DOMINIKA YA 23 YA MWAKA B
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.119:137,124
Ee Bwana, wewe ndiwe mwenye haki, na hukumu zako ni za adili. Kama zilivyo rehema zako umtendee mtumishi wako.

UTUKUFU husemwa.

KOLEKTA:
Ee Mungu, umetuletea ukombozi na kutufanya watoto wako. Utusikilize kwa wema sisi watoto wa upendo wako. Tunakuomba ili wote wanaomwamini Kristo wapewe uhuru wa kweli na urithi wa milele. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Isa.35:4-7a
Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi. Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa. Ndipo mtu aliye kilema ataruka-ruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba; maana katika nyika maji yatabubujika; na vijito jangwani. Na mchanga ung'aao mfano wa maji utakuwa ziwa la maji, na nchi yenye kiu itakuwa chemchemi za maji;

WIMBO WA KATIKATI: Zab.146:7-10(K)1
1. Bwana ndiye ashikaye kweli milele,
Huwafanyia hukumu walioonewa,
Huwapa wenye njaa chakula;
Bwana hufungua waliofungwa;

(K) Ee nafsi yangu, umsifu Bwana.

2. Bwana huwafumbua macho waliopofuka;
Bwana huwainua walioinama;
Bwana huwapenda wenye haki;
Bwana huwahifadhi wageni; (K)

3. Huwategemeza yatima na mjane;
Bali njia ya wasio haki huipotosha.
Bwana atamiliki milele, Mungu wako,
Ee Sayuni, kizazi hata kizazi. (K)

SOMO 2: Yak.2:1-5
Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu. Maana akiingia katika sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu na mavazi mazuri; kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu; nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, Keti wewe hapa mahali pazuri; na kumwambia yule maskini, Simama wewe pale, au keti miguuni pangu, je! Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu? Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, Je! Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao?

SHANGILIO: Yn.8:12
Aleluya, aleluya!
Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema Bwana; Yeye anifuataye atakuwa na nuru ya uzima.
Aleluya!

INJILI: Mk.7:31-37
Yesu alitoka katika mipaka ya Tiro, akapita katikati ya Sidoni, akaenda mpaka bahari ya Galilaya, kati ya mipaka ya Dekapoli. Wakamletea kiziwi, naye ni mwenye utasi, wakamsihi amwekee mikono. Akamtenga na mkutano faraghani, akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema mate, akamgusa ulimi, akatazama juu mbinguni, akaugua, akamwambia, Efatha, maana yake, Funguka. Mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea, akasema vizuri. Akawaonya wasimwambie mtu; lakini kadiri ya alivyozidi kuwaagiza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari; wakashangaa mno kupita kiasi, wakinena, Ametenda mambo yote vema; viziwi awafanya wasikie, na bubu waseme.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Umati wa watu walishangilia hotuba na mafundisho ya Yesu kwa maneno haya: Ametenda yote vema, amewafanya viziwi wasikie na bubu waseme.

Ee Mungu Baba,
1. Tunawaombea wote wanaojiita wakristo ili wasikilize maneno yako na kuyatangaza kwa moyo wa matumaini.

2. Tunaomba kwa ajili ya dunia ili mataifa yote yasikilize habari njema ya Enjili, na kutafuta njia ya usalama na amani.

3. Utufungue midomo yetu tuimbe sifa zako kwa moyo mnyofu.

4. Baada ya kufunguliwa mdomo na masikio katika ubatizo: Utusaidie tusikia mafundisho yako na kuimba sifa zako.

Ee Baba wa huruma, tunakupelekea maombi yetu kwa njia ya Yesu Kristo, Bwana wetu. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Mungu, uliye asili ya ibada ya kweli na ya amani, tunakuomba utujalie ili kwa vipaji hivi tuitukuze inavyotakiwa adhama yako, na kwa njia ya kushiriki fumbo hili takatifu tuunganike kiaminifu katika nia moja. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.42:1-2
Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji, vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku, ee Mungu. Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai.

Au:
Yn.8:12

Bwana asema: Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, umewalisha waamini wako na kuwatia uzima kwenye meza ya neno lako na ya sakramenti ya mbinguni. Uwajalie, ili kwa vipaji hivyo bora vya Mwanao mpendwa, wastahili kushirikishwa daima uzima wake. Anayeishi na kutawala milele na milele.