Generic placeholder image

JUMAPILI 2 MAJILIO
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Tumwabudu Bwana, mfalme atakayekuja.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)
Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Sikieni sauti ya mjumbe
'Kristo yu karibu', yasema,
'Tupieni mbali za giza ndoto,
Na mkaribisheni Kristo,
Yeye aliye nuru ya mchana!'

Roho iloshikana na dunia
Iamshwe na hilo onyo kali;
Yesu Kristo ni lake jua,
Liondoalo ulegevu wote,
Asubuhi uwinguni hung'aa.

Basi na atakapokuja tena
Kwa utukufu na vitisho vingi,
Na kuifunika hofu dunia,
Na atokee katika mawingu
Aje na kuwa wetu mtetezi.

ANT. I: Tunao mji imara. Mkombozi ataulinda kwa kuujengea ukuta na boma. Fungueni milango, kwa maana Mungu yu nasi, aleluya.

Zab.118 Sala ya shukrani
Huyu ndiye lile Jiwe mlilolikataa ninyi waashi, ambalo sasa limekuwa jiwe kuu la msingi (Mate.4:11)

Mshukuruni Mungu, kwa kuwa ni mwema,*
kwa maana upendo wake mkuu ni wa milele.

Watu wa Israeli waseme:*
"Upendo wake mkuu ni wa milele.“

Wazao wa Aroni waseme:*
“Upendo wake mkuu ni wa milele."

Wote wamchao Mungu waseme:*
"Upendo wake mkuu ni wa milele."

Katika taabu yangu nilimlilia Mungu,*
naye akanisikiliza na kuniokoa.

Mungu yuko nami, siogopi kitu;*
mwanadamu atanifanya nini?

Mungu yuko nami, ananisaidia;*
nami nitashuhudia kushindwa kwa adui zangu.

Ni afadhali kumtumainia Mungu,*
kuliko kumtegemea mwanadamu.

Ni afadhali kumtumainia Mungu,*
kuliko kuwategemea viongozi wa dunia.

Watu wote wasiomjua Mungu walinizingira,*
lakini kwa nguvu ya Mungu nikawapondaponda.

Walinizunguka kila upande,*
lakini kwa nguvu ya Mungu nikawapondaponda.

Walinivamia kwa wingi kama nyuki,/
lakini wakateketea kama kichaka motoni;*
kwa nguvu ya Mungu nikawapondaponda.

Nilishambuliwa mno karibu nishindwe*
Jakini Mungu alinisaidia.

Mungu hunijalia nguvu na uhodari;*
yeye mwenyewe ameniokoa.

Sikilizeni sauti za furaha na ushindi/
katika mahema ya watu waadilifu;*
"Mkono wa Mungu umetenda mambo ya ajabu!

Mkono wa Mungu umeleta ushindi!*
Mkono wa Mungu umetenda mambo ya ajabu!"

Sitakufa, bali nitaishi,*
na kutangaza matendo ya Mungu.

Mungu ameniadhibu sana,*
lakini hakuniacha nife.

Nifungulie milango ya Hekalu;*
nitaingia na kumshukuru Mungu!

Huu ndio mlango wa Mungu,*
ambao waadilifu waweza kuupitia.

Nakushukuru, Ee Mungu, kwa kunisikiliza;*
kwa sababu wewe umeniokoa.

Jiwe walilolikataa waashi,*
limekuwa jiwe kuu la msingi.

Jambo hili limefanywa na Mungu;*
nalo ni jambo la ajabu mno kwetu.

Hi ndiyo siku aliyoifanya Mungu;*
basi, tushangilie na kufurahi.

Utuokoe, Ee Mungu, utuokoe!*
Ee Mungu, tunakusihi, utupe fanaka!

Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Mungu!*
Twakubariki kutoka nyumbani mwa Mungu.

Mungu ni Mungu, naye ni mwema kwetu./
Shikeni matawi mikononi, anzeni sherehe,*
mkiandamana mpaka madhabahuni.

Ndiwe Mungu wangu, ninakushukuru*
ninakutukuza, Ee Mungu wangu.

Mshukuruni Mungu kwa kuwa ni mwema,*
kwa maana upendo wake mkuu ni wa milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Tunao mji imara. Mkombozi ataulinda kwa kuujengea ukuta na boma. Fungueni milango, kwa maana Mungu yu nasi, aleluya.

ANT. II: Njooni kwenye maji, enyi nyote wenye kiu: mtafuteni Bwana pindi apatikanapo, aleluya.

WIMBO: Dan.3:52-56 Kila kiumbe kimsifu Bwana
Mwumba astahili sifa milele (Rom.1:25)

Umehimidiwa, Ee Bwana, MUNGU wa baba zetu;*
Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.

Limehimidiwa jina lako takatifu, tukufu;*
Lastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.

Umehimidiwa katika hekalu la fahari yako takatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Umehimidiwa juu ya kiti cha ufalme wako,*
Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.

Umehimidiwa utazamaye vilindi, uketiye juu ya makerubi;*
Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.

Umehimidiwa katika anga la mbinguni*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Tumtukuze Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Umehimidiwa katika anga la mbinguni,*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Ant. II: Njooni kwenye maji, enyi nyote wenye kiu: mtafuteni Bwana pindi apatikanapo, aleluya.

ANT. III: Tazameni, Bwana Mungu wetu atakuja kwa enzi, na kuyaangaza macho ya watumishi wake, aleluya.

Zab.150 Zaburi ya kumsifu Mungu
Msifuni Mungu rohoni mwenu, msifuni kwa mioyo yenu, yaani: mtukuzeni Mungu kwa roho na kwa mwili (Hesychius)

Msifuni Mungu Hekaluni mwake;*
msifuni kwa ajili ya enzi yake mbinguni.

Msifuni kwa ajili ya matendo yake makuu;*
msifuni kwa ajili ya utukufu wake mkuu.

Msifuni kwa mlio wa tarumbeta;*
msifuni kwa zeze na kinubi!

Msifuni kwa ngoma na michezo;*
msifuni kwa filimbi na bango!

Msifuni kwa kupiga matoazi;/
msifuni kwa kuvumisha matoazi.*
Kila kiumbe chenye uhai na kimsifu Mungu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Tazameni, Bwana Mungu wetu atakuja kwa enzi, na kuyaangaza macho ya watumishi wake, aleluya.

SOMO: Rom.13:11-12
Zaidi ya hayo, ninyi mnajua tumo katika wakati gani: sasa ndio wakati wa kuamka usingizini; naam, wokovu wetu u karibu zaidi sasa kuliko wakati ule tulipoanza kuamini. Usiku unakwisha na mchana unakaribia. Basi, tutupilie mbali mambo yote ya giza, tukajitwalie silaha za mwanga.

KIITIKIZANO
K. Kristo, Mwana wa Mungu Aliye Hai, utuhurumie. (W. Warudie)
K. Unakuja ulimwenguni.
W. Utuhurumie.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Kristo, ...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Tazama, namtuma mjumbe kabla yako, akutayarishie njia.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Tazama, namtuma mjumbe kabla yako, akutayarishie njia.

MAOMBI
Huu ndio wakati ambapo yatupasa kuamka kutoka usingizini: wokovu uko karibu nasi zaidi sasa kuliko wakati ule tulipopokea imani.
W. Baba wa nuru, tunakutukuza.

Kristo yu aja, ujio wake umekaribia:
- Katika sadaka yetu ya leo, tumtazamie kwa matumaini na furaha. (W.)

Leo tunaposikia Maandiko Matakatifu, yakitangaza ujio wa Mwanao,
- akili na mioyo yetu iamshwe na Neno wako. (W.)

Tunapopokea Mwili na Damu ya Mwanao,
- tuponywe na kutiwa nguvu mpya kwa pendo lako. (W.)

Sisi tulio viungo vya mwili mmoja, utuwezeshe kutafuta amani,
- na kushirikiana katika maisha yetu, mpaka Kristo atakapokuja. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu Mwenyezi, mwenye huruma, usiruhusu kazi zetu za kila siku, wala shughuli za maisha haya, zitucheleweshe kwenda kukutana na Mwanao, bali kwa hekima yako utuangaze na kutuingiza katika ushirika wake. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.