JUMAPILI YA 20 YA MWAKA B
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.84:9-10
Ee Mungu, ngao yetu, uangalie, umtazame uso Masiya wako. Hakika siku moja katika nyua zako ni bora kuliko siku elfu.

KOLEKTA:
Ee Mungu, umewaandalia wakupendao mema yasiyoonekana. Uwashe mioyoni mwetu moto wa upendo wako, ili, kwa kukupenda wewe katika yote na kuliko yote, tuzifikie ahadi zako zinazopita hamu zote. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Mit.9:1-6
Hekima ameijenga nyumba yake, amezichonga nguzo zake saba; Amechinja nyama zake, amechanganya divai yake, ameiandalia meza yake pia. Amewatuma wajakazi wake, analia, Mahali pa mjini palipoinuka sana, Kila aliye mjinga na aingie humu, Tena amwambia mtu aliyepungukiwa na akili, Njoo ule mkate wangu, Ukanywe divai niliyoichanganya. Enyi wajinga, acheni ujinga, mkaishi, Mkaende katika njia ya ufahamu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.34:1-2,9-14(K)8
1. Nitamhimidi Bwana kila wakati,
Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
wanyenyekevu wasikie wakafurahi.

(K) Onjeni muone ya kuwa Bwana yu mwema.

2. Mcheni Bwana, enyi watakatifu wake,
Yaani, wamchao hawahitaji kitu.
Wana-simba hutindikiwa, huona njaa;
Bali wamtafutao Bwana hawatahitaji kitu
Chochote kilicho chema. (K)

3. Njoni, enyi wana, mnisikilize,
nami nitawafundisha kumcha Bwana.
Ni nani mtu yule apendezwaye na uzima,
apendaye siku nyingi apate kuona mema? (K)

4. Uuzuie ulimi wako na mabaya,
Na midomo yako na kusema hila.
Uache mabaya ukatende mema,
Utafute amani ukaifuatie. (K)

SOMO 2: Efe.5:15-20
Angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima, bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu. Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana. Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho; mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu; na kumshukuru Mungu Baba siku zote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo.

SHANGILIO: Yn.14:6
Aleluya, aleluya!
mimi ndimi Njia, na Ukweli, na Uzima, asema Bwana; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya!

INJILI: Yn.6:51-59
Yesu aliwaambia makutano: Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Basi Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule? Basi yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele, nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi. Hiki ndicho chakula kishukacho kutoka mbinguni; si kama mababa walivyokula, wakafa; bali akilaye chakula hicho ataishi milele. Maneno hayo aliyasema katika sinagogi, alipokuwa akifundisha, huko Kapernaumu.

Nasadiki husemwa.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, uvipokee vipaji vyetu vinavyotufanya tushirikiane nawe katika muungano huu mtukufu, ili tunapokutolea vile ulivyotupatia, tustahili kukupokea wewe mwenyewe. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.130:7
Kwa Bwana kuna fadhili, na kwake kuna ukombozi mwingi.

Au:
Yn.6:51-52

Bwana asema: Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, kwa njia ya sakramenti hii tumefanywa washiriki wa Kristo. Tunakuomba kwa unyenyekevu huruma yako, ili, kwa kufanana naye hapa duniani, tustahili kuwa washiriki pamoja naye pia kule mbinguni. Anayeishi na kutawala milele na milele.