DOMINIKA YA 29 YA MWAKA B
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.17:6,8
Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika, utege sikio lako ulisikie neno langu. Ee Bwana, unilinde
kama mboni ya jicho, unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako.
UTUKUFU husemwa.
KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi wa milele, utuwezeshe daima kuyafuata mapenzi yako kwa uchaji na kuitumikia
fahari yako kwa moyo mnyofu. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala
nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Isa.53:10-11
Bwana aliridhika kumchubua; Amemhuzunisha; Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi,
Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi; Na mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake; Ataona
mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika. Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki atawafanya
wengi kuwa wenye haki; Naye atayachukua maovu yao.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.33:4-5,18-20,22(K)22
1. Neno la Bwana lina adili,
Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
Huzipenda haki na hukumu,
Nchi imejaa fadhili za Bwana.
(K) Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi, kama vile tulivyokungoja Wewe.
2. Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao,
Wazingojeao fadhili zake.
Yeye huwaponya nafsi zao na mauti,
Na kuwahuisha wakati wa njaa. (K)
3. Nafsi zetu ninamngoja Bwana,
Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.
Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi,
Kama vile tunavyokungoja Wewe. (K)
SOMO 2: Ebr.4:14-16
Iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungano
yetu. Kwa kuwa hatuna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye
alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha
neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.
SHANGILIO: Efe.1:17,18
Aleluya, aleluya!
Ewe Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Uyatie nuru macho ya mioyo yetu,
ili tujue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo.
Aleluya!
INJILI: Mk.10:35-45
Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, walimwendea, wakamwambia, Mwalimu, twataka utufanyie lolote
tutakalokuomba. Akawaambia, Mwataka niwafanyie nini? Wakamwambia, Utujalie sisi tuketi, mmoja mkono
wako wa kuume na mmoja mkono wako wa kushoto, katika utukufu wako. Yesu akawaambia, Hamjui mnaloliomba. Mwaweza kunywea kikombe
ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi? Wakamwambia, Twaweza. Yesu akawaambia, Kikombe
ninyweacho mimi mtakinywea, na ubatizo nibatizwao mimi mtabatizwa; lakini habari ya kuketi mkono wangu
wa kuume au mkono wangu wa kushoto si langu kuwapa, ila wao watapewa waliowekewa tayari. Hata wale
kumi waliposikia wakaanza kuwakasirikia Yakobo na Yohane. Yesu akawaita, akawaambia, Mwajua ya kuwa
wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini
haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka
kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote. Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali
kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Mitume wawili, Yoane na Yakobo walikuwa hawajatambua bado
kwamba ufalme wa Mungu si ufalme wa kidunia ambapo watu
hupewa vyeo mbalimbali vya utawala. Ufalme wa Mungu unaanza
katika mioyo ya waumini wanaofuata amri za Mungu ambazo ni
msingi wa maisha bora.
Ee Baba Mungu,
1. Utupe roho ya unyenyekevu na utuangaze tusipiganie vyeo
na heshima hapa duniani, bali tuitumie dunia kama
matayarisho ya kufika mbinguni.
2. Utuhimize kutenda matendo ya kueneza ufalme wa
mapendo, amani, ushirikiano na umoja hapa duniani.
3. Duniani tunaona kwamba wakubwa wanatumia mamlaka
ovyo kwa faida yao: Utusaidie kupinga mwenendo huu wa
ubinafsi na kueneza ufalme wa wema haki, na amani.
4. Utupe moyo wa kutumikia badala ya kutumikiwa.
Ee Mungu wa huruma, ulimtuma Mwana wako atutangazie ufalme
wako. Usikilize maombi yetu ka njia ya Yesu Kristo Bwana
wetu. Amina.
MAOMBI
Mitume wawili, Yoane na Yakobo walikuwa hawajatambua
bado kwamba ufalme wa Mungu si ufalme wa kidunia ambapo watu hupewa
vyeo mbalimbali vya utawala. Ufalme wa Mungu unaanza katika mioyo ya waumini
wanaofuata amri za Mungu ambazo ni msingi wa maisha bora.
Ee Baba Mungu,
1. Utupe roho ya unyenyekevu na utuangaze tusipiganie vyeo na heshima hapa
duniani, bali tuitumie dunia kama matayarisho
ya kufika mbinguni. Ee Bwana.
2. Utuhimize kutenda matendo ya kueneza ufalme wa mapendo, amani,
ushirikiano na umoja hapa duniani. Ee Bwana.
3. Duniani tunaona kwamba wakubwa wanatumia mamlaka ovyo kwa faida yao:
Utusaidie kupinga mwenendo huu wa ubinafsi na kueneza
ufalme wa wema haki, na amani. Ee Bwana.
4. Utupe moyo wa kutumikia badala ya kutumikiwa. Ee Bwana.
Ee Mungu wa huruma, ulimtuma Mwana wako
atutangazie ufalme wako. Usikilize maombi yetu kwa njia ya
Yesu Kristo Bwana wetu. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba utujalie tuweze kukutumikia kwa uhuru wa moyo kwa vipaji vyako. Ututakase
kwa neema yako, na utusafishe kwa mafumbo hayohayo tunayoyaadhimisha. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu
ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.33:18-19
Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao, wazingojeao fadhili zake. Yeye huwaponya nafsi zao
na mauti, na kuwahuisha wakati wa njaa.
Au:
Mk.10:45
Mwana wa Adamu amekuja apate kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, tunakuomba utujalie ili, kwa njia ya kushiriki mara nyingi mafumbo haya ya mbinguni,
tuweze kupata msaada wa riziki za duniani, na ufahamu wa mema ya milele. Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu.