DOMINIKA YA 26 YA MWAKA B
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Dan.3:31,29,30,43,42
Ee Bwana, yote uliyotutendea, umeyatenda kwa haki, kwa kuwa sisi tumetenda dhambi, wala hatukuzitii amri zako. Ulitukuze jina lako na kututendea sawasawa na wingi wa huruma zako.

UTUKUFU husemwa.

KOLEKTA:
Ee Mungu, unayedhihirisha uweza wako hasa kwa kusamehe na kuhurumia. Utuongezee neema yako, ili, kwa kuzikimbilia ahadi zako, tushirikishwe mema ya mbinguni. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Hes.11:25-29
Bwana alishuka ndani ya wingu, akanena naye, akatwaa sehemu ya roho iliyokuwa juu ya Musa, akaitia juu ya wale wazee sabini; ikawa, roho hiyo ilipowashukia, wakatabiri, lakini hawakufanya hivyo tena. Lakini watu wawili walisalia kambini, jina la mmoja aliitwa Eldadi, na jina la wa pili aliitwa Medadi; na roho ile ikawashukia; nao walikuwa miongoni mwao walioandikwa, lakini walikuwa hawakutoka kwenda Hemani; nao wakatabiri kambini. Mtu mmoja kijana akapiga mbio, akaenda akamwambia Musa, akasema, Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini. Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa tangu ujana wake, akajibu akasema, Ee Bwana wangu Musa, uwakataze. Musa akamwambia, Je! Umekuwa na wivu kwa ajili yangu; ingekuwa heri kama watu wote wa Bwana wangekuwa manabii, na kama Bwana angewatia roho yake.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.19:7,9,11-13(K)8
1. Sharia ya Bwana ni kamilifu,
Huiburudisha nafsi.
Ushuhuda wa Bwana ni amini,
Humtia mjinga hekima.

(K) Maagizo ya Bwana ni ya adili, huufurahisha moyo.

2. Kicho cha Bwana ni kitakatifu,
Kinadumu milele.
Hukumu za Bwana ni kweli,
Zina haki kabisa. (K)

3. Tena mtumishi wako huonywa kwazo,
Katika kuzishika kuna thawabu nyingi.
Ni nani awezaye kuyatambua makossa yake?
Unitakase na mambo ya siri. (K)

4. Umzuie mtumishi wako asitende mambo ya kiburi,
Yasinitawale mimi.
Ndipo nitakapokuwa kamili,
Nami nitakuwa safi, bila kosa lililo kubwa. (K)

SOMO 2: Yak.5:1-6
Haya basi, enyi matajiri! Lieni, mkapige yowe kwa sababu ya mashaka yenu yanayowajia. Mali zenu zimeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto. Mmejiwekea akiba katika siku za mwisho. Angalieni, ujira wa wakulima waliovuna mashamba yenu, ninyi mliouzuia kwa hila, unapiga kelele, na vilio vyao waliovuna vimeingia masikioni mwa Bwana wa majeshi. Mmefanya anasa katika dunia, na kujifurahisha kwa tamaa; mmejilisha mioyo yenu kama siku ya machinjo. Mmehukumu mwenye haki mkamwua; wala hashindani nanyi.

SHANGILIO: Yn.10:27
Aleluya, aleluya!
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, asema Bwana; Nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya!

INJILI: Mk.9:38-43,45,47-48
Yohane alimwambia Yesu, Mwalimu tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye hafuatani nasi; tukamkataza, kwa sababu hafuatani nasi. Yesu akasema, Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya mwujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya; kwa sababu asiye kinyume chetu, yu upande wetu. Kwa kuwa yeyote atakayewanywesha ninyi kikombe cha maji, kwa kuwa ninyi ni watu wa Kristo, amin, nawaambia, hatakosa thawabu yake. Na yeyote atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, afadhali afungiwe jiwe la kusagia shingoni mwake, na kutupwa baharini. Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanamu, kwenye moto usiozimika. Na mguu wako ukikukosesha, ukate, ni afadhali kuingia katika uzima, u kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili, na kutupwa katika jehanamu. Na jicho lako likikukosesha, ling’oe, ulitupe, ni afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu, una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanamu; ambao humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Bwana Yesu anatuonya tusiwakwaze wengine kwa mifano yetu mibaya au kwa mwenendo wetu usiofaa.

Ee Mungu Baba,
1. Sisi waumini tuna wajibu wa kuwatunza wengine wasipotee: utupe neema ya kuwajenga wengine badala ya kuwaharibu kwa mifano yetu mibaya.

2. Utupe mwanga wa kutambua hatari zote zinazopingana na imani yetu na kuziacha.

3. Utupe moyo wa kujinasua na yote yanayotushawishi kukuasi wewe.

4. Utusaidie tuangalie tusiwakwaze wengine kwa mienendo yetu mibaya.

5. Uwakaribishe ndugu zetu, marafiki na wafadhili marehemu katika ufalme wako wa milele.

Ee Mungu Mwenyezi, hutaki kiumbe kimoja kipotee wala kupotoshwa. Sisi pengine tunaharibu mambo kwa makusudi au pengine bila kujua. Uyasikilize maombi yetu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Mungu mwenye huruma, ukubali dhabihu yetu hii ikupendeze, nayo itufungulie chemchemi ya baraka zote. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.119:49-50
Ee Bwana, likumbuke neno ulilomwambia mtumishi wako, kwa sababu umenitumainisha. Hii ndiyo faraja yangu katika taabu yangu.

Au
1Yn.3:16

Katika hili tumelifahamu pendo la Mungu, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, sakramenti hii ya mbinguni itufanye wapya rohoni na mwilini, ili tuwe warithi pamoja naye katika utukufu wake yeye, ambaye tunayashiriki mateso yake tukiitangaza mauti yake. Anayeishi na kutawala milele na milele.