Generic placeholder image

JUMAPILI JUMA LA 27 LA MWAKA
MASIFU YA JIONI I

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Ewe mwangavu Mwanga wa Mungu
Utukufu wake yeye Baba,
Kwako wewe, Ee Kristo,
Kwako Bwana ndio tunaimba;
Pamoja na nyota ya jioni,
Wakati jua linapotua,
Sala zetu tunakutolea.

Wastahili sifa milele
Usifiwe Baba nawe Mwana,
Pia wewe Roho wake Mungu,
Uliye Mtakatifu sana.
Na ulimwengu wakutukuza
Unakushukuru, Ee Kristo
Uliyetoa uzima wako.

ANT. I: Toka maawio ya jua hata machweo yake, jina la Bwana lisifiwe.

Zab.113 Sifa kwa Mungu mtukufu
Amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao. vya enzi, akawakweza wanyenyekevu (Lk.1:52)

Enyi watumishi wa Mungu,*
lisifuni jina lake!

Jina lake litukuzwe,*
sasa na hata milele.

Kutoka mashariki hata magharibi,*
litukuzwe jina la Mungu!

Mungu atawala mataifa yote,*
utukufu wake wazipita mbingu.

Hakuna aliye sawa na Mungu, Mungu wetu,*
ambaye anakaa juu kabisa;

lakini huinama chini*
kuzitazama mbingu na nchi.

Humwinua fukara kutoka mavumbini;*
humnyanyua maskini kutoka unyonge wake,

na kumweka pamoja na wakuu;*
naam, pamoja na wakuu wa watu wake.

Humrudishia hadhi mwanamke aliye tasa;*
na kumfurahisha kwa kumjalia watoto.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Toka maawio ya jua hata machweo yake, jina la Bwana lisifiwe.

ANT. II: Nitapokea kikombe cha wokovu, na kulitangaza jina la Bwana.

Zab.116:10-19 Shukrani kwa kuokolewa kifoni
Kwa njia ya Yesu, tumtolee Mungu sadaka ya sifa daima (Ebr.13:15)

Nampenda Mungu, kwa maana anisikia,*
maana amesikiliza kilio cha ombi langu.

Yeye hunisikiliza*
kila ninapomlilia.

Hatari ya kifo ilinizunguka,/
vitisho vya kaburi vilinivamia;*
nilijawa mahangaiko na majonzi.

Kisha nikamlilia Mungu:*
"Ee Mungu, tafadhali unisalimishe!”

Mungu amejaa wema na haki;*
Mungu wetu ni mwenye huruma.

Mungu huwalinda wanyofu*
nilikuwa nimekandamizwa, naye akaniokoa.

Uwe na utulivu mkuu, ee roho yangu,*
kwa maana Mungu amenitendea vyema.

Ameniokoa kifoni na kufuta machozi yangu;*
akanilinda nisije nikaanguka.

Basi, nitatembea mbele yake Mungu,*
katika nchi ya watu walio hai.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Nitapokea kikombe cha wokovu, na kulitangaza jina la Bwana.

ANT. III: Bwana Yesu alijinyenyekeza; kwa hiyo, Mungu akamtukuza milele.

WIMBO: Filp.2:6-11 Kristo, mtumishi wa Mungu
Kristo Yesu, kwa asili,*
alikuwa daima Mungu;

lakini hakufikiri kwamba/
kule kuwa sawa na Mungu*
ni kitu cha kung'ang'ania kwa nguvu.

Bali, kwa hiari yake mwenyewe,*
aliachilia hayo yote,

akajitwalia hali ya mtumishi/
akawa sawa na wanadamu,*
akaonekana kama wanadamu.

Alijinyenyekeza na kutii mpaka kufa,*
hata kufa msalabani.

Kwa sababu hiyo*
Mungu alimkweza juu kabisa,

akampa jina lililo kuu zaidi*
kuliko majina yote.

Ili kwa heshima ya jina la Yesu,/
viumbe vyote mbinguni, duniani na kuzimu,*
vipige magoti mbele yake;

Na kila mtu akiri/
Kwamba Yesu Kristo ni Bwana,*
kwa utukufu wa Mungu Baba.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Bwana Yesu alijinyenyekeza; kwa hiyo Mungu akamtukuza milele.

SOMO: Ebr.13:20-21
Mungu amemfufua Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye ni Mchungaji Mkuu wa kondoo kwa sababu ya kumwaga damu yake iliyothibitisha Agano la milele. Mungu wa amani awakamilishe katika kila tendo jema, ili mtekeleze mapenzi yake; yeye na afanye ndani yetu, kwa njia ya Kristo, yale yanayompendeza mwenyewe. Utukufu uwe kwake, milele na milele! Amina.

KIITIKIZANO
K. Jinsi yalivyo makuu matendo yako, Ee Bwana! (W. Warudie)
K. Yote umeyafanya kwa hekima.
W. Matendo yako, Ee Bwana!
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Jinsi...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Atawaangamiza kabisa hao waovu, na hilo shamba la mizabibu atawapangisha wakulima wengine, ambao watampa mavuno wakati wa mavuno.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Atawaangamiza kabisa hao waovu, na hilo shamba la mizabibu atawapangisha wakulima wengine, ambao watampa mavuno wakati wa mavuno.

MAOMBI
Kristo Bwana wetu anawashughulikia wote wanaomhitaji, na hutenda makuu kwa sababu anawapenda. Kwa hiyo, tusiogope kumwomba katika mahitaji yetu yote.
W. Utuoneshe mapendo yako.

Bwana, tunafahamu kwamba mema tuliyopokea leo yametoka kwako:
- utujalie tuyapokee kwa shukrani, na tujifunze kuyatoa kwa wenye dhiki. (W.)

Mwokozi na nuru ya watu wote, uwatunze kwa namna ya pekee wale uliowatuma kueneza neno lako:
- moto wa Roho wako uwake kwa nguvu ndani yao. (W.)

Uijalie dunia ipate kuujua ukweli wako;
- utusaidie kutekeleza yote uliyotuagiza kufanya. (W.)

Uliponya magonjwa na kuondoa maumivu ya ndugu zako:
- ponya roho zetu, na uzifariji. (W.)

Uwajalie pumziko waamini marehemu;
- na uwafikishe kwako, wakusifu milele. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu Mwenyezi wa milele, ambaye kwa upendo wako unatupatia mema mengi zaidi kuliko yale tunayoomba na kustahili, utufungulie hazina za huruma yako. Utusamehe makosa yetu yote yanayotukera katika dhamiri, na utuongezee hata yale tusiyothubutu kuomba. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe pamoja na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.