JUMAPILI YA 17 YA MWAKA B MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.68:5-6,35
Mungu yu katika kao lake takatifu; Mungu huwakalisha wapweke nyumbani, Yeye huwapa watu wake nguvu na uwezo.

KOLEKTA:
Ee Mungu, wewe ndiwe ngao yao wote wanaokukimbilia. Pasipo wewe hapana kilicho thabiti wala kitakatifu. Utuzidishie rehema yako, ili kwa mamlaka na maongozi yako, tupate kuzitumia mali za muda huu kwa namna inayotuwezesha kuambatana na zile zinazodumu milele. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: 2Fal.4:42-44
Alikuja mtu kutoka Baal-shalisha, akamletea mtu wa Mungu chakula cha malimbuko, mikate ishirini ya shayiri, na masuke mabichi ya ngano guniani. Akasema, Uwape watu, ili wale. Na mtumishi wake akasema, Je! Niwaandikie hiki watu mia? Lakini akasema, Uwape watu, ili wale; kwa kuwa Bwana asema hivi, Watakula na kusaza. Basi akawaandikia, nao wakala, wakasaza, sawasawa na neno la Bwana.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.145:10-11,15-18(K)16
1. Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru,
Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
Wataunena utukufu wa ufalme wako,
Na kuuhadithia uweza wako.

(K) Waufumbua mkono wako, wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake.

2. Macho ya watu yakuelekea Wewe,
Nawe huwapa chakula chao wakati wake.
Waufumbua mkono wako,
Wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake. (K)

3. Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote,
Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote.
Bwana yu karibu na wote wamwitao,
Wote wamwitao kwa uaminifu. (K)

SOMO 2: Efe:4.1-6
Nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.

SHANGILIO: Yn.14:6
Aleluya, aleluya!
Mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima, asema Bwana; Mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya!

INJILI: Yn.6:1-15
Yesu alikwenda zake ng'ambo ya Bahari ya Galilaya, nayo ndiyo ya Tiberia. Na mkutano mkuu wakamfuata, kwa sababu waliziona ishara alizowafanyia wagonjwa. Naye Yesu akakwea mlimani, akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. Na Pasaka, sikukuu ya Wayahudi, ilikuwa karibu. Basi Yesu alipoinua macho yake akaona mkutano mkuu wanakuja kwake, alimwambia Filipo, Tununue wapi mikate, ili hawa wapate kula? Na hilo alilinena ili kumjaribu; kwa maana alijua mwenyewe atakalotenda. Filipo akamjibu, Mikate ya dinari mia mbili haiwatoshi, kila mmoja apate kidogo tu. Wanafunzi wake mmojawapo, Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, Yupo hapa mtoto, yuna mikate mitano ya shayiri na samaki wawili, lakini hivi ni nini kwa watu wengi kama hawa? Yesu akasema, Waketisheni watu. Na mahali pale palikuwa na majani tele. Basi watu waume wakaketi, wapata elfu tano jumla yao. Basi Yesu akaitwaa ile mikate, akashukuru, akawagawia walioketi; na kadhalika katika wale samaki kwa kadiri walivyotaka. Nao waliposhiba, aliwaambia wanafunzi wake, Kusanyeni vipande vilivyobaki, kisipotee cho chote. Basi wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili, vipande vya mikate mitano ya shayiri vilivyowabakia wale waliokula. Basi watu wale, walipoiona ishara aliyoifanya, walisema, Hakika huyu ni nabii yule ajaye ulimwenguni. Kisha Yesu, hali akitambua ya kuwa walitaka kuja kumshika ili wamfanye mfalme, akajitenga, akaenda tena mlimani yeye peke yake.

Nasadiki husemwa.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba uvipokee vipaji. hivi tunavyokutolea kutoka wingi wa vitu ulivyotukirimia. Kwa nguvu tendaji ya neema yako mafumbo haya matakatifu yatakatifuze mwenendo wetu wa maisha ya sasa, na kutufikisha kwenye furaha za milele. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.103:2
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, wala usizisahau fadhili zake zote.

Au:
Mt.5:7-8

Heri wenye rehema, maana hao watapata rehema. Heri wenye moyo safi, maana hao watamwona Mungu

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, tumepokea sakramenti ya kimungu, ambayo ni ukumbusho wa daima wa Mateso ya Mwanao. Tunakuomba zawadi hii aliyotujalia Mwanao kwa mapendo yasiyo na kifani ituletee wokovu. Anayeishi na kutawala milele na milele.