DOMINIKA YA 28 YA MWAKA B
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.130:3-4
Bwana, kama wewe ungehesabu maovu, ee Bwana, nani angesimama? Lakini kwako kuna msamaha, ee Mungu wa Israeli.

UTUKUFU husemwa.

KOLEKTA:
Ee Bwana, tunakuomba neema yako itutangulie daima na kutusindikiza, nayo itubidiishe kutenda mema. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Hek.7:7-11
Naliomba, nikapewa ufahamu; nalimwita Mungu, nikajiliwa na roho ya Hekima. Naliichagua kuliko fimbo za enzi na viti vya enzi, wala mali sikuifananisha na kitu cha thamani; mradi dhahabu yote ya nchi ni kama mchanga kidogo. Naliipenda kupita afya njema na uzuri wa sura, hata Zaidi ya nuru nikataka kuwa nayo, kwa maana mwangaza wake haufifii kamwe. Na pamoja nayo nikajiliwa na mema yote jamii, na mikononi mwake mali isiyoweza kuhesabika.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.90:12-17(K)14
1. Utujulishe kuzihesabu siku zetu,
Tujipatie moyo wa hekima.
Ee, Bwana, urudi, hata lini?
Uwahurumie watumishi wako.

(K) Utushibishe kwa fadhili zako ili tufurahi.

2. Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako,
Nasi, tutashangilia kwa kadiri ya siku ulizotutesa,
Kama miaka ile tuliyoona mabaya. (K)

3. Matendo yako na yaonekane kwa watumishi wako,
Na adhama yako kwa watoto wao.
Na uzuri wa Bwana, Mungu wetu, uwe juu yetu,
Naam, kazi ya mikono yetu uithibitishe. (K)

SOMO 2: Ebr.4:12-13
Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu.

SHANGILIO: Mdo.16:14
Aleluya, aleluya!
Fungua mioyo yetu, ee Bwana, ili tuyatunze maneno ya Mwanao,
Aleluya!

INJILI: Mk.10:17-30
Yesu alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza, Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele? Yesu akamwambia, Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu. Wazijua amri, Usiue, Usizini, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako. Akamwambia, Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu. Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja, Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate. Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi. Yesu akatazama kotekote, akawaambia wanafunzi wake, Jinsi itakavyokuwa shida wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu! Wanafunzi wakashangaa kwa maneno yake. Yesu akajibu tena, akawaambia, Watoto, jinsi ilivyo shida wenye kutegemea mali kuingia katika ufalme wa Mungu! Ni rahisi ngamia kupenya katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. Nao wakashangaa mno, wakimwambia, Ni nani, basi, awezaye kuokoka? Yesu akawakazia macho akasema, Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yawezekana kwa Mungu. Petro akaanza kumwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata wewe. Yesu akasema, Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto na mashamba, pamoja, na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Tunashutushwa sana kwa neno la Yesu aliyesema: Ni rahisi kwa ngamia kupenya tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.

Ee Baba Mungu,
1. Ulinde mioyo yetu isinaswe katika tamaa za mali na kusahau hazina ya mbinguni. Ee Bwana.

2. Tunawaombea wakubwa wa serikali ili wahakikishe kuwa rasilimali za nchi yetu zinagawanywa sawa kati ya rata. Ee Bwana.

3. Utusaidie tusifanywe watumwa wa mali au fedha bali tutumie vitu hivi kwa ajili ya manufaa yetu na wenzetu. Ee Bwana.

4. Utuamshe kuzitumia mali zetu kuhudumia kazi za Kanisa. Ee Bwana.

5. Ufungue mioyo yetu tusimtenge mtu yeyote, bali tumshirikishe mahitaji ya lazima. Ee Bwana.

Ee Mungu Mwenyezi, kuna mambo mengi hapa duniani yanayotuzuia kwenda katika njia iendayo kwako. Utusaidie na uyapokee maombi yetu, kwa Kristo Bwana wetu. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, upokee sala pamoja na matoleo ya dhabihu ya waamini wako, ili, kwa matendo haya ya ibada, tupate kuufikia utukufu wa mbinguni. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.34:10
Matajiri hutindikiwa, huona njaa; bali wamtafutao Bwana hawatahitaji kitu chochote kilicho chema.

Au:
1Yn.3:2

Bwana atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana mtukufu, tunakuomba kwa unyenyekevu, utushirikishe umungu wako kama unavyotulisha Mwili na Damu takatifu ya Mwanao. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.