JUMAPILI YA 19 YA MWAKA B

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.74:20,19,22,23
Ee Bwana, ulitafakari agano, usisahau milele uhai wa watu wako walioonewa. Ee Mungu, usimame, ujitetee mwenyewe, usiisahau sauti ya watesi wako.

KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi wa milele, kwa kufundishwa na Roho Mtakatifu tunathubutu kukuita Baba. Uikamilishe mioyoni mwetu roho ya kuwa wana, ili tustahili kuingia katika urithi tulioahidiwa. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: 1Fal.19:4-8
Eliya yeye mwenyewe aliendelea katika jangwa mwendo wa siku moja, akaenda akaketi chini ya mretemu. Akajiombea roho yake afe, akasema, Yatosha sasa, Ee Bwana, uiondoe roho yangu; kwa kuwa mimi si mwema kuliko baba zangu. Naye akajinyosha akalala chini ya mretemu; na tazama, malaika akamgusa, akamwambia, Inuka, ule. Akatazama, kumbe! pana mkate umeokwa juu ya makaa, na gudulia la maji, kichwani pake. Akala, akanywa, akaiinyosha tena Malaika wa Bwana akamwendea mara ya pili, akamgusa, akasema. Inuka, ule, maana safari hii ni kubwa mno kwako. Akainuka, akala, akanywa, akaenda katika nguvu za chakula hicho siku arobaini mchana na usiku hata akafika Horebu, mlima wa Mungu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.34:1-8(K)8
1. Nitamhimidi Bwana kila wakati,
Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
Wenyenyekevu wasikie wakafurahi.

(K) Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema.

2. Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
Nalimtafuta Bwana akanijibu,
Akaniponya na hofu zangu zote. (K)

3. Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
Wala nyuso zao hazitaona haya.
Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
Akamwokoa na taabu zake zote. (K)

4. Malaika wa Bwana hufanya kituo,
Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.
Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema;
Heri mtu yule anayemtumaini. (K)

SOMO 2: Efe.4:30-5:2
Msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi. Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya; tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi. Hivyo mfuateni Mungu, kama watoto wanaopendwa; mkaenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi; tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato.

SHANGILIO: Yn.6:63,68
Aleluya, aleluya!
Bwana, maneno yako ni roho tena ni uzima; Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya!

INJILI: Yn.6:41-51
Wayahudi walimnung’unikia Yesu kwa sababu alisema, Mimi ni chakula kilichoshuka kutoka mbinguni. Wakasema, Huyu siye Yesu, mwana wa Yusufu, ambaye twamjua babaye na mamaye? Sasa asemaje huyu, Nimeshuka kutoka mbinguni? Basi Yesu akajibu, akawaambia, Msinung’unike ninyi kwa ninyi. Hakuna mtu awezaye kuja kwangu. asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho. Imeandikwa katika manabii, Na wote watakuwa wamefundishwa na Mungu. Basi kila aliyesikia na kujifunza kwa Baba huja kwangu. Si kwamba mtu amemwona Baba, ila yeye atokaye kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba. Amin, amin, nawaambia, Yeye aaminiye yuna uzima wa milele. Mimi ndimi chakula cha uzima. Baba zenu waliila mana jangwani; wakafa. Hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni, kwamba mtu akile wala asife. Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi mileie. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.

Nasadiki husemwa.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, uwe radhi kuvipokea vipaji vya kanisa lako ulivyotujalia kwa huruma yako tupate kukutolea; nawe kwa uweza wako unavifanya vigeuke kuwa sakramenti ya wokovu kwa ajili yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.147:12.14
Msifu Bwana, ee Yerusalemu, akushibishaye kwa unono wa ngano.

Au:
Yn 6:51

Bwana asema: Chakula nitakachotoa mimi, ni mwili wangu kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, sakramenti yako tuliyoipokea ituokoe na ituimarishe katika nuru ya ukweli wako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.