JUMAPILI 2 MAJILIO
MASIFU YA JIONI II
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya
UTENZI
Muumba wa nyota za usiku,
Mwanga wa milele wa taifa,
Mkombozi wetu sisi sote,
Utusikie tukuitapo.
Kwa mwili wa Maria 'likuja,
Tuokoke dhambi na aibu,
Kwa neema yako Mkombozi
Sasa njoo tuponye wadhambi.
Na siku ya hukumu ya mwisho,
Sisi tutakapofufuliwa,
Fika Mkombozi mwenye baraka,
Tupeleke rahani milele.
Irvin Udulutsch OSB
ANT. I: Tazama, Bwana atakuja akiwa katika mawingu ya juu na uwezo
mkuu, aleluya.
Zab.110:1-5,7 Kutawazwa kwa mfalme mteule
Kristo sharti atawale mpaka Mungu atakapowashinda adui zake na kuwaweka chini ya
miguu yake (1Kor.15:25)
Mungu amemwambia bwana wangu,*
"Keti upande wangu wa kulia,
Mpaka niwafanye maadui zako,*
kama kibao cha kuegemea miguu yako."
Toka Sion Mungu ataeneza enzi yako.*
Asema: "Tawala juu ya adui zako!"
Watu wako watajitolea,*
siku utakapopambana na adui.
Vijana wako watakujia kwenye milima mitakatifu,*
kama vile umande wa asubuhi.
Mungu ameapa, wala hataghairi:/
"Kwamba wewe ni kuhani milele,*
kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki."
Mungu yuko upande wako wa kulia;*
atakapokasirika, atawaponda wafalme.
Njiani mfalme atakunywa maji ya kijito;*
kwa hiyo atainua kichwa juu kwa ushindi.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Tazama, Bwana atakuja akiwa katika mawingu ya juu na uwezo
mkuu, aleluya
ANT. II: Bwana atakuja, wala hatatusahau. Mngojeeni hata kama itaonekana
anakawia, maana hakika atakuja, aleluya.
Zab.115 Mungu mmoja wa kweli
Mmemgeukia Mungu, mkaziacha sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai na wa kweli (1Tes.1:9)
Sio sisi, Ee Mungu, sio sisi;/
bali wewe peke yako utukuzwe,*
kwa ajili ya upendo wako mkuu na uaminifu wako.
Kwa nini mataifa yanatuuliza:*
"Mungu wenu yuko wapi?"
Mungu wetu yuko mbinguni;*
yote anayotaka huyafanya.
Miungu yao imefanywa kwa fedha na dhahabu;*
imetengenezwa kwa mikono ya wanadamu.
Ina vinywa lakini haisemi;*
ina macho lakini haioni.
Ina masikio lakini haisikii;*
ina pua lakini hainusi.
Ina mikono lakini haipapasi;/
ina miguu lakini haitembei.*
Haiwezi kamwe kutoa sauti.
Wote wanaoitengeneza wanafanana nayo,*
kadhalika na wote walio na imani nayo.
Enyi watu wa Israeli mtumainieni Mungu;*
yeye ni msaidizi wenu na ngao yenu.
Enyi wazao wa Aroni mtumainieni Mungu;*
yeye ni msaidizi wenu na mlinzi wenu.
Enyi mnaomcha Mungu mtumainieni Mungu;*
yeye ni msaidizi wenu na mlinzi wenu.
Mungu anatukumbuka, na atatubariki;/
atawabariki watu wa Israeli,*
atawabariki wazao wa Aron.
Atawabariki wote wamchao,*
atawabariki wazao wa Aron.
Mungu awajalieni watoto;*
awajalie ninyi na wazao wenu!
Mbarikiwe na Mungu,*
aliyeumba mbingu na dunia.
Mbingu ni mali yake Mungu,*
bali dunia amewapa wanadamu.
Sio wafu wanaomsifu Mungu,*
wala ye yote aliyeshuka kuzimuni.
Basi ni sisi tutakaomsifu Mungu,*
sasa na hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. II: Bwana atakuja, wala hatatusahau. Mngojeeni hata kama itaonekana
anakawia, maana hakika atakuja, aleluya.
ANT. III: Bwana ni hakimu wetu, Bwana ni Mfalme wetu. Yeye atakuja kutuokoa.
WIMBO: Ufu.19:1,2,5-7 Arusi ya Mwana-kondoo
Aleluya.
Wokovu, utukufu na nguvu ni mali yake Mungu wetu!*
(W. Aleluya)
Maana hukumu yake ni ya kweli na ya haki.
W. Aleluya (aleluya).
Aleluya.
Msifuni Mungu enyi watumishi wake wote,*
(W. Aleluya)
Nanyi nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa.
W. Aleluya (aleluya).
Aleluya.
Bwana, Mungu wetu Mwenyezi , ni Mfalme!*
(W. Aleluya)
Tufurahi na kushangilia; tumtukuze.
W. Aleluya (aleluya).
Aleluya.
Wakati wa arusi ya Mwana-kondoo umefika,*
(W. Aleluya)
Na bibi arusi yuko tayari.
W. Aleluya (aleluya).
Aleluya.
Atukuzwe Baba na Mwana, na Roho Mtakatifu,*
(W. Aleluya)
Kama mwanzo na sasa na siku zote, na milele. Amina.*
W. Aleluya (aleluya).
Ant. III: Bwana ni hakimu wetu, Bwana ni Mfalme wetu. Yeye atakuja kutuokoa.
SOMO: Filp.4:4-5
Basi, furahini daima katika kuungana na Bwana! Nasema tena: furahini! Mwe wapole kwa watu wote,
Bwana yu karibu.
KIITIKIZANO
K. Utuoneshe, Ee Bwana, fadhili zako. (W. Warudie)
K. Na utujalie wokovu wako.
W. Na fadhili zako.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Utuoneshe...
Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Una heri, Ewe Maria, kwa sababu ulikuwa na imani: ahadi ya Bwana kwako itatimia, aleluya.
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.
Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.
Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,
kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Una heri, Ewe Maria, kwa sababu ulikuwa na imani: ahadi ya Bwana
kwako itatimia, aleluya.
MAOMBI
Sauti ya Yohane Mbatizaji iliayo jangwani yasikika tena leo kwa njia ya Kanisa:
W. Uiweke tayari mioyo yetu, Ee Bwana.
Kwa kutujia kwa neema wakati huu wa Majilio, -(W.)
Kwa kazi impasayo mwanadamu kutenda, ili kuufanya ulimwengu uwe wenye haki zaidi, -(W.)
Kwa uelewano tutakaohitaji juma hili, kwa ajili ya familia zetu na marafiki, -(W.)
Kwa kifo, kwa hukumu yetu, na kwa uzima wa milele pamoja nawe, -(W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Mungu Mwenyezi, mwenye huruma, usiruhusu kazi zetu za kila siku, wala shughuli za maisha haya,
zitucheleweshe kwenda kukutana na Mwanao, bali kwa hekima yako utuangaze na utuingize katika
ushirika wake. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala
nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.