Generic placeholder image

JUMAPILI JUMA LA 16 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Baba wa milele, Mungu wa pendo,
Ambaye kwa vumbi ulituumba,
Tugeuze kwa neema ya Roho,
Tutie thamani tulio duni.

Utuandae kwa siku ya siku
Atakapokuja Kristo kwa enzi
Kutugeuza tena toka vumbi
Na miili yetu kuing'arisha.

Ee Mungu, hujaonwa, hujaguswa,
Viumbe vyote vyakudhihirisha;
Mbegu ya utukufu ndani mwetu
Itachanua tutapokuona.

ANT. I: Ye yote aulaye mkate huu ataishi milele, aleluya.

Zab.23 Mungu mchungaji wetu
Mwana-kondoo atakuwa mchungaji wao, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji ya uzima (Ufu.7:17)

Mungu ni mchungaji wangu;*
sitapungukiwa chochote,

Hunipumzisha kwenye malisho mabichi;/
huniongoza kwenye maji matulivu na safi,*
na kunirudishia nguvu.

Huniongoza katika njia iliyo sawa,*
kwa ajili ya jina lake.

Nijapopita katika giza kuu, sitaogopa,/
kwa kuwa wewe Mungu u pamoja nami;*
fimbo yako na bakora yako vyanilinda.

Waniandalia karamu mbele ya adui zangu;/
umenipaka mafuta kichwani mwangu,*
na kikombe changu wakijaza mpaka kufurika.

Hakika wema wako na upendo wako mkuu,/
vitakuwa pamoja nami maisha yangu yote.*
Nitakaa nyumbani mwako muda wote niishipo.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Ye yote aulaye mkate huu ataishi milele, aleluya.

ANT. II: Bwana atakuja kwa utukufu, na atafanya maajabu kwa ajili ya watakatifu wake, aleluya.

Zab.76 Mungu Mshindi
Watamwona Mwana wa Mtu akija juu ya mawingu ya angani (Mt.24:30)

I
Mungu anajulikana katika Yuda;*
jina lake ni kuu katika Israeli.

Hema lake liko huko Salemu;*
makao yake yako huko Sion.

Huko alivunja mishale ya adui;*
alivunja ngao, panga na silaha.

Wewe, Ee Mungu, watukuka mno;/
umejaa fahari kuu unaporudi,*
kutoka milimani ulikowashinda adui.

Washupavu wao wamenyang'anywa nyara zao,/
sasa wanalala usingizi wao wa mwisho,*
ushujaa wao wote haukuwafaa kitu.

Ulipowakemea, Ee Mungu wa Yakobo,*
farasi na wapanda farasi walikufa ganzi.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana atakuja kwa utukufu, na atafanya maajabu kwa ajili ya watakatifu wake, aleluya.

ANT. III: Mtoleeni Bwana Mungu wenu sala na zawadi, aleluya.

II
Wewe, Ee Mungu, ni wa kutisha mno!*
Nani awezaye kustahimili ukikasirika?

Umejulisha hukumu yako toka mbinguni,*
nayo dunia ikaogopa na kunyamaa;

wakati ulipoinuka, Ee Mungu, kutoa hukumu,*
kuwaokoa wote wanaodhulumiwa duniani.

Ghadhabu ya watu husababisha tu sifa kwako;*
na walioponea huko Emati watafanya sikukuu zako.

Mpeni Mungu, Mungu wenu, yale mliyoahidi;*
enyi mlio karibu, mpeni vipaji Mungu wa kutisha.

Yeye huwanyenyekesha wakuu;*
huwatisha wafalme wa dunia.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Dunia iliogopa, ikakaa kimya, Mungu aliposimama kuihukumu.

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: 1Kor.6:19-20
Je, hamjui kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, ambaye mlimpokea kutoka kwa Mungu? Ninyi, basi, si mali yenu wenyewe. Mlinunuliwa kwa bei kubwa. Kwa hiyo, itumieni miili yenu kwa ajili ya kumtukuza Mungu.

K. Roho yangu inatamani na kuonea shauku maskani ya Bwana.
W. Moyo wangu na roho yangu humfanyia shangwe Mungu aliye hai.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Adhuhuri: Kum.10:12
BWANA, Mungu wako, anataka nini kwako, ila umche BWANA, Mungu wako, na kwenda katika njia zake zote, na kumpenda, na kumtumikia BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote.

K. Ee Bwana, nani atakaribishwa patakatifu pako?
W. Ni mtu aendaye kwa ukamilifu, na anenaye ukweli kutoka moyoni mwake.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Wim.8:6b-7
Kwa maana upendo una nguvu kama mauti, Na wivu ni mkali kama ahera. Mwako wake ni mwako wa moto, Na miali yake ni miali ya Yahu. Maji mengi hayawezi kuuzimisha upendo, Wala mito haiwezi kuuzamisha.

K. Nakupenda, Bwana, uliye nguvu yangu.
W. Wewe ni mlinzi na mwokozi wangu mwenye

SALA:
Tuombe: Bwana, utufadhili sisi tunaokutumikia, na kwa wema wako, utuongezee neema zako: ili, tukiwa na moyo wa imani, matumaini na mapendo, tuweze daima kuwa macho, na kuendelea kuzishika amri zako. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.