DOMINIKA YA 25 YA MWAKA B
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA:
Bwana asema: Mimi ndimi wokovu wa watu. Katika shida yoyote wataniita, nami nitawasikiliza;
nami nitakuwa Bwana wao hata milele.
UTUKUFU husemwa.
KOLEKTA:
Ee Mungu, uliyaweka maagizo yote ya sheria takatifu katika upendo kwako na kwa jirani. Utujalie
kuzishika amri zako, tupate kustahili kuufikia uzima wa milele. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Hek.2:12:17-20
Zaidi ya hayo tumwotee mtu wa haki, maana hatuna haja naye, naye yu kinyume cha matendo yetu,
atukaripia ya kama tumeiasi torati, na kutushitaki ya kama tumekosa adabu. Haya na tuone kama
maneno yake ni kweli; tufanye kujaribu yatakayompata wakati wa mwisho wake; mradi mwenye haki
akiwa ni mwana wa Mungu, Yeye atamtegemeza na kumwokoa mikononi mwa adui zake. Na tumhakikishe
kwa jeuri na maumivu, ili tujifunze upole wake na kuithibitisha saburi yake akidhulumiwa. Hata
tumhukumu auawe mauti ya aibu, maana ataangaliwa sawasawa na maneno yake.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.54:1-4,6(K)4
1. Ee Mungu, kwa jina lako uniokoe,
Na kwa uwezo wako unifanyie hukumu.
Ee Mungu uyasikie maombi yangu,
Uyasikilize maneno ya kinywa changu.
(K) Bwana ndiye anayeitegemeza nafsi yangu.
2. Kwa maana wageni wamenishambulia,
Wote watishao wanaitafuta nafsi yangu;
Hawakumweka Mungu mbele yao. (K)
3. Tazama, Mungu anayenisaidia;
Bwana ndiye anayeitegemeza nafsi yangu.
Kwa ukunjufu wa moyo nitakutolea dhabihu,
Ee Bwana, nitalishukuru jina lako, maana ni jema. (K)
SOMO 2: Yak.3:16-4:3
Hapo palipo wivu na ugomvi, ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya. Lakini hekima itokayo
juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema
na matunda mema, haina fitina, haina unafiki, na tunda la haki hupandwa katika amani na wale
wafanyao amani. Vita vyatoka wapi, na mapigano yaliyoko kati yetu yatoka wapi? Si humu, katika
tamaa zenu zifanyazo vita katika viungo vyenu? Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu,
wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi! Hata mwaomba,
wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.
SHANGILIO: Mdo.16:14
Aleluya, aleluya!
Fungua mioyo yetu, Ee Bwana, ili tuyatunze maneno ya Mwanao.
Aleluya!
INJILI: Mk.9:30-37
Wakatoka huko, wakapita katikati ya Galilaya; naye hakutaka mtu kujua. Kwa sababu alikuwa
akiwafundisha wanafunzi wake, akawaambia, Mwana wa Adamu yuaenda kutiwa katika mikono ya watu,
nao watamwua; hata akiisha kuuawa, baada ya siku tatu atafufuka. Lakini hawakulifahamu neno
lile, wakaogopa kumwuliza. Wakafika Kapernaumu; hata alipokuwamo nyumbani, akawauliza,
Mlishindania nini njiani? Wakanyamaza; kwa maana njia walikuwa wakibishana wao kwa wao,
ni nani aliye mkubwa. Akaketi chini, akawaita wale Thenashara akawaambia, Mtu atakaye kuwa
wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote. Akatwaa kitoto, akamweka katikati
yao, akamkumbatia, akawaambia, Mtu akimpokea mtoto mmoja wa namna hii kwa jina langu, anipokea
mimi, na mtu akinipokea mimi, humpokea, si mimi, bali yeye aliyenituma.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Hapa duniani kila mtu anatafuta kuwa mkubwa kuliko mwenzake,
kuwa na fedha nyingi zaidi, kuwa na nyumba kubwa zaidi na
kadhalika. Kwake Yesu, kutafuta ukubwa ni kinyume na sheria
yake, ambaye alikuwa mtumishi wa wote. Tumuombe Baba
Mungu.
Ee Bwana Mungu,
1. Uwafanye viongozi wa Kanisa na serikali kutumia
mamlaka na madaraka yao katika kuinua hali ya maisha ya
wanyonge.
2. Utuongoze tusitafute ukubwa au utajiri ili kuwadharau
wengine.
3. Sisi tunashawishiwa kuwaheshimu "wakubwa" na
kuwadharau wadogo: Utusaidie kuelewa kwamba ufuasi
wako haufuati desturi za duniani.
4. Wewe ulikuwa mtumishi wetu kwa kutukomboa kwa kutoa
maisha yako: Utupe neema ya kufuata mfano wako wa
utumishi kwa kuwatumikia wale tunaoishi nao.
Ee Mungu Mwenyezi, uliweka taratibu ya Ufalme wa Mungu
ambayo ni kinyume na taratibu ya duniani. Ukubwa upande wako
ni kuwatumikia wengine. Utusaidie kuelewa hayo na kuyatimiza
na usikilize maombi yetu, kwa Kristo Bwana wetu. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, uwe radhi kuvipokea vipaji vya taifa lako, ili hayo wanayoungama kwa imani na uchaji
wayapate kwa njia ya sakramenti za mbinguni. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.119:4-5
Wewe umetuamuru mausia yako, ili sisi tuyatii sana. Ningependa njia zangu ziwe thabiti, nizitii amri
zako.
Au:
Yn.10:14
Bwana asema: Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua
mimi.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, sisi unaotulisha kwa sakramenti zako uwe radhi kutuinua kwa njia ya misaada yako ya
siku zote, ili tuyapokee matunda ya ukombozi katika mafumbo na katika mwenendo wetu. Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu.