Generic placeholder image

JUMAPILI 1 MAJILIO
MASIFU YA JIONI I

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Muumba wa nyota za usiku,
Mwanga wa milele wa taifa,
Mkombozi wetu sisi sote,
Utusikie tukuitapo.

Kwa mwili wa Maria 'likuja,
Tuokoke dhambi na aibu,
Kwa neema yako Mkombozi
Sasa njoo tuponye wadhambi.

Na siku ya hukumu ya mwisho,
Sisi tutakapofufuliwa,
Fika Mkombozi mwenye baraka,
Tupeleke rahani milele.
Irvin Udulutsch OSB

ANT. I: Watangazieni watu wote, Bwana atakuja kutuokoa.

Zab.141.1-9 Habari za tamaa mbaya
Moshi wa ubani ukapanda juu, pamoja na sala za watu wa Mungu, kutoka mikononi mwake huyo malaika aliyekuwa mbele ya Mungu (Ufu.8:4)

Nakulilia, Ee Mungu, uje hima kunisaidia!*
Usikilize sauti yangu ninapokulilia!

Sala zangu uzipokee kama ubani;/
kuinuliwa kwa mikono yangu*
kuwe kama sadaka ya jioni.

Ee Mungu, uweke ulinzi kinywani pangu,*
weka uangalizi mdomoni mwangu.

Unikinge nisielekee kufanya mabaya,/
nisijiunge na upotovu wa watu waovu;*
na nisishiriki kamwe katika karamu zao.

Kwa faida yangu, mtu mwema na anionye kwa kunipiga,/
lakini sikubali kamwe kusifiwa na wabaya,*
maana nasali daima dhidi ya maovu yao.

Wakuu wao watakapopondwa miambani,*
ndipo watakapotambua ukweli wa maneno yangu.

Mifupa yao imetawanywa mdomoni pa kuzimu*
kama vipande vya kuni na mawe ardhini!

Bali mimi nakuamini, Ee Mungu, Mungu wangu;*
wewe ni kimbilio langu, usiniache bila ulinzi.

Unikinge na mitego waliyonitegea,*
uniepushe na matanzi ya hao watu waovu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Watangazieni watu wote, Bwana atakuja kutuokoa.

ANT. II: Tazameni, Bwana atakuja pamoja na wateule wake. Siku hiyo utatokea mwanga mkubwa, aleluya.

Zab.142 Dua ya mtu aliyeachwa pweke
Hayo yote yametimia katika mateso ya Bwana (Mt. Hilari)

Namlilia Mungu kwa sauti,*
namsihi Mungu kwa kilio.

Natoa malalamiko yangu mbele yake,*
namweleza mahangaiko yangu yote.

Ninapokaribia kukata tamaa kabisa,/
yeye yupo, anajua mwenendo wangu.*
Adui wamenitegea mtego njiani mwangu.

Nikiangalia huku na huko,*
hakuna mtu wa kunisaidia;

sina tena mahali pa kukimbilia,*
Wewe ni kimbilio langu.

Wewe ndiwe yote niliyo nayo*
katika nchi ya walio hai.

Usikilize kilio changu, maana nimekuwa hoi;*
uniokoe na adui zangu, maana wamenizidi nguvu.

Unitoe humu kifungoni,*
nipate kulisifu jina lako

kati ya jamii ya waadilifu;*
kwasababu wewe umenitendea mema.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Tazameni, Bwana atakuja pamoja na wateule wake. Siku hiyo utatokea mwanga mkubwa, aleluya.

ANT. III: Bwana atakuja na uwezo mkuu, na watu wote watamwona.

WIMBO: Filp.2:6-11 Kristo, mtumishi wa Mungu
Yesu, kwa asili,*
alikuwa daima Mungu;

lakini hakufikiri kwamba/
kule kuwa sawa na Mungu*
ni kitu cha kung'ang'ania kwa nguvu.

Bali, kwa hiari yake mwenyewe,*
aliachilia hayo yote,

akajitwalia hali ya mtumishi/
akawa sawa na wanadamu,*
akaonekana kama wanadamu.

Alijinyenyekeza na kutii mpaka kufa,*
hata kufa msalabani.

Kwa sababu hiyo*
Mungu alimkweza juu kabisa,

akampa jina lililo kuu zaidi*
kuliko majina yote.

Ili kwa heshima ya jina la Yesu,/
viumbe vyote mbinguni, duniani na kuzimu,*
vipige magoti mbele yake;

Na kila mtu akiri/
Kwamba Yesu Kristo ni Bwana,*
kwa utukufu wa Mungu Baba.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Bwana atakuja na uwezo mkuu, na watu wote watamwona.

SOMO: 1Tes.5:23-24
Mungu anayetupatia amani awafanye ninyi watakatifu kwa kila namna na kuzilinda nafsi zenu - roho, mioyo na miili yenu - mbali na hatia yo yote wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye anayewaita ninyi atafanya hivyo kwani ni mwaminifu.

KIITIKIZANO
K. Utuoneshe, Ee Bwana, fadhili zako za milele. (W. Warudie)
K. Na utujalie wokovu wako.
W. Na fadhili zako za milele.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Utuoneshe...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Tazameni, jina la Bwana laja kutoka mbali. Utukufu wake waujaza ulimwengu wote.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Tazameni, jina la Bwana laja kutoka mbali. Utukufu wake waujaza ulimwengu wote.

MAOMBI
Mwana wa Mungu anakuja kwa uwezo mkuu: Binadamu wote watauona uso wake, na watazaliwa upya.
W. Njoo, Bwana Yesu; usikawie!

Utatuletea hekima, ufahamu mpya na mang'amuzi. (W.)

Utatuletea habari njema, na nguvu itakayobadili maisha yetu. (W.)

Utatuletea ukweli, ukituonesha njia ya kwenda kwa Baba yetu. (W.)

Wewe uliyezaliwa na mama, utatujalia, katika ubinadamu wetu, tuweze kuingia kwenye uzima na furaha ya milele. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Utujalie, Baba Mwenyezi, hapo Kristo atakapokuja tena, tuweze kwenda kumlaki, huku tumechukua mavuno ya kazi tulizofanikiwa kwa msaada wa neema zako. Tunaomba Kristo atupokee katika jumuiya ya watakatifu, na atukaribishe katika ufalme wa mbinguni. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.