JUMAPILI 1 MAJILIO
SALA ZA MCHANA
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
E Bwana Mbarikiwa,
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.
Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.
Ee fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;
Na yote yanafanyika
Kadiri unavyotaka.
Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu
Milele inayodumu
Kabla ya Adhuhuri
ANT.: Manabii walitabiri kwamba Mwokozi atazaliwa na bikira.
Adhuhuri
ANT.: Malaika Gabrieli alimwambia Maria, 'Furahi, wewe uliyependelewa
sana! Bwana yu pamoja nawe. Umebarikiwa kuliko wanawake wote.'
Baada ya Adhuhuri
ANT.: Maria alihangaishwa sana na amkio hilo, akajiuliza: 'Salamu hii
ina maana gani?' Akawaza: 'Nitamzaa Mfalme bila kupoteza ubikira!'
Zab.118 Sala ya shukrani
Huyu ndiye lile jiwe mlilokataa ninyi waashi, ambalo sasa limekuwa jiwe kuu la msingi
(Rej. Mate. 4:11)
Zab.118 Sala ya shukrani
Huyu ndiye lile jiwe mlilokataa ninyi waashi, ambalo sasa limekuwa jiwe kuu la msingi
(mate.4:11)
I
Mshukuruni Mungu, kwa kuwa ni mwema,*
kwa maana upendo wake mkuu ni wa milele.
Watu wa Israeli waseme:*
"Upendo wake mkuu ni wa milele."
Wazao wa Aroni waseme:*
"Upendo wake mkuu ni wa milele."
Wote wamchao Mungu waseme:*
"Upendo wake mkuu ni wa milele."
Katika taabu yangu nilimlilia Mungu,*
naye akanisikiliza na kuniokoa.
Mungu yuko nami, siogopi kitu;*
mwanadamu atanifanya nini?
Mungu yuko nami, ananisaidia;*
nami nitashuhudia kushindwa kwa adui zangu.
Ni afadhali kumtumainia Mungu,*
kuliko kumtegemea mwanadamu.
Ni afadhali kumtumainia Mungu,*
kuliko kuwategemea viongozi wa dunia.
Watu wote wasiomjua Mungu walinizingira,*
lakini kwa nguvu ya Mungu nikawapondaponda.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
II
Walinizunguka kila upande,*
lakini kwa nguvu ya Mungu nikawapondaponda.
Walinivamia kwa wingi kama nyuki,/
lakini wakateketea kama kichaka motoni;*
kwangu nguvu ya Mungu nikawapondaponda.
Nilishambuliwa mno karibu nishindwe,*
lakini Mungu alinisaidia.
Mungu hunijalia nguvu na uhodari;*
yeye mwenyewe ameniokoa.
Sikilizeni sauti za furaha na ushindi/
katika mahema ya watu waadilifu;*
"Mkono wa Mungu umetenda mambo ya ajabu!
Mkono wa Mungu umeleta ushindi!*
Mkono wa Mungu umetenda mambo ya ajabu!"
Sitakufa, bali nitaishi,*
na kutangaza matendo ya Mungu.
Mungu ameniadhibu sana,*
lakini hakuniacha nife.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
III
Nifungulie milango ya Hekalu;*
nitaingia na kumshukuru Mungu!
Huu ndio mlango wa Mungu,*
ambao waadilifu waweza kupitia.
Nakushukuru, Ee Mungu, kwa kunisikiliza;*
kwa sababu wewe umeniokoa.
Jiwe walilolikataa waashi,*
limekuwa jiwe kuu la msingi.
Jambo hili limefanywa na Mungu;*
nalo ni jambo la ajabu mno kwetu.
Hii ndiyo siku aliyoifanya Mungu;*
basi, tushangilie na kufurahi.
Utuokoe, Ee Mungu, utuokoe!*
Ee Mungu, tunakusihi, utupe fanaka!
Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Mungu!*
Twakubariki toka nyumbani mwa Mungu.
Mungu ni Mungu, naye ni mwema kwetu./
Shikeni matawi mikononi, anzeni sherehe,*
mkiandamana mpaka madhabahuni.
Ndiwe, Mungu wangu, ninakushukuru*
ninakutukuza, Ee Mungu wangu.
Mshukuruni Mungu kwa kuwa ni mwema,*
kwa maana upendo wake mkuu ni wa milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Kabla ya Adhuhuri
ANT.: Manabii walitabiri kwamba Mwokozi atazaliwa na bikira.
Adhuhuri
ANT.: Malaika Gabrieli alimwambia Maria, 'Furahi, wewe uliyependelewa
sana! Bwana yu pamoja nawe. Umebarikiwa kuliko wanawake wote.'
Baada ya Adhuhuri
ANT.: Maria alihangaishwa sana na amkio hilo, akajiuliza: 'Salamu hii
ina maana gani?' Akawaza: 'Nitamzaa Mfalme bila kupoteza ubikira!'
MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: Rom.13:13-14a
Mwenendo wetu uwe wa adabu kama inavyostahili wakati wa mwanga; tusiwe na ulafi na ulevi,
uchafu na uasherati, ugomvi na wivu. Bwana Yesu Kristo awe vazi lenu.
K. Mataifa yatalicha jina lako, Bwana.
W. Na wafalme wote wa dunia watatukuza utukufu wako.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Adhuhuri: 1Tes.3:12-13
Bwana awawezeshe ninyi kupendana na kuwapenda watu wote zaidi na zaidi, kama vile sisi tunavyowapenda
ninyi. Hivyo ataiimarisha mioyo yenu nanyi mtakuwa wakamilifu na watakatifu mbele ya Mungu na Baba yetu
wakati Bwana wetu Yesu atakapokuja pamoja na wote walio wake.
K. Utukumbuke, Ee Bwana, kwa upendo wako ulio nao kwa watu wako.
W. Njoo utuokoe.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Baada ya Adhuhuri: 2Tes.1:6,7,10
Kwa kuwa ni haki, Mungu atawalipa mateso wale wawatesao ninyi, na kuwalipa ninyi mteswao
leo pamoja na sisi, wakati wa kufunuliwa kwake Bwana Yesu kutoka mbinguni pamoja na malaika
wa uweza wake, siku hiyo atakapokuja ili kutukuzwa katika watakatifu wake na kustaajabiwa
katika wote waliomsadiki.
K. Njoo, Ee Bwana, usikawie.
W. Uwafungue watu wako kutoka katika dhambi zao.
SALA:
Tuombe: Utujalie, Baba Mwenyezi, hapo Kristo atakapokuja tena, tuweze kwenda kumlaki, huku
tumechukua mavuno ya kazi tulizofanikiwa kwa msaada wa neema zako. Tunaomba Kristo atupokee
katika jumuiya ya watakatifu, na atukaribishe katika ufalme wa mbinguni. Tunaomba hayo kwa
njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.