JUMAPILI YA 2 KWARESIMA MWAKA C
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.17:8-9
Moyo wangu umekuambia: Bwana, uso wako nitautafuta. Usinifiche uso wako.
AU. Zab.25:6,2,22
Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako, maana zimekuwako tokea zamani. Adui zangu
wasifurahi kwa kunishinda; utukomboe, ee Mungu wa Israeli, katika taabu zetu zote.
KOLEKTA:
Ee Mungu, umetuamuru kumsikiliza Mwanao mpendwa. Uwe radhi kuilisha mioyo yetu kwa neno lako, ili,
kwa macho ya kiroho yaliyotakaswa, tufurahi kuuona utukufu wako. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu milele na mielele.
SOMO 1: Mwa.15:5-12,17-18
Mungu alimleta Abramu nje, akasema, Tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu.
Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. Akamwamini Bwana, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki.
Kisha akamwambia, Mimi ni Bwana, niliyekuleta kutoka Uru wa Wakaldayo nikupe nchi hii ili uirithi.
Akasema, Ee Bwana Mungu, nipateje kujua ya kwamba nitairithi? Akamwambia, Unipatie ndama wa miaka
mitatu, na mbuzi mke wa miaka mitatu, na kondoo mume wa miaka mitatu, na hua, na mwana njiwa. Akampatia
hao wote, akawapasua vipande viwili, akaweka kila kipande kuelekea mwenzake, ila ndege hakuwapasua. Hata
tai walipotua juu ya mizoga Abramu akawafukuza. Na jua lilipokuwa likichwa usingizi mzito ulimshika
Abramu, hofu ya giza kuu ikamwangukia. Ikawa, jua lilipokuchwa likawa giza, tazama, tanuru ya moshi na
mwenge unaowaka ulipita kati ya vile vipande vya nyama. Siku ile Bwana akafanya agano na Abramu, akasema,
Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.27:1,7-9,13-4,(K)1
1. Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani?
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.
2. Ee Bwana, usikie, kwa sauti yangu ninalia,
Unifadhili, unijibu.
Moyo wangu umekuambia,
Bwana, uso wako nitautafuta. (K)
3. Usinifiche uso wako,
Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira.
Umekuwa msaada wangu, usinitupe,
Wala usiniache, ee Mungu wa wokovu wangu. (K)
4. Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana
Katika nchi ya walio hai.
Umngoje Bwana, uwe hodari,
Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana. (K)
SOMO 2: Flp.3:17-4:1
Ndugu zangu, mnifuate mimi, mkawatazame wao waendao kwa kuufuata mfano tuliowapa ninyi. Maana wengi
huenenda, ambao nimewaambieni mara nyingi habari zao, na sasa nawaambia hata kwa machozi, kuwa ni
adui za msalaba wa Kristo; mwisho wao ni uharibifu, mungu wao ni tumbo, utukufu wao u katika fedheha
yao, waniao mambo ya duniani. Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia
Mwokozi, Bwana Yesu Kristo, atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa
utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake. Basi ndugu
zangu, wapendwa wangu, ninaowaonea shauku, furaha yangu, na taji yangu, hivyo simameni imara katika
Bwana, wapenzi wangu.
SHANGILIO: Mt.17:5
Sauti ya Baba ilitoka katika wingu jeupe:
“Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu,
Msikieni yeye”
INJILI: Lk.9:28b-36
Yesu aliwatwaa Petro na Yohane na Yakobo, akapanda mlimani ili kuomba. Ikawa katika kusali kwake
sura ya uso wake ikageuka, mavazi yake yakawa meupe, yakimetameta. Na tazama, watu wawili walikuwa
wakizungumza naye, nao ni Musa na Eliya; walioonekana katika utukufu, wakanena habari za kufariki
kwake atakakotimiza Yerusalemu. Petro na wale waliokuwa pamoja naye walikuwa wamelemewa na usingizi;
lakini walipokwisha amka waliuona utukufu wake, na wale wawili waliosimama pamoja naye. Ikawa hao
walipokuwa wakijitenga naye, Petro alimwambia Yesu, Bwana mkubwa, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na
tufanye vibanda vitatu; kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya; hali hajui asemalo.
Alipokuwa akisema hayo, lilitokea wingu likawatia uvuli, wakaogopa walipoingia katika wingu hilo.
Sauti ikatoka katika wingu, ikisema, Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye. Na sauti hiyo
ilipokwisha, Yesu alionekana yu peke yake. Nao wakanyamaza, wasitangaze kwa mtu siku zile lolote
katika hayo waliyoyaona.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Yesu aligeuka sura yake mbele ya wafuasi wachache na kuwaonesha utukufu wake wa mbinguni. Alitaka kuwaimarisha
na kuwatia moyo wa kumfuata katika njia ya mateso inayotustahilia tuzo ya mbinguni.
1. Ee Bwana Yesu, uliwaonesha wafuasi utukufu wa mbinguni. Utujalie alama za utukufu wako kwa kujaza mioyo
yetu furaha halisi ya kuteuliwa nawe.
2. Petro aligundua kwamba utukufu unatutamanisha tuwe nao daima. Utujaze hamu ya kutenda matendo yanayotuongoza
kwenye utukufu wa milele.
3. Katika mlima wa utukufu uliongea na wateule wa zamani. Utujalie hamu ya kuonja mambo ya mbinguni kwa
kuwasiliana na watakatifu wako.
4. Ee Bwana Yesu, Mungu Baba alikudhihirisha kuwa ndiwe Mwana wake wa pekee. Akatuambia: Msikieni yeye. Uzibue
masikio ya mioyo yetu ili tuwe tayari kukusikiliza wewe na wenzetu daima.
5. Uwashirikishe marehemu wetu utukufu wako.
Ee Mungu Baba, ni vigumu kutembea katika njia ya imani bila kuona miale michache ya mwanga wa utukufu. Utujalie
dalili chache kwa njia ya Bwana wetu. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba, dhabihu hii ifute dhambi zetu, na kuwatakasa waamini wako mwili na roho,
ili wawe tayari kuadhimisha sikukuu ya Pasaka. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
UTANGULIZI
Bwana Yesu kugeuka sura
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru wewe daima na
popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele, kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Yeye aliwaambia mapema wafuasi wake kwamba atauawa; akawaonesha katika mlima mtakatifu uangavu wake,
kusudi wajue kwamba, kadiri ya ushahidi wa Torati na Manabii, atafikia utukufu wa ufufuko kwa kuteswa.
Kwa hiyo, sisi pamoja na Nguvu za mbinguni, tunakutukuza daima hapa duniani tukisifu bila mwisho adhama
yako kwa sauti kuu:
Mtakatifu, Mtakatifu,Mtakatifu, Bwana Mungu wa majeshi.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Mt.17:5
Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, kwa kupokea mafumbo matakatifu, twafanya bidii kukutolea shukrani, kwani, ingawa
tupo bado duniani, unatujalia kushirikishwa tayari mambo ya mbinguni. Kwa njia ya Kristo Bwana
wetu.
SALA YA KUWAOMBEA WAAMINI
Ee Bwana, uwabariki waamini wako kwa baraka zisizo na mwisho, na uwafanye waambatane hivi na
Injili ya Mwanao pekee, hata wautamani daima ule utukufu ambao uzuri wake aliwaonesha Mitume
katika mwili wake, na mwishowe waweze kuupata kwa furaha. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.