Generic placeholder image

JUMAPILI 1 MAJILIO
MASIFU YA JIONI II

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Muumba wa nyota za usiku,
Mwanga wa milele wa taifa,
Mkombozi wetu sisi sote,
Utusikie tukuitapo.

Kwa mwili wa Maria 'likuja,
Tuokoke dhambi na aibu,
Kwa neema yako Mkombozi
Sasa njoo tuponye wadhambi.

Na siku ya hukumu ya mwisho,
Sisi tutakapofufuliwa,
Fika Mkombozi mwenye baraka,
Tupeleke rahani milele.
Irvin Udulutsch OSB

ANT. I: Furahi, Ee Binti Sion; piga kelele kwa sauti ya shangwe, Ee binti Yerusalemu, aleluya.

Zab.110:1-5,7 Kutawazwa kwa mfalme mteule
Maana Kristo sharti atawale mpaka Mungu atakapowashinda adui zake na kuwaweka chini ya miguu yake (Kor.15:25)

Mungu amemwambia bwana wangu,*
"Keti upande wangu wa kulia,

Mpaka niwafanye maadui zako,*
kama kibao cha kuegemea miguu yako."

Toka Sion Mungu ataeneza enzi yako.*
Asema: "Tawala juu ya adui zako!"

Watu wako watajitolea,*
siku utakapopambana na adui.

Vijana wako watakujia kwenye milima mitakatifu,*
kama vile umande wa asubuhi.

Mungu ameapa, wala hataghairi:/
"Kwamba wewe ni kuhani milele,*
kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki."

Mungu yuko upande wako wa kulia;*
atakapokasirika, atawaponda wafalme.

Njiani mfalme atakunywa maji ya kijito;*
kwa hiyo atainua kichwa juu kwa ushindi.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Furahi, Ee Binti Sion; piga kelele kwa sauti ya shangwe, Ee binti Yerusalemu, aleluya.

ANT. II: Kristo Mfalme wetu atakuja. Yeye ndiye Mwana-Kondoo, ambaye ujio wake ulitangazwa na Yohane.

Zab.114:1-8 Mungu pamoja na watu wake
Nanyi mliouacha ulimwengu huu, tambueni kuwa mmeokolewa kutoka Misri (Mt. Augustino)

Watu wa Israeli walipoondoka nchini Misri,*
wazao wa Yakobo walipotoka ugenini,

Yuda likawa taifa takatifu la Mungu,*
Israeli ikawa mali yake mwenyewe.

Bahari ya Shamu iliona ikakimbia;*
mto Yordani ukaacha kutiririka!

Milima ilirukaruka kama kondoo dume,*
vilima vikaruka kama wana-kondoo!

Ee bahari, imekuwaje hata ukakimbia?*
Nawe Yordani, kwa nini ukaacha kutiririka?

Enyi milima, mbona mliruka kama kondoo dume?*
Nanyi vilima, imekuwaje mkaruka kama wanakondoo?

Tetemeka, ewe dunia, mbele yake Mungu;*
Naam, mbele ya Mungu wa Yakobo,

anayeugusa mwamba ukawa bwawa la maji,*
nayo majabali yakawa chemchemi za maji.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Kristo Mfalme wetu atakuja. Yeye ndiye Mwana-Kondoo, ambaye ujio wake ulitangazwa na Yohane.

ANT. III: Tazameni, naja upesi kumlipa kila mmoja kadiri ya matendo yake, asema Bwana

WIMBO: Ufu.19:1,2,5-7 Arusi ya Mwana-kondoo

Aleluya.
Wokovu, utukufu na nguvu ni mali yake Mungu wetu!*
(W. Aleluya)
Maana hukumu yake ni ya kweli na ya haki.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Msifuni Mungu enyi watumishi wake wote,*
(W. Aleluya)
Nanyi nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Bwana, Mungu wetu Mwenyezi , ni Mfalme!*
(W. Aleluya)
Tufurahi na kushangilia; tumtukuze.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Wakati wa arusi ya Mwana-kondoo umefika,*
(W. Aleluya)
Na bibi arusi yuko tayari.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Atukuzwe Baba na Mwana, na Roho Mtakatifu,*
(W. Aleluya)
Kama mwanzo na sasa na siku zote, na milele. Amina.*
W. Aleluya (aleluya).

Ant. III: Tazameni, naja upesi kumlipa kila mmoja kadiri ya matendo yake, asema Bwana

SOMO: Filp.4:4-5
Basi, furahini daima katika kuungana na Bwana! Nasema tena: furahini! Mwe wapole kwa watu wote, Bwana yu karibu.

KIITIKIZANO
K. Utuoneshe, Ee Bwana, fadhili zako. (W. Warudie)
K. Na utujalie wokovu wako.
W. Na fadhili zako.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Utuoneshe...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Usiogope, Maria, maana Mungu amekupa upendeleo. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mwana, aleluya.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana.
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Usiogope, Maria, maana Mungu amekupa upendeleo. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mwana, aleluya.

MAOMBI
Tunamwomba Bwana wetu, ambaye ni Njia, Ukweli na Uzima.
W. Njoo, ukae nasi, Bwana.

Malaika Gabrieli alimjulisha Bikira Maria ujio wako:
- Mwana wa Aliye Juu, njoo, uutwae utawala wako. (W.)

Yohane Mbatizaji alifurahia kuiona siku yako:
- njoo, utuletee wokovu wako. (W.)

Mzee Simeoni alikukiri wewe, Nuru ya Ulimwengu:
- uwajalie mwanga wako watu wote wenye nia njema. (W.)

Tunakutazamia wewe kama walinzi wa usiku waingojeavyo asubuhi:
- wewe ndio jua litakalowaamsha marehemu, na kuwapatia uzima mpya. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Utujalie, Baba Mwenyezi, hapo Kristo atakapokuja tena, tuweze kwenda kumlaki, huku tumechukua mavuno ya kazi tulizofanikiwa kwa msaada wa neema zako. Tunaomba Kristo atupokee katika jumuiya ya watakatifu, na atukaribishe katika ufalme wa mbinguni. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.