Generic placeholder image

JUMAPILI JUMA LA 17 LA MWAKA
MASIFU YA JIONI I

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Ewe mwangavu Mwanga wa Mungu
Utukufu wake yeye Baba,
Kwako wewe, Ee Kristo,
Kwako Bwana ndio tunaimba;
Pamoja na nyota ya jioni,
Wakati jua linapotua,
Sala zetu tunakutolea.

Wastahili sifa milele
Usifiwe Baba nawe Mwana,
Pia wewe Roho wake Mungu,
Uliye Mtakatifu sana.
Na ulimwengu wakutukuza
Unakushukuru, Ee Kristo
Uliyetoa uzima wako.

ANT. I: Ee Bwana, sala yangu ipae mbele yako kama moshi wa ubani.

Zab.141.1-9 Habari za tamaa mbaya
Moshi wa ubani ukapanda juu, pamoja na sala za watu wa Mungu, kutoka mikononi mwake huyo malaika aliyekuwa mbele ya Mungu (Ufu.8:4)

Nakulilia, Ee Mungu, uje hima kunisaidia!*
Usikilize sauti yangu ninapokulilia!

Sala zangu uzipokee kama ubani;/
kuinuliwa kwa mikono yangu*
kuwe kama sadaka ya jioni.

Ee Mungu, uweke ulinzi kinywani pangu,*
weka uangalizi mdomoni mwangu.

Unikinge nisielekee kufanya mabaya,/
nisijiunge na upotovu wa watu waovu;*
na nisishiriki kamwe katika karamu zao.

Kwa faida yangu, mtu mwema na anionye kwa kunipiga,/
lakini sikubali kamwe kusifiwa na wabaya,*
maana nasali daima dhidi ya maovu yao.

Wakuu wao watakapopondwa miambani,*
ndipo watakapotambua ukweli wa maneno yangu.

Mifupa yao imetawanywa mdomoni pa kuzimu*
kama vipande vya kuni na mawe ardhini!

Bali mimi nakuamini, Ee Mungu, Mungu wangu;*
wewe ni kimbilio langu, usiniache bila ulinzi.

Unikinge na mitego waliyonitegea,*
uniepushe na matanzi ya hao watu waovu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Ee Bwana, sala yangu ipae mbele yako kama moshi wa ubani.

ANT. II: Bwana, wewe ndiwe kimbilio langu; ndiwe urithi wangu katika nchi ya walio hai.

Zab.142 Dua ya mtu aliyeachwa pweke
Hayo yote yametimia katika mateso ya Bwana (Mt. Hilari)

Namlilia Mungu kwa sauti,*
namsihi Mungu kwa kilio.

Natoa malalamiko yangu mbele yake,*
namweleza mahangaiko yangu yote.

Ninapokaribia kukata tamaa kabisa,/
yeye yupo, anajua mwenendo wangu.*
Adui wamenitegea mtego njiani mwangu.

Nikiangalia huku na huko,*
hakuna mtu wa kunisaidia;

sina tena mahali pa kukimbilia,*
Wewe ni kimbilio langu.

Wewe ndiwe yote niliyo nayo*
katika nchi ya walio hai.

Usikilize kilio changu, maana nimekuwa hoi;*
uniokoe na adui zangu, maana wamenizidi nguvu.

Unitoe humu kifungoni,*
nipate kulisifu jina lako

kati ya jamii ya waadilifu;*
kwasababu wewe umenitendea mema.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana, wewe ndiwe kimbilio langu; ndiwe urithi wangu katika nchi ya walio hai.

ANT. III: Bwana Yesu alijinyenyekeza; kwa hiyo Mungu amemtukuza sana milele.

WIMBO: Filp.2:6-11 Kristo, mtumishi wa Mungu
Yesu, kwa asili,*
alikuwa daima Mungu;

lakini hakufikiri kwamba/
kule kuwa sawa na Mungu*
ni kitu cha kung'ang'ania kwa nguvu.

Bali, kwa hiari yake mwenyewe,*
aliachilia hayo yote,

akajitwalia hali ya mtumishi/
akawa sawa na wanadamu,*
akaonekana kama wanadamu.

Alijinyenyekeza na kutii mpaka kufa,*
hata kufa msalabani.

Kwa sababu hiyo*
Mungu alimkweza juu kabisa,

akampa jina lililo kuu zaidi*
kuliko majina yote.

Ili kwa heshima ya jina la Yesu,/
viumbe vyote mbinguni, duniani na kuzimu,*
vipige magoti mbele yake;

Na kila mtu akiri/
Kwamba Yesu Kristo ni Bwana,*
kwa utukufu wa Mungu Baba.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Bwana Yesu alijinyenyekeza; kwa hiyo Mungu amemtukuza sana milele.

SOMO: Rom.11:33-6
Utajiri, hekima na elimu ya Mungu ni kuu mno! Huruma zake hazichunguziki, na njia zake hazieleweki! Kama yasemavyo Maandiko matakatifu: "Nani aliyepata kuyajua mawazo ya Bwana? Nani awezaye kuwa mshauri wake? Au, nani aliyempa yeye kitu kwanza hata aweze kukilipwa tena kitu hicho?" Kwa maana vitu vyote vyatoka kwake, vyote vipo kwa uwezo wake na kwa ajili yake. Utukufu na uwe kwake hata milele! Amina.

KIITIKIZANO
K. Jinsi yalivyo makuu matendo yako, Ee Bwana! (W. Warudie)
K. Yote umeyafanya kwa hekima.
W. Matendo yako, Ee Bwana!
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Jinsi...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Utawala wa mbinguni umefanana na mfanyabiashara atafutaye lulu nzuri. Akisha ipata lulu ya thamani kubwa, huuza yote aliyo nayo, na kuinunua hiyo lulu.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Utawala wa mbinguni umefanana na mfanyabiashara atafutaye lulu nzuri. Akisha ipata lulu ya thamani kubwa, huuza yote aliyo nayo, na kuinunua hiyo lulu.

MAOMBI
Tusali kwa unyenyekevu tukimtukuza Mungu Mmoja, Baba na Mwana na Roho Mtakatifu:
W. Bwana, uwe pamoja na watu wako.

Mungu Mwenyezi, utujalie haki istawi duniani,
- ili watu wako wapate kuishi kwa furaha katika amani yako. (W.)

Uwaingize watu wote katika ufalme wako,
- ili wanadamu wote wapate kuokoka. (W.)

Uwajalie watu wa ndoa wadumu katika amani, na waishi kadiri ya matakwa yako;
- uwawezeshe kuishi pamoja kwa mapendo siku zote. (W.)

Uwape tuzo wale wote waliotupatia msaada,
- na uwajalie uzima wa milele. (W.)

Uwahurumie wale waliopoteza maisha yao kwa sababu ya chuki au vita,
- uwapokee kwako mbinguni kwenye raha na faraja. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu

Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, mlinzi wa wale wanaokutumainia, pasipo wewe hakuna lililo thabiti, hakuna lililo takatifu: ututegemeze daima kwa upendo wako. Utuelekeze jinsi ya kutumia vitu vya ulimwengu huu hata tuweze, kwa wakati huu, kuzingatia yale yanayodumu milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.