Generic placeholder image

JUMAPILI JUMA LA 16 LA MWAKA
MASIFU YA JIONI II

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya

UTENZI tazama pia AU
Ee Mungu twasifu lako jina;
Bwana wa wote twakusujudia!
Vyote duniani enzi vyakiri
Na vyote mbinguni vyakuabudu.
Milki yako haina mipaka,
Ni wa milele wako utawala.

Sikilizeni! Utenzi wa mbingu!
Malaika waimba kwa sauti;
Makerubi na pia Maserafi
Kwa sauti tamu hujaza mbingu
Waimba na kusifu bila mwisho:
Mtakatifu 'takatifu Bwana.

Mtakatifu Baba, pia Mwana,
Mtakatifu Roho, E Utatu.
U Mmoja tu katika udhati
Mungu usiyegawanyika katu;
Twakuabudu tukipiga goti,
Wakati hilo fumbo twaungama.

E Bwana waokoe watu wako
Waliozungukwa na majaribu;
Tusaidie twepe dhambi leo
Situache kamwe tuvurugike.
Loo, tumaini langu ni kwako,
Bwana usiniache peke yangu.

AU

Msifu Mfalme wa mbinguni,
Miguuni pake peleka ushuru wako;
Amenikomboa na kuniponya,
Kanitia nguvu, kanisamehe;
Nani basi kama mimi apaswa kuimba?
Msifu Yeye! Msifu Yeye!
Msifu Yeye! Msifu Yeye!
Msifu Mfalme wa milele.

Msifu kwa hisani aloonesha
Kwa baba zetu mahangaikoni;.
Msifu Yeye asobadilika milele,
Si mwepesi wa kukaripia
Ni mwepesi wa kubariki;
Msifu Yeye! Msifu Yeye!
Msifu Yeye! Msifu Yeye!
Katika uaminifu wake ni Mkuu.

Atutunza na kuturehemu kama baba;
Udhaifu wetu aujua vema,
Kwa upole anatuchukua
Na kutujaza matumaini,
Hutuokoa na adui zetu wote;
Msifu Yeye! Msifu Yeye!
Msifu Yeye! Msifu Yeye!
Kama huruma yake ilivyoenea.

Enyi malaika tusaidieni,
Na tusaidieni kumuabudu Yeye;
Ninyi mwamwona Yeye uso kwa uso;
Jua na mwezi mbele zake inameni,
Vyote vilivyoko wakati wote angani.
Msifuni Yeye! Msifuni Yeye!
Msifuni Yeye! Msifuni Yeye!
Pamoja nasi msifuni Mungu Mhisani.

ANT. I: Katika utukufu mkuu nilikuzaa, kabla ya alfajiri, aleluya.

Zab.110:1-5,7 Kutawazwa kwa mfalme mteule
Kristo sharti atawale mpaka Mungu atakapowashinda adui zake na kuwaweka chini ya miguu yake (1Kor.15:25)

Mungu amemwambia bwana wangu,*
"Keti upande wangu wa kulia,

Mpaka niwafanye maadui zako,*
kama kibao cha kuegemea miguu yako."

Toka Sion Mungu ataeneza enzi yako.*
Asema: "Tawala juu ya adui zako!"

Watu wako watajitolea,*
siku utakapopambana na adui.

Vijana wako watakujia kwenye milima mitakatifu,*
kama vile umande wa asubuhi.

Mungu ameapa, wala hataghairi:/
"Kwamba wewe ni kuhani milele,*
kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki."

Mungu yuko upande wako wa kulia;*
atakapokasirika, atawaponda wafalme.

Njiani mfalme atakunywa maji ya kijito;*
kwa hiyo atainua kichwa juu kwa ushindi.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Katika utukufu mkuu nilikuzaa, kabla ya alfajiri, aleluya.

ANT. II: Heri walio na njaa na kiu ya kufanya atakavyo Mungu, maana watashibishwa.

Zab.112 Furaha ya mtu mwema
Ishini kama watoto wa mwanga; maana matokeo ya mwanga ni wema kamili, uadilifu na ukweli. (Ef.5:8-9)

Heri mtu anayemcha Mungu,*
anayefurahia sana kutii amri zake.

Watoto wake watakuwa wenye enzi duniani;*
wazao wake watabarikiwa.

Jamaa yake itakuwa tajiri,*
naye atakuwa na fanaka daima.

Watu wema huangaziwa mwanga wa furaha,/
kama vile taa iangazavyo gizani;*
naam, watu wenye huruma, wapole na waadilifu.

Heri mtu mkarimu, akopeshaye bila faida;*
aendeshaye shughuli zake kwa kutumia haki.

Mwadilifu hatashindwa kamwe,*
na atakumbukwa daima.

Akipata habari mbaya haogopi;*
moyo wake ni thabiti na humtumainia Mungu.

Hana wasiwasi, wala haogopi;*
ana hakika adui zake watashindwa.

Huwapa maskini kwa ukarimu;/
wema wake haubadiliki.*
Mtu wa namna hiyo atasifika daima.

Waovu huona hayo na kuudhika;/
husaga meno kwa chuki na kutoweka,*
mambo huenda kinyume cha matazamio yao.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Heri walio na njaa na kiu ya kufanya atakavyo Mungu, maana watashibishwa.

ANT. III: Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote, wakubwa kwa wadogo, aleluya.

WIMBO: Ufu.19:1,2,5-7 Arusi ya Mwana-kondoo

Aleluya.
Wokovu, utukufu na nguvu ni mali yake Mungu wetu!*
(W. Aleluya)
Maana hukumu yake ni ya kweli na ya haki.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Msifuni Mungu enyi watumishi wake wote,*
(W. Aleluya)
Nanyi nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Bwana, Mungu wetu Mwenyezi , ni Mfalme!*
(W. Aleluya)
Tufurahi na kushangilia; tumtukuze.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Wakati wa arusi ya Mwana-kondoo umefika,*
(W. Aleluya)
Na bibi arusi yuko tayari.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Atukuzwe Baba na Mwana, na Roho Mtakatifu,*
(W. Aleluya)
Kama mwanzo na sasa na siku zote, na milele. Amina.*
W. Aleluya (aleluya).

Ant. III: Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote, wakubwa kwa wadogo, aleluya.

SOMO: Ebr.12:22-24
Lakini ninyi mmefika mlimani Sion, kwenye mji wa Mungu aliye hai. Mmefika Yerusalemu, mji wa mbinguni, ambapo wamekusanyika malaika elfu nyingi wasiohesabika. Mmefika kwenye kusanyiko kubwa la wazaliwa wa kwanza wa Mungu, ambao majina yao yameandikwa mbinguni. Mnasimama mbele ya Mungu aliye hakimu wa wote, na mbele ya roho za watu waadilifu waliofanywa kuwa wakamilifu. Mmefika kwa Yesu ambaye ameratibisha Agano jipya, na ambaye damu yake iliyomwagika inasema mambo mema zaidi kuliko ile ya Abeli.

KIITIKIZANO
K. Bwana Mungu wetu ni Mwenyezi, uwezo wake ni mkuu. (W. Warudie)
K. Hekima yake haina mipaka.
W. Uwezo wake ni mkuu.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Maria amechagua kitu bora zaidi, ambacho hakuna mtu atakayekiondoa kwake.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Maria amechagua kitu bora zaidi, ambacho hakuna mtu atakayekiondoa kwake.

MAOMBI
Kwa njia ya Kanisa, Mungu ametujulisha nia yake ya kuviunganisha vitu vyote katika Kristo. Tuombe ili matakwa yake yatimizwe.
W. Baba, uviunganishe vitu vyote katika Kristo.

Tunakushukuru kwa uwepo na nguvu ya Roho wako katika Kanisa:
- utupe ari na moyo wa kutafuta umoja, kusali pamoja na kufanya kazi kwa ushirika. (W.)

Tunakushukuru kwa kutujalia watu ambao kazi zao zautangaza upendo wako:
- utusaidie tuweze kuzihudumia jumuiya zetu. (W.)

Baba, uwatunze wote wanaolitumikia Kanisa lako kwa kuhubiri neno lako na kuadhimisha sakramenti:
- uwawezeshe kuwakusanya wanao wote katika umoja alioomba Kristo. (W.)

Watu wako wamekwisha elewa hasara ya vita na chuki:
- uwajalie waweze kufurahia amani walioachiwa na Mwanao. (W.)

Uwatimizie matumaini yao wale waliofariki dunia katika amani yako:
- uwafikishe kwenye ufufuko wa mwisho, utakapokuwa yote katika yote. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana, utufadhili sisi tunaokutumikia, na kwa wema wako, utuongezee neema zako: ili, tukiwa na moyo wa imani, matumaini na mapendo, tuweze daima kuwa macho, na kuendelea kuzishika amri zako. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.