;*
"Wote wakupendao wafanikiwe!

Ukumbini mwako muwe na amani,*
majumbani mwako uweko usalama!"

Kwa ajili ya jamaa na ndugu zangu,*
ee Yerusalemu, nakutakia amani!

Kwa ajili ya nyumba ya Mungu, Mungu wetu,*
hinakuombea upate fanaka!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Salini kwa ajili ya amani ya Yerusalemu.

ANT. II: Toka alfajiri hadi usiku, roho yangu yamtamani Bwana.

Zab.130 Kuomba msaada
Yeye atawaokoa watu wake (Mt.1:21)

Katika unyonge wangu, nakulilia, Ee Mungu./
Ee Bwana, sikiliza sauti yangu,*
uitegee sikio sauti ya ombi langu.

Kama, Ee Mungu, ungeweka kumbukumbu ya madhambi yetu,*
ni nani, Ee Bwana, angeweza kusimama mbele yako?

Lakini wewe watusamehe dhambi,*
ili tukutumikie kwa uchaji.

Naweka tumaini langu lote kwa Mungu;*
nina imani sana na neno lake.

Namngojea Mungu kwa hamu kubwa,/
kuliko mlinzi usiku anavyongojea, pambazuko;*
kuliko walinzi wanavyongojea kupambazuke.

Ee Israeli, umtumainie Mungu,/
maana yeye ni mwenye upendo mkuu;*
daima yuko tayari kutuokoa.

Naam, atawaokoa watu wa Israeli,*
katika maovu yao yote.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Toka alfajiri hadi usiku, roho yangu yamtamani Bwana.

ANT. III: Kila kiumbe, mbinguni na duniani, kilipigie goti jina la Yesu, aleluya.

WIMBO: Filp:2:6-11 Kristo, mtumishi wa Mungu
Kristo Yesu, kwa asili,*
alikuwa daima Mungu;

lakini hakufikiri kwamba/
kule kuwa sawa na Mungu*
ni kitu cha kung'ang'ania kwa nguvu.

Bali, kwa hiari yake mwenyewe,*
aliachilia hayo yote,

akajitwalia hali ya mtumishi,/
akawa sawa na wanadamu,*
akaonekana kama wanadamu.

Alijinyenyekeza na kutii mpaka kufa,*
hata kufa msalabani.

Kwa sababu hiyo*
Mungu alimkweza juu kabisa,

akampa jina lililo kuu zaidi*
kuliko majina yote.

Ili kwa heshima ya jina la Yesu,/
viumbe vyote mbinguni, duniani na kuzimu,*
vipige magoti mbele yake;

Na kila mtu akiri /
kwamba Yesu Kristo ni Bwana,*
kwa utukufu wa Mungu Baba.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Kila kiumbe, mbinguni na duniani, kilipigie goti jina la Yesu, aleluya.

SOMO: 2Pet.1:19-20
Ujumbe wa manabii watuthibitishia jambo hilo; nanyi mwafanya vema kama mkiuzingatia, maana ni kama taa inayoangaza mahali penye giza mpaka Siku ile itakapopambazuka, na mwanga wa nyota ya asubuhi utakapong'ara mioyoni mwenu. Zaidi ya hayo, lakini, kumbukeni kwamba hakuna mtu ye yote awezaye kufafanua mwenyewe unabii ulio katika Maandiko matakatifu.

KIITIKIZANO
K. Tangu mawio ya jua hata machweo yake, jina la Bwana litukuzwe. (W. Warudie)
K. Utukufu wake u juu ya mbingu.
W. Jina la Bwana litukuzwe.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Tangu...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Utawala wa mbinguni umefanana na chachu aliyotwaa mwanamke mmoja, akaichanganya na unga madebe matatu, hata unga wote ukaumuka.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Utawala wa mbinguni umefanana na chachu aliyotwaa mwanamke mmoja, akaichanganya na unga madebe matatu, hata unga wote ukaumuka.

MAOMBI
Tumwombe Kristo, ambaye huwajalia nduguze mapendo kwa wema wake.
W. Bwana Yesu, sikia sala zetu.

Mzaliwa wa kwanza kutoka wafu, umetutakasa kwa damu yako;
- utuwezeshe kuyaelewa yote uliyotutendea. (W.)

Umetuita tuwe watangazaji wa neno lako:
- utusaidie tuweze kuelewa undani wa neno hilo, na kuishi kadiri ya ujumbe wako. (W.)

Mfalme wa amani, uwaongoze watawala:
- na Roho wako aiamshe mioyo yao, ili wawahudumie wale waliotupwa na jumuiya zao. (W.)

Uwaongoze wanaokandamizwa na kudhulumiwa kwa sababu ya utaifa, rangi au dini:
- utu wao na haki zao zitambuliwe na kuheshimiwa. (W.)

Uwapokee wote waliokufa katika amani yako;
- uwapeleke kwenye uzima wa milele pamoja na Mama yetu, Bikira Maria, na watakatifu wote. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana, utufadhili sisi tunaokutumikia, na kwa wema wako, utuongezee neema zako: ili, tukiwa na moyo wa imani, matumaini na mapendo, tuweze daima kuwa macho, na kuendelea kuzishika amri zako. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.