DOMINIKA YA 22 YA MWAKA B
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.86:3,5
Wewe, Bwana, unifadhili, maana nakulilia wewe mchana kutwa. Kwa maana wewe, Bwana, u mwema,
umekuwa tayari kusamehe, na mwingi wa fadhili kwa watu wote wakuitao.
UTUKUFU husemwa.
KOLEKTA:
Ee Mungu wa majeshi, ambaye kila kilicho bora ni chako, ututilie mioyoni mwetu upendo wa jina lako.
Pia, kwa kutuongezea uchaji, uyasitawishe ndani yetu yale yaliyo mema, na uyahifadhi kwa ulinzi wako
imara yale uliyoyasitawisha. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe
katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Kum.4:1-2,6-8
Na sasa, Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mzitende; mpate kuishi
na kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zenu. Msiliongeze neno niwaamurulo
wala msilipunguze, mpate kuzishika amri za Bwana, Mungu wenu, niwaamuruzo. Zishikeni basi,
mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia amri
hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili. Kwa maana liko
taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama Bwana, Mungu wetu, alivyo, kila
tumwitapo? Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii
yote, ninayoiweka mbele yenu leo.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.15:1-5(K)1
1. Bwana, ni nani atakayefanya maskani yake
Katika kilima chako kitakatifu?
Ni mtu aendaye kwa ukamilifu,
Na kutenda haki;
Asemaye kweli kwa moyo wake.
(K) Bwana, ni nani atakayekaa katika hema yako?
2. Ni yeye ambaye hakumtenda mwenziwe mabaya,
Wala hakumsengenya jirani yake.
Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa,
Bali huwaheshimu wamchao Bwana. (K)
3. Ni yeye ambaye hayabadili maneno yake,
Ingawa ameapa kwa hasara yake.
Ambaye hakutoa fedha yake apate kula riba,
Wala hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia.
Mtu atendaye mambo hayo hataondoshwa milele. (K)
SOMO 2: Yak.1:17-18,21-22,27
Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba
wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeukageuka. Kwa kupenda kwake mwenyewe
alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake. Kwa hiyo wekeeni mbali
uchafu wote na ubaya uzidio, na kupokea kwa upole neno lile lililopandwa ndani, liwezalo
kuziokoa roho zenu. Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya
nafsi zenu. Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii. Kwenda kuwatazama yatima
na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa.
SHANGILIO: Yn.6:63,68
Aleluya, aleluya!
Bwana, maneno yako ni roho, tena ni uzima, Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya!
INJILI: Mk.7:1-8,14-15,21-23
Mafarisayo, na baadhi ya waandishi waliotoka Yerusalemu, wakakusanyika mbele ya Yesu wakaona
wengine katika wanafunzi wake wakila vyakula kwa mikono najisi, yaani, isiyonawiwa. Kwa maana
Mafarisayo na Wayahudi wote wasiponawa mikono mpaka kiwiko, hawali, wakishika mapokeo ya wazee
wao; tena wakitoka sokoni, wasipotawadha, hawali; na yako mambo mengine waliyopokea huyashika,
kama kuosha vikombe, na midumu, na vyombo vya shaba. Basi wale Mafarisayo na waandishi
wakamwuliza, Mbona wanafunzi wako hawaendi kwa kuyafuata mapokeo ya wazee, bali hula chakula
kwa mikono najisi? Akawaambia, Isaya alitabiri vema juu yenu ninyi wanafiki, kama ilivyoandikwa,
Watu hawa huniheshimu kwa midomo Ila mioyo yao iko mbali nami; Nao waniabudu bure, Wakifundisha
mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu. Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya
wanadamu. Akawaita makutano tena, akawaambia, Nisikieni nyote na kufahamu. Hakuna kitu kilicho
nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo
unajisi yule mtu. Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, ukorofi, hila, ufisadi,
kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu
unajisi.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Wayahudi wa kale walifikiri kwamba kushika desturi zao za
zamani ni dini inayowaletea wokovu. Kumbe Yesu alileta dini
mpya na kuleta kanuni kuu ambayo ni upendo.
Ee Mungu Baba,
1. Utufungue macho ili imani yetu isafishe mambo yaliyo
katika utamaduni wetu ambayo yanayopingana na amri
zako.
2. Utusaidie kujali habari njema ya wokovu uliyotuletea, zaidi
ya mapokeo na desturi za zamani.
3. Miiko ilibuniwa na binadamu: Utusaidie kujali uhuru wa
imani zaidi kuliko utumwa wa miiko ya zamani.
4. Kwako kuna mwiko mmoja tu yaani, dhambi, Usafishe
mioyo yetu na tamaa mbaya na maelekeo yasiyofaa.
Ee Mungu wa upendo, ulituwekea amri ya mapendo kuwa amri
kuu. Uyapokee maombi yetu kwa jina la Kristo, Bwana wetu.
Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, sadaka takatifu tunayokutolea ituletee daima baraka na wokovu, ili jambo linalotendwa kwa
fumbo, likamilishwe ndani yetu kwa nguvu ya sadaka hii. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.31:19
Ee Bwana, jinsi zilivyo nyingi fadhili zako ulizowawekea wakuchao.
Au:
Mt.5:9-10
Heri wapatanishi; maana hao wataitwa wana wa Mungu. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki;
maana ufalme wa mbinguni ni wao.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, sisi tuliolishwa mkate wa meza ya mbinguni, tunakuomba sana, ili chakula hicho cha
mapendo kitutie nguvu moyoni, hata tuhamasishwe kuwatumikia jirani zetu kwa ajili yako. Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu.