Generic placeholder image

JUMAPILI JUMA LA 27 LA MWAKA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Njooni, tumwimbie Bwana; tumfanyie shangwe Mungu anayetuokoa, Aleluya.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI tazama pia AU
Mungu usiye mipaka
Ndanimo Wewe twaishi,
Ee ufufuo na Mwanga,
Utenzi wa asubuhi
Wewe tunakuimbia,
Unyamavu wa usiku
Sasa tunaumaliza.

Jogoo yule wa kwanza
Anapoanza kuwika,
Na vyote viamkapo
Kutoka usingizini,
Ndipo huchipua upya
Uzima na tumaini,
Na rangi huonekana.

Mwumba wa vyote vilivyo,
Kipimo cha vitu vyote
Na mwisho wa vyote hivyo,
Ee Mungu msamehevu
Sahau makosa yetu,
Na sikia zetu sala
Kabla hatujakwomba.

Sifa iwe kwako Baba,
Mwana, Roho Mtakatifu,
Ee Utatu Mtakatifu,
Chemchemi ya neema,
Unayetuita sisi
'Toka utovu wa vyote
Tuje kwako tutulie.

AU

Kristo ni Mwokozi wa dunia,
Awapendaye walio safi,
Kisima cha hekima ya mbingu,
Thibitisho la imani yetu
Hifadhi ya tumaini letu,
Silaha za askari wake,
Bwana wa dunia na mbingu,
Afya yetu tunapoishi,
Uzima wetu tunapokufa.

Chini katika kiza kinene,
Alilala kafungwa mfungwa,
Ilipowadia yake saa,
Alifufuka taji kavaa.
Na sasa, mbinguni kisha paa,
Kiti cha enzi amekalia,
Ambacho kamwe hakukiacha;
Hicho ni mali ya Baba yake,
Hicho ni mali yake mwenyewe.

Utukufu wote kwake Baba,
Ambaye peke Hakuzaliwa;
Heshima yote iwe kwa Yesu,
Pekee aliye Mwana wake;
Pia kwa Roho Mtakatifu;
Utatu ulo Mkamilifu.
Vitu vyote haya na vijibu,
Haya jibuni binadamu:
Amin - iwe hivyo - Amina.

ANT. I: Bwana aliye juu, ndiye mwenye ukuu.

Zab.93 Mungu mfalme
Bwana, Mungu wetu Mwenyezi, ni Mfalme! Tufurahi. na kushangilia; tumtukuze (Ufu.19:6-7)

Mungu anatawala, amejivika fahari!/
Mungu amevaa fahari na nguvu!*
Ameuimarisha ulimwengu, hautatikisika kamwe.

Kiti cha enzi ni imara tangu awali;*
wewe umekuwapo kabla ya kuwako nyakati.

Ee Mungu, vilima vyapaaza sauti zao;*
naam, vyapaaza sauti na mvumo wao.

Mungu ana enzi kuu juu mbinguni,/
ana nguvu kuliko mlio wa bahari,*
ana nguvu kuliko mawimbi ya maji.

Ee Mungu, maagizo yako ni thabiti;*.
nyumba yako ni takatifu milele na milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Bwana aliye juu, ndiye mwenye ukuu.

ANT. II: Usifiwe, Bwana, na utukuzwe milele, aleluya.

WIMBO: Dan.3:37-88,56 Kila kiumbe kimsifu Bwana
Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote (Ufu.19:5)

Enyi viumbe vyote vya Bwana, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Malaika za Bwana, mhimidini Bwana;*
Enyi mbingu, mhimidini Bwana.

Maji yote yaliyo juu angani, mhimidini Bwana;*
Mawezo yote ya Bwana, mhimidini Bwana.

Jua na mwezi, mhimidini Bwana;*
Nyota za mbinguni, mhimidini Bwana.

Manyunyu yote na ukungu, mhimidini Bwana;*
Pepo zote, mhimidini Bwana.

Moto na hari, mhimidini Bwana;*
Kipupwe na musimu, mhimidini Bwana.

Umande na sakitu, mhimidini Bwana;*
Jalidi na baridi, mhimidini Bwana.

Barafu na theluji, mhimidini Bwana;*
Usiku na mchana, mhimidini Bwana.

Dunia na imhimidi Bwana;*
Imsifu na kumwadhimisha milele.

Milima na vilima, mhimidini Bwana;*
Mimea yote ya nchi, mhimidini Bwana.

Chemchemi, mhimidini Bwana;*
Bahari na mito, mhimidini Bwana.

Nyangumi na vyote viendavyo majini, mhimidini Bwana;*
Ndege zote za angani, mhimidini Bwana.

Hayawani na wanyama wafugwao, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Wanadamu, mhimidini Bwana;*
Bani Israeli, mhimidini Bwana.

Makuhani wa Bwana, mhimidini Bwana;*
Watumishi wa Bwana, mhimidini Bwana.

Roho na nafsi zao wenye haki, mhimidini Bwana;*
Watakatifu na wanyenyekevu moyoni, mhimidini Bwana.

Enyi Anania, Azaria, na Misaeli, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Tumtukuze Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Umehimidiwa katika anga la mbinguni,*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Ant. II: Usifiwe, Bwana, na utukuzwe milele, aleluya.

ANT. III: Enyi mlio mbinguni, msifuni Bwana, aleluya.

Zab.148 Ulimwengu wote umsifu Mungu
Kwake yeye aketiye katika kiti cha enzi, na kwa Mwana-kondoo, iwe sifa na heshima na utukufu na enzi milele (Ufu.5:13)

Msifuni Mungu kutoka mbinguni,*
msifuni enyi mnaoishi huko juu.

Msifuni enyi malaika wake wote,*
msifuni enyi jeshi lote la mbinguni.

Msifuni enyi jua na mwezi,*
msifuni enyi nyota zote zing'aazo.

Msifuni enyi mbingu za juu,*
na maji yaliyo juu ya mbingu.

Lazima kulisifu jina la Mungu,*
maana yeye aliamuru, na vyote vikawa.

Yeye aliviweka mahali pao daima;*
amri yake yadumu milele.

Msifuni Mungu kutoka duniani;*
vilindi vya bahari na majoka yake, msifuni.

Msifuni enyi moto, mvua ya mawe na theluji,*
upepo wa tufani unaotimiza amri yake.

Msifuni enyi milima na vilima,*
miti ya matunda na misitu!

Msifuni enyi wanyama wa porini na wafugwao,*
wanyama watambaao na ndege wote!

Msifuni enyi wafalme wote na mataifa*
viongozi na watawala wote duniani!

Msifuni enyi wavulana na wasichana;*
wazee wote pamoja na watoto pia!

Nyote lisifuni jina la Mungu,/
maana jina lake peke yake latukuka;*
utukufu wake wapita dunia na mbingu.

Taifa la Israeli liko karibu naye;/
yeye amelikuza na kulipatia nguvu,*
hivyo watu wake wote waaminifu wanamsifu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Enyi mlio mbinguni, msifuni Bwana, alelulya.

SOMO: Eze.37:12b-14
Tazama, nitafunua makaburi yenu, na kuwapandisha kutoka katika makaburi yenu, enyi watu wangu, nami nitawaingizeni katika nchi ya Israeli. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapoyafunua makaburi yenu, na kuwatoa ninyi katika makaburi yenu enyi watu wangu. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi, nami nitawawekeni katika nchi yenu, nanyi mtajua ya kuwa mimi, BWANA, nimesema hayo, na kuyatimiza, asema BWANA.

KIITIKIZANO
K. Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai utuhurumie. (W. Warudie)
K. Umeketi mkono wa kuume wa Baba.
W. Utuhurumie
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Wewe...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Waacheni watoto wadogo waje kwangu; kwa sababu utawala wa mbinguni ni kwa ajili ya watu walio kama watoto hawa.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Waacheni watoto wadogo waje kwangu; kwa sababu utawala wa mbinguni ni kwa ajili ya watu walio kama watoto hawa.

MAOMBI
Tumwombe Baba, aliyemleta Roho Mtakatifu aangaze mioyo ya watu wote.
W. Bwana, tuletee mwanga wa Roho wako.

Ewe Mtukufu, asili ya mwanga:
- ulimwengu wote unakusifu. (W.)

Kwa ufufuko wa Mwanao, dunia imejazwa mwanga wako:
- mwanga huo uliangaze Kanisa, kwa njia ya karama ya Roho wako(W.)

Kwa nguvu ya Roho wako Mtakatifu, wafuasi waliyakumbuka yote waliyofundishwa na Yesu:
- ulishushie Kanisa Roho huyo, ili liwe aminifu kwako. (W.)

Mwanga wa Mataifa yote, uwatazame wale wanaoishi katika giza:
- ifungue mioyo yao, ili wakupokee wewe uliye Mungu wa kweli. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu Mwenyezi wa milele, ambaye kwa upendo wako unatupatia mema mengi zaidi kuliko yale tunayoomba na kustahili, utufungulie hazina za huruma yako. Utusamehe makosa yetu yote yanayotukera katika dhamiri, na utuongezee hata yale tusiyothubutu kuomba. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe pamoja na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.