Generic placeholder image

JUMAPILI JUMA LA 27 LA MWAKA
MASIFU YA JIONI II

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI tazama pia AU
Mwanzoni Mungu aliumba mbingu,
Pia dunia tupu yenye giza;
Kilindini Rohoye ilivuma
Pumzi ikafanyiza mawimbi.

Kisha Mungu aliumba Mwanga,
Kuja kwa huo kulifuta giza,
Pakawa asubuhi na jioni:
Mwisho wa siku ya kwanza ya Mungu.

Atukuzwe Baba wa ulimwengu,
Na Kristo Mwana wa pekee,
Wao na Roho vyote watawala:
Utatu katika Mungu Mmoja.

AU

Sifa kwa Mtakatifu kabisa
Aliye juu na katika kina,
Asemayo mastaajabivu,
Katika yote mkweli kabisa.

Hekima pendevu ya Mungu wetu!
Ingawa dhambi na fedheha pote,
Kaja vitani Adamu wa pili,
Ili kutuoko alikuja.

Ee upendo wa busara yote!
Mwili na damu katika Adamu
Dhidi ya adui vilivyoshindwa,
Na vijitahidi hadi ushindi.

Karama bora kuliko neema,
Mwili na damu vinadhihirisha,
Uwepo hasa wa Mungu mwenyewe,
Na yake dhati, umungu mtupu.

Kwa upendo tele ukawa mtu,
Adui ya watu ukamshinda,
Mateso mawili ulikubali,
Ili binadamu anufaike.

Mosi, kwa faragha bustanini,
Wa aidha juu msalabani;
Ni funzo na himizo kwa nduguzo,
Tupende kuteswa na kufa pia.

Sifa kwa Mtakatifu kabisa,
Aliye juu na katika kina,
Asemayo mastaajabivu,
Katika yote mkweli kabisa.

ANT. I: Bwana alimwambia Bwana wangu; 'Keti mkono wangu wa kuume', aleluya, aleluya.

Zab.110:1-5,7 Kutawazwa kwa mfalme mteule
Maana Kristo sharti atawale mpaka Mungu atakapowashinda adui zake na kuwaweka chini ya miguu yake (Kor.15:25)

Mungu amemwambia bwana wangu,*
"Keti upande wangu wa kulia,

Mpaka niwafanye maadui zako,*
kama kibao cha kuegemea miguu yako."

Toka Sion Mungu ataeneza enzi yako.*
Asema: "Tawala juu ya adui zako!"

Watu wako watajitolea,*
siku utakapopambana na adui.

Vijana wako watakujia kwenye milima mitakatifu,*
kama vile umande wa asubuhi.

Mungu ameapa, wala hataghairi:/
"Kwamba wewe ni kuhani milele,*
kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki."

Mungu yuko upande wako wa kulia;*
atakapokasirika, atawaponda wafalme.

Njiani mfalme atakunywa maji ya kijito;*
kwa hiyo atainua kichwa juu kwa ushindi.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Bwana alimwambia Bwana wangu; 'Keti mkono wangu wa kuume', aleluya, aleluya.

ANT. II: Bwana ni mwingi wa fadhili na rehema; hutufanya tukumbuke matendo yake ya ajabu, aleluya.

Zab.111 Mungu asifika kwa matendo yake
Bwana, Mungu Mwenyezi, matendo yako ni makuu mno (Ufu.15:3)

Nitamshukuru Mungu kwa moyo wangu wote,*
katika jumuiya ya watu.

Matendo ya Mungu ni ya ajabu mno!*
Wote wanaoyafurahia hutaka kuyaelewa.

Kila afanyacho kimejaa utukufu na fahari;*
na uadilifu wake wadumu milele.

Mungu hutukumbusha matendo yake ya ajabu;*
Mungu ni mwema na mwenye huruma.

Huwapa chakula wenye kumcha;*
hasahau kamwe agano lake.

Amewaonesha watu wake enzi yake,*
kwa kuwapatia nchi za mataifa mengine.

Matendo yake ni ya haki, na ya kuaminika;*
amri zake zote ni za kutegemewa daima.

Amri zake zadumu daima na milele;*
zimetolewa kwa ukweli na uadilifu.

Aliwakomboa watu wake,/
na kufanya nao agano la milele.*
Yeye ni mtakatifu na wa kutisha mno.

Kumcha Mungu ni msingi wa hekima;/
wote wanaozitii amri zake hujaliwa busara.*
Sifa zake zadumu milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana ni mwingi wa fadhili na rehema; hutufanya tukumbuke matendo yake ya ajabu, aleluya.

ANT. III: Bwana, Mungu Mwenyezi, ni Mfalme wetu, aleluya.

WIMBO: Ufu.19:1,2,5-7 Arusi ya Mwana-kondoo

Aleluya.
Wokovu, utukufu na nguvu ni mali yake Mungu wetu!*
(W. Aleluya)
Maana hukumu yake ni ya kweli na ya haki.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Msifuni Mungu enyi watumishi wake wote,*
(W. Aleluya)
Nanyi nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Bwana, Mungu wetu Mwenyezi , ni Mfalme!*
(W. Aleluya)
Tufurahi na kushangilia; tumtukuze.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Wakati wa arusi ya Mwana-kondoo umefika,*
(W. Aleluya)
Na bibi arusi yuko tayari.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Atukuzwe Baba na Mwana, na Roho Mtakatifu,*
(W. Aleluya)
Kama mwanzo na sasa na siku zote, na milele. Amina.*
W. Aleluya (aleluya).

Ant. III: Bwana, Mungu Mwenyezi, ni Mfalme wetu, aleluya.

SOMO: 1Pet.1:3-5
Asifiwe Mungu, Baba ya Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa huruma yake kuu alitufanya tuzaliwe upya kwa kumfufua Yesu kutoka wafu. Ametujalia tumaini lenye uzima, na hivyo tunatazamia kupata baraka zile ambazo Mungu aliwawekea watu wake. Mungu aliwawekeeni baraka hizo mbinguni ambako haziwezi kuoza, au kuharibika, au kufifia. Hizo zitakuwa zenu ninyi, ambao kwa imani mnalindwa salama kwa nguvu ya Mungu kwa ajili ya wokovu ambao uko tayari kufunuliwa mwisho wa nyakati.

KIITIKIZANO
K. Umehimidiwa, Ee Bwana, katika anga la mbinguni. (W. Warudie)
K. Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
W. Katika anga la mbinguni.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Umehimidiwa...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Jiambieni wenyewe, 'Sisi ni watumishi tusio na faida, tumefanya tu yale tuliyopaswa kufanya.'

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Jiambieni wenyewe, 'Sisi ni watumishi tusio na faida, tumefanya tu yale tuliyopaswa kufanya.'

MAOMBI
Mungu ndiye Mwumba. Mapendo yake hufanya upya vitu vyote, na ni chanzo cha matumaini yetu. Tumwelekee kwa imani na matumaini:
W. Bwana, zipokee shukrani na sala zetu.

Tunakushukuru kwa mpango uliouweka katika viumbe vyako:
- umetujalia uzima na maliasili. (W.)

Tunatoa shukrani kwa kutushirikisha katika kuiendeleza kazi yako ya kuumba:
- tunakusifu kwa vipaji vya uvumbuzi na usanifu ulivyotujalia. (W.)

Tunayaombea mataifa yote duniani:
- viongozi watafute amani na uelewano kati ya watu. (W.)

Tunawaombea wale wote ambao hawana makao;
- uwajalie makazi wakimbizi waliofukuzwa nchini kwao. (W.)

Umetujalia uhai, ambao ni zawadi yako ya kwanza kwetu:
- uwajalie marehemu wafikie utimilifu wa uzima huo ndani yako (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu Mwenyezi wa milele, ambaye kwa upendo wako unatupatia mema mengi zaidi kuliko yale tunayoomba na kustahili, utufungulie hazina za huruma yako. Utusamehe makosa yetu yote yanayotukera katika dhamiri, na utuongezee hata yale tusiyothubutu kuomba. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe pamoja na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.