DOMINIKA YA 1 MAJILIO

MASOMO MWAKA C

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.25:1-3
Nakuinulia nafsi yangu, Ee Mungu wangu, nimekutumaini Wewe, nisiaibike. Adui zangu wasifurahi kwa kunishinda. Naam, wakungojao hawataaibika hata mmoja.

KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi, twakuomba, uwajalie waamini wako ari ya kumlaki kwa matendo ya haki Kristo wako anayekuja, ili, akiisha kuwaweka kuumeni kwake, wapate kuumiliki ufalme wa mbinguni. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Yer.33:14-16
Tazama, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapolitimiza neno lile jema nililolinena, katika habari za nyumba ya Israeli, na katika habari za nyumba ya Yuda. Katika siku zile, na wakati ule, nitamchipushia Daudi Chipukizi la haki; naye Atafanya hukumu na haki katika nchi hii. Katika siku zile Yuda ataokolewa, na Yerusalemu utakaa salama; na jina lake atakaloitwa ni hili, Bwana ni haki yetu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.25:4-5,8-9,10,14. (K)1
1. Ee Bwana, unijulishe njia zako,
Unifundishe mapito yako,
Uniongoze katika kweli yako,
Na kunifundisha.

(K) Ee Bwana, nakuinulia nafsi yangu.

2. Bwana yu mwema, mwenye adili,
Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
Wenye upole atawaongoza katika hukumu,
Wenye upole atawafundisha njia yake. (K)

3. Njia zote za Bwana ni fadhili na kweli,
Kwao walishikao agano lake na shuhuda zake.
Siri ya Bwana iko kwao wamchao.
Naye atawajulisha agano lake. (K)

SOMO 2: 1The.3:12-13:4:1-2
Ndugu zangu: Bwana na awaongeze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi na kwa watu wote, kama vile sisi nasi tulivyo kwenu; apate kuifanya imara mioyo yenu iwe bila lawama katika utakatifu mbele za Mungu, Baba yetu, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu pamoja na watakatifu wake wote. Iliyobaki, ndugu, tunakusihini na kuwaonya kwamba mwenende katika Bwana Yesu; kama mlivyopokea kwetu jinsi iwapasavyo kuenenda na kumpendeza Mungu, kama nanyi mnavyoenenda, vivyo hivyo mpate kuzidi sana. Kwa kuwa mnajua ni maagizo gani tuliyowapa kwa Bwana Yesu.

SHANGILIO: Zab.85:7
Aleluya, aleluya!
Ee Bwana utuoneshe rehema zako, Utupe na wokovu wako,
Aleluya!

SOMO 3: INJILI: Lk.21:25-28,34-36
Siku ile kutakuwa ishara katika jua; na mwezi, na nyota; na katika nchi dhiki ya mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake; watu wakivunjika mioyo kwa hofu, na kwa kutazama mambo yatakayoupata ulimwengu. Kwa kuwa nguvu za mbinguni zitatikisika. Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu mwingi. Basi, mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia. Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo; kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima. Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika hayo yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Ndugu zangu, Bwana wetu Yesu Kristo anatutisha kidogo kwa kutuambia kwamba mambo ya dunia hii yatapita na kwamba Mungu ataumba dunia mpya ambapo wateule wataishi katika heri ya milele. Ee Mungu Mwenyezi,

1. Utusaidie kuepuka mitego ya dunia hii inayotaka kutunasa na kutusahaulisha mambo ya mbinguni.

2. Utufumbue macho tuone mitego iliyo katika maisha yetu ya kila siku kama vile, kuwanyima wenye shida misaada inayotakiwa, rushwa na kutaka kutajirika kwa udanganyifu.

3. Utukumbushe kwamba matendo yetu mema yatatupatia tuzo ya heri ya huko mbinguni.

4. Uwasaidie wakubwa wa dini kutoa mfano wa imani unaowavutia waumini wote.

5. Uwasamehe marehemu wetu udhaifu wao na kuwapokea katika uzima wa heri.

Ee Baba mwema, haya ndiyo tunayothubutu kuyatamka kwako. Pamoja na haya, tunaomba utujalie pia yale tuliyoshindwa kutamka. Kwa jina la Kristo, Bwana wetu.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana tunakuomba, uvipokee vipaji tunavyokutolea, ambavyo tumevipokea kutoka kwa mema yako. Na yale unayotujalia kuyatenda kwa ibada katika wakati huu, yawe kwetu tuzo ya ukombozi wako wa milele. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

1. UTANGULIZI WA MAJILIO:
MAJILIO I:

K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.

K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele, kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Yeye, katika ujio wake wa kwanza, alipokuja katika unyenyekevu wa mwili, aliutimiza mpango ulioandaliwa nawe tangu kale. Hivyo, akatufungulia njia ya wokovu wa milele, ili, atakapokuja tena katika utukufu wa enzi yake, hatimaye tupewe waziwazi mema yaliyoahidiwa, ambayo kwa sasa tunathubutu kuyatarajia, tukikesha.
Kwa sababu hiyo, sisi pamoja na Malaika na Malaika Wakuu, pamoja na Viti vya enzi na Milki, na majeshi yote ya Malaika wa mbinguni, twaimba utenzi wa utukufu wako, tukisema bila mwisho:

W. Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,
Bwana Mungu wa majeshi.
Mbingu na dunia zimejaa utukufu wako.
Hosana juu mbinguni.
Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.
Hosana juu mbinguni.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.85:12
Bwana atatoa kilicho chema, na nchi yetu itatoa mazao yake.

SALA BAADA YA KOMUNYO
Ee Bwana tunakuomba, yatufae sisi mafumbo tuliyoyaadhimisha, ambayo tangu sasa, wakati tunapoenenda kati ya mambo yapitayo, tunaandaliwa kwayo kuyapenda mambo ya mbinguni na kuambatana na yale yadumuyo. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.