DOMINIKA YA 27 YA MWAKA B
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Est.4:17b.17c
Ee Bwana, ulimwengu wote u katika uweza wako, wala hakuna awezaye kuyapinga mapenzi yako.
Wewe umeviumba mbingu na nchi, na vitu vyote vya ajabu vilivyopo chini ya mbingu; nawe ndiwe Bwana
wa vyote.
UTUKUFU husemwa.
KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi wa milele, kwa wingi wa huruma yako watenda mambo ya ajabu sana kuliko
yote tunayostahili na kuyatamani sisi tukuombao. Utushushie rehema yako, utuondolee yale yanayozitia
hofu dhamiri zetu, na kutuongezea yale ambayo hatuthubutu kuomba. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu
Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Mwa.2:18:24
Bwana Mungu alisema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanya msaidizi wa kufanana naye.
Bwana Mungu akafanyiza kutoka katika ardhi kila mnyama wa msituni, na kila ndege wa angani,
akamletea Adamu ili aone atawaitaje; kila kiumbe hai, jina alilokiita Adamu likawa ndilo jina
lake. Adamu akawapa majina yao kila mnyama wa kufugwa, na ndege wa angani, na kila mnyama wa
mwituni; lakini hakuonekana wa kumsaidia Adamu aliyefanana naye. Bwana Mungu akamletea Adamu
usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, na
ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu. Adamu akasema,
Sasa huyo ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke,
kwa maana ametwaliwa katika mwanamume. Kwa hiyo mwanamume, atamwacha baba yake na mama yake
naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.128(K)5
1. Heri kila mtu amchaye Bwana,
Aendaye katika njia yake.
Taabu ya mikono yako hakika utaila,
Utakuwa mwenye heri na baraka tele.
(K) Bwana atubariki siku zote za maisha yetu.
2. Mke wako atakuwa kama mzabibu uzaao,
Vyumbani mwa nyumba yako.
Wanao kama miche ya mizeituni,
Wakizunguka meza yako. (K)
3. Hakika, atabarikiwa hivyo,
Yule amchaye Bwana.
Bwana akubariki toka Sayuni,
Uone uheri wa Yerusalemu siku zote za maisha yako;
Naam, ukawaone wana wa wanao.
Amani ikae na Israeli. (K)
SOMO 2: Ebr.2:9-11
Ndugu, twamwona yeye aliyefanywa mdogo punde kuliko malaika, yaani, Yesu, kwa sababu ya maumivu
ya mauti, amevikwa taji ya utukufu na heshima, ili kwa neema ya Mungu aionje mauti kwa ajili ya
kila mtu. Kwa kuwa ilimpasa yeye, ambaye kwa ajili yake na kwa njia yake vitu vyote vimekuwapo,
akileta wana wengi waufikilie utukufu, kumkamilisha kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso.
Maana yeye atakasaye na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii haoni haya kuwaita
ndugu zake.
SHANGILIO: Yn.14:23
Aleluya, aleluya!
Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda;
nasi tutakuja kwake.
Aleluya!
INJILI: Mk.10:2-16
Mafarisayo walimwendea Yesu, wakamwuliza, Je, ni halali mtu kumwacha mkewe? Huku wakimjaribu.
Naye akajibu, akawaambia, Musa aliwaamuru nini? Wakasema, Musa alitoa ruhusa kuandika hati ya
talaka na kumwacha. Yesu akawaambia, Kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu aliwaandikia amri hii.
Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha
baba na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja, hata wamekuwa si wawili
tena, bali mwili mmoja. Basi alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe. Hata nyumbani
tena wanafunzi wakamwuliza habari ya neno hilo. Akawaambia, Kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa
mwingine azini juu yake; na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine azini. Basi wakamletea
watoto wadogo ili awaguse; wanafunzi wake wakawakemea. Ila Yesu alipoona alichukizwa sana, akawaambia,
Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao.
Amin, nawaambieni, Yeyote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa. Akawakumbatia,
akaweka mikono juu yao, akawabarikia.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Katika Enjili ya leo tumesikia: Aliyounganisha Mungu,
mwanadamu asithubutu kuyatenganisha. Kwa hiyo tuombe
udumifu kwa ndoa za kikristu.
Ee Baba Mungu,
1. Uimarishe familia zote zisivunjwe wala kuharibiwa na
mitindo ya maisha ya siku hizi ya kutodumu katika ndoa.
2. Uwape watu wa ndoa nguvu ya kuvumilia matatizo katika
familia zao na kujaribu kuyatatua kwa ushirikiano mwema.
3. Uwaongoze watu wa ndoa kushikamana kwa uaminifu na
amani na ulinde familia zetu ziwe kama bustani za
kusitawishia imani.
4. Waongoze vijana wetu kutambua thamani ya ndoa na
familia kama msingi wa jamii imara.
5. Utuoneshe njia za kuwasaidia wale ambao ndoa zao zipo
katika hatari ya kuvunjika.
6. Uwasaidie watoto wanaohangaika kutokana na kuvunjika kwa
ndoa za wazazi wao.
Ee Mungu Mwenyezi, toka mwanzo wa dunia uliweka ndoa kuwa
msingi wa maisha ya familia. Uziimarishe familia zetu na usikilize
maombi yetu tunayokupelekea kwa jina la Kristo Bwana wetu.
Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba tu upokee sadaka hii iliyowekwa kwa amri yako. Na, kwa haya mafumbo
matakatifu tunayoadhimisha kwa mujibu wa utumishi wetu wa kikuhani, uwe radhi kutimiza ndani
yetu kazi ya ukombozi wako unaotutakatifuza. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Omb.3:25
Bwana ni mwema kwa hao wamngojeao, kwa hiyo nafsi imtafutayo.
Au
1Kor 10:17
Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja: kwa maana sisi sote twashiriki mkate
mmoja na kikombe kimoja.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Mungu mwenyezi, utujalie sakramenti hii tuliyopokea ituchangamshe na kutulisha. tupate
kugeuka kuwa kile tunachokipokea. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.