Generic placeholder image

JUMAPILI 2 MAJILIO
MASIFU YA JIONI I

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya

UTENZI
Muumba wa nyota za usiku,
Mwanga wa milele wa taifa,
Mkombozi wetu sisi sote,
Utusikie tukuitapo.

Kwa mwili wa Maria 'likuja,
Tuokoke dhambi na aibu,
Kwa neema yako Mkombozi
Sasa njoo tuponye wadhambi.

Na siku ya hukumu ya mwisho,
Sisi tutakapofufuliwa,
Fika Mkombozi mwenye baraka,
Tupeleke rahani milele.
Irvin Udulutsch OSB

ANT. I: Ewe Sion mpya, shangilia na kufurahia. Tazama sasa jinsi Mfalme wako, Mwokozi wetu, atakavyokuja kwako kwa unyenyekevu.

Zab.119:105-112 XIV Sheria ya Mungu ni mwanga
Hii ndiyo amri yangu: pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda ninyi (Yoh.15:12)

Neno lako ni taa ya kuniongoza,*
na mwanga katika njia yangu.

Nimeapa na kuthibitisha kiapo changu,*
kwamba nitashika maagizo yako maadilifu.

Ee Mungu, ninateseka mno;*
unipe uhai kama ulivyoahidi.

Ee Mungu, upokee sala yangu ya shukrani;*
na unifundishe maagizo yako.

Maisha yangu yamo hatarini daima,*
lakini siisahau sheria yako.

Waovu wamenitegea mtego kuninasa,*
lakini sikiuki amri zako.

Maagizo yako ni rasilimali yangu daima;*
naam, ni furaha ya moyo wangu.

Nimekusudia kwa moyo wote*
kutimiza kanuni zako milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Ewe Sion mpya, shangilia na kufurahia. Tazama sasa jinsi Mfalme wako, Mwokozi wetu, atakavyokuja kwako kwa unyenyekevu.

ANT. II: Itieni nguvu mikono iliyochoka: muwe imara na semeni, Tazameni, Mungu wetu atakuja kutuokoa, aleluya.

Zab.16 Kuomba usalama
Mungu alimfufua Yesu, akamwokoa kutoka katika maumivu ya kifo (Mate.2:24)

Unilinde, Ee Mungu;*
nakimbilia usalama kwako.

Nimemwambia Mungu: “Wewe ni Bwana wangu;*
mema yote niliyo nayo yatoka kwako."

Ni bora sana hao watakatifu walioko nchini;*
kukaa nao ndiyo furaha yangu.

Lakini wanaokimbilia miungu mingine,*
wanajizidishia taabu wao wenyewe.

Damu ya matambiko sitawatolea kamwe;*
na majina ya miungu hiyo sitayataja kamwe.

Ee Mungu, wewe peke yako, ndiwe tegemeo langu;/
wewe wanipa mahitaji yangu yote;*
maisha yangu yamo mikononi mwako.

Umenipimia sehemu nzuri sana;*
naam, kila ulichonipa ni kizuri sana.

Nitamtukuza Mungu kwa kuniongoza,*
na usiku dhamiri yangu yanionya.

Namweka Mungu mbele yangu daima,*
yuko karibu nami, wala sitatikisika.

Kwa hiyo nafurahi na kushangilia,*
nami nitakaa salama salimini,

kwani wanikinga na nguvu za kuzimu,*
wala humwachi mpendwa wako apotee huko ahera.

Utanionyesha njia ya kufikia uzima;/
kuwako kwako kwanijaza furaha,*
uwezo wako waniletea raha daima.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Itieni nguvu mikono iliyochoka: muwe imara na semeni, Tazameni, Mungu wetu atakuja kutuokoa, aleluya.

ANT. III: Kwa njia ya Musa watu walipewa sheria, kwa njia ya Yesu Kristo tumepewa neema na kweli.

WIMBO: Filp.2:6-11 Kristo, mtumishi wa Mungu
Yesu, kwa asili,*
alikuwa daima Mungu;

lakini hakufikiri kwamba/
kule kuwa sawa na Mungu*
ni kitu cha kung'ang'ania kwa nguvu.

Bali, kwa hiari yake mwenyewe,*
aliachilia hayo yote,

akajitwalia hali ya mtumishi/
akawa sawa na wanadamu,*
akaonekana kama wanadamu.

Alijinyenyekeza na kutii mpaka kufa,*
hata kufa msalabani.

Kwa sababu hiyo*
Mungu alimkweza juu kabisa,

akampa jina lililo kuu zaidi*
kuliko majina yote.

Ili kwa heshima ya jina la Yesu,/
viumbe vyote mbinguni, duniani na kuzimu,*
vipige magoti mbele yake;

Na kila mtu akiri/
Kwamba Yesu Kristo ni Bwana,*
kwa utukufu wa Mungu Baba.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Kwa njia ya Musa watu walipewa sheria, kwa njia ya Yesu Kristo tumepewa neema na kweli.

SOMO: 1Tes.5:23-24
Mungu anayetupatia amani awafanye ninyi watakatifu kwa kila namna na kuzilinda nafsi zenu - roho, mioyo na miili yenu - mbali na hatia yo yote wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye anayewaita ninyi atafanya hivyo kwani ni mwaminifu.

KIITIKIZANO
K. Utuoneshe, Ee Bwana, fadhili zako za milele. (W. Warudie)
K. Na utujalie wokovu wako.
W. Na fadhili zako za milele.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Utuoneshe...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Uje, Ee Bwana, na utuletee amani na tufurahi mbele yako kwa mioyo minyofu.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana.
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Uje, Ee Bwana, na utuletee amani na tufurahi mbele yako kwa mioyo minyofu.

MAOMBI
Kabla wakati haujaanza, Neno alikuwako pamoja na Baba; wakati ulipotimia alikuja kwetu kwa njia ya Bikira Maria.
W. Kwa njia ya Kanisa, uje kwetu leo, Bwana Yesu.

Vyote viliumbwa kwa njia yake:
- tunaomba maisha yetu yawe nuru kwa wengine. (W.)

Neno yu pamoja na Mungu:
- tunaomba tuishi naye katika upendo wa Baba. (W.)

Neno alikuja kwake, lakini watu wake hawakumpokea.
- Tumkaribishe Neno mioyoni mwetu kwa kuwasaidia wale wanaohitaji msaada wetu. (W.)

Neno alikuja kwetu, amejaa neema na kweli;
- tunaomba marehemu wote wahesabiwe kuwa wana wa Mungu. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu Mwenyezi, mwenye huruma, usiruhusu kazi zetu za kila siku, wala shughuli za maisha haya, zitucheleweshe kwenda kukutana na Mwanao, bali kwa hekima yako utuangaze na utuingize katika ushirika wake. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.