DOMINIKA YA 24 YA MWAKA B
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Ybs.36.15-16
Ee Bwana, uwape amani wakungojao, ili watu wawasadiki manabii wako; uisikilize sala yao wakuombao,
na ya taifa lako Isareli
UTUKUFU husemwa.
KOLEKTA:
Utuangalie, ee Mungu muumba na mtawala wa vitu vyote. Utujalie tuweze kukutumikia kwa moyo
wote, ili tufurahie matunda ya upatanisho wako. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi
na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Isa.50:5-9
Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma. Naliwatolea wapigao
mgongo wangu, na wang’oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa
mate. Maana Bwana Mungu atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso
wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya. Yeye anipatiaye haki yangu yu karibu; ni
nani atakayeshindana nami? Na tusimame pamoja; ni nani aliye hasimu yangu? Na anikaribie basi.
Tazama, Bwana Mungu atanisaidia; ni nani atakayenihukumu kuwa mkosa?
WIMBO WA KATIKATI: Zab.116:1-6,8-9(K)9
1. Aleluya,
Nampenda Bwana kwa kuwa ananisikiliza
Sauti yangu na dua zangu.
Kwa maana amenitegea sikio lake,
Kwa hiyo nitamwita siku zangu zote!
(K) Nitaenenda mbele za Bwana, katika nchi ya walio hai.
2. Kamba za mauti zilinizunguka,
Shida za kuzimu zilinipata.
Niliona taabu na huzuni,
Nikaliitia jina la Bwana;
Ee Bwana, Mungu wangu, uniokoe. (K)
3. Bwana ni mwenye neema na haki,
Naam, Mungu wetu ni mwenye rehema,
Bwana huwalinda wasio na hila,
Nilikuwa taabuni, akaniokoa. (K)
4. Maana ameniponya nafsi yangu na mauti,
Macho yangu na machozi,
Na miguu yangu na kuanguka.
Nitaenenda mbele za Bwana
Katika nchi za walio hai. (K)
SOMO 2: Yak.2:14-18
Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! Ile imani
yaweza kumwokoa? Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki, na
mtu wa kwenu akawaambia, Enendeni zenu kwa amani, mkaote moteo na kushiba, lakini asiwape
mahitaji ya mwili, yafaa nini? Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini
mwake. Lakini mtu atasema, Wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nioneshe imani yako pasipo
matendo, nami nitakuonesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu.
SHANGILIO: Mdo.16:14
Aleluya, aleluya!
Fungua mioyo yetu, Ee Bwana, ili tuyatunze maneno ya Mwanao.
Aleluya!
INJILI: Mk.8:27-35
Yesu alitoka na wanafunzi wake, wakaenda kwenye vijiji vya Kaisaria Filipi; na njiani akawauliza
wanafunzi wake, akasema, Watu huninena mimi kuwa ni nani? Wakamjibu, Yohana Mbatizaji; wengine,
Eliya; wengine, Mmojawapo wa manabii. Naye akawauliza, Na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani?
Petro akamjibu, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo. Akawaonya wasimwambie mtu habari zake. Akaanza
kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee,
na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka. Naye alikuwa
akinena neno hilo waziwazi. Petro akamchukua, akaanza kumkemea. Akageuka, akawatazama wanafunzi
wake, akamkemea Petro, akasema, Nenda nyuma yangu; Shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu,
bali ya wanadamu. Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, Mtu yeyote akitaka
kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponywa
nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya
Injili, huyu ataisalimisha.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Bwana Yesu aliweka masharti makali ya kumfuata. Kumbe sisi
sote wakati wa ubatizo tuliona ni rahisi kufuata njia ya Yesu
aliyetufungulia njia ya kwenda kwa Mungu Baba.
Ee Bwana Mungu,
1. Petro alitambua kwa mwangaza wa Roho Mtakatifu
kwamba Yesu ni Masia: Utuangaze akili zetu ili
kumtambua Yesu zaidi na zaidi katika maisha ya kila siku.
2. Tunawaombea viongozi wa Kanisa ili wawatayarishe
makatekista kwa kuwapa mafunzo imara na vitendea kazi
kwa ajili ya utume wao.
3. Tunawaombea viongozi wa serikali na wakuu wa shule ili
watoe nafasi ya mafundisho ya dini katika shule zote za
serikali.
4. Kushika dini ni zaidi kuliko kujua kanuni za imani kwa
moyo: Utusaidie kutimiza kanuni ya imani yetu kwa
matendo katika maisha yetu ya kawaida ya kila siku.
5. Mtu akipata dunia yote kuwa mali yake, anaweza kupoteza
roho yake: Utupe moyo wa kuacha yote yanayotuzuia
kukufuata.
Ee Mungu Mwenyezi, Mwana wako alikwenda njia ya mateso ili
kufikia utukufu wa mbinguni. Utusaidie kumfuata na usikilize
maombi yetu kwa jina la Kristo Bwana wetu. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, uwe radhi kuyasikiliza maombi yetu, na upokee kwa wema vipaji hivi wanavyokutolea
watumishi wako, ili kile alichokutolea kila mmoja wetu kwa heshima ya jina lako, kifae kwa wokovu wa
wote. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.36:7
Ee Mungu, jinsi zilivyo na thamani fadhili zako! Wanadamu huukimbilia uvuli wa mbawa zako.
Au:
1Kor.10:16
Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je, si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si
ushirika wa mwili wa Bwana?
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, nguvu ya kipawa cha mbinguni tulichokipokea itujaze mwili na roho, ili tusitawaliwe
na tamaa zetu, ila tu na nguvu hiyo. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.