Generic placeholder image

JUMAPILI 2 MAJILIO
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Njoo Roho Mtakatifu,
Ndani yetu sisi uishi,
Pamoja nawe waje pia
Mungu Baba na Mungu Mwana,
Nazo zako tele neema
Njoo upate tujalia,
Zitufanye watakatifu,
Pia tuwe kitu kimoja.

Imara katika upendo
Na viwe, roho na ulimi,
Yako sifa kuitangaza
Kila mahali duniani,
Na ule upendo jalie-
Ulio mwetu mioyoni-
Mioyo mingine iwashwe
Kutokana na mwako wake.

Ee Mtukufu kabisa
Utatu ulio upendo,
Moyo wake bin-Adamu
Kwa ajili yako 'liumbwa,
Kwako Wewe na iwe sifa
Kwa wimbo usio na mwisho,
Haki yako Wewe pekee
Kwabudiwa hata milele.

Kabla ya Adhuhuri
ANT.: Manabii walitabiri kwamba Mwokozi atazaliwa na bikira.

Adhuhuri
ANT.: Malaika Gabrieli alimwambia Maria, 'Furahi, wewe uliyependelewa sana! Bwana yu pamoja nawe. Umebarikiwa kuliko wanawake wote.'

Baada ya Adhuhuri
ANT.: Maria alihangaishwa sana na amkio hilo, akajiuliza: 'Salamu hii ina maana gani?' Akawaza: 'Nitamzaa Mfalme bila kupoteza ubikira!'

Zab.23 Mungu mchungaji wetu
Mwana-kondoo atakuwa mchungaji wao, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji ya uzima (Ufu.7:17)

Mungu ni mchungaji wangu;*
sitapungukiwa chochote,

Hunipumzisha kwenye malisho mabichi;/
huniongoza kwenye maji matulivu na safi,*
na kunirudishia nguvu.

Huniongoza katika njia iliyo sawa,*
kwa ajili ya jina lake.

Nijapopita katika giza kuu, sitaogopa,/
kwa kuwa wewe Mungu u pamoja nami;*
fimbo yako na bakora yako vyanilinda.

Waniandalia karamu mbele ya adui zangu;/
umenipaka mafuta kichwani mwangu,*
na kikombe changu wakijaza mpaka kufurika.

Hakika wema wako na upendo wako mkuu,/
vitakuwa pamoja nami maisha yangu yote.*
Nitakaa nyumbani mwako muda wote niishipo.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.76 Mungu Mshindi
Watamwona Mwana wa Mtu akija juu ya mawingu ya angani (Mt.24:30)

I
Mungu anajulikana katika Yuda;*
jina lake ni kuu katika Israeli.

Hema lake liko huko Salemu;*
makao yake yako huko Sion.

Huko alivunja mishale ya adui;*
alivunja ngao, panga na silaha.

Wewe, Ee Mungu, watukuka mno;/
umejaa fahari kuu unaporudi,*
kutoka milimani ulikowashinda adui.

Washupavu wao wamenyang'anywa nyara zao,/
sasa wanalala usingizi wao wa mwisho,*
ushujaa wao wote haukuwafaa kitu.

Ulipowakemea, Ee Mungu wa Yakobo,*
farasi na wapanda farasi walikufa ganzi.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

II
Wewe, Ee Mungu, ni wa kutisha mno!*
Nani awezaye kustahimili ukikasirika?

Umejulisha hukumu yako toka mbinguni,*
nayo dunia ikaogopa na kunyamaa;

wakati ulipoinuka, Ee Mungu, kutoa hukumu,*
kuwaokoa wote wanaodhulumiwa duniani.

Ghadhabu ya watu husababisha tu sifa kwako;*
na walioponea huko Emati watafanya sikukuu zako.

Mpeni Mungu, Mungu wenu, yale mliyoahidi;*
enyi mlio karibu, mpeni vipaji Mungu wa kutisha.

Yeye huwanyenyekesha wakuu;*
huwatisha wafalme wa dunia.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Kabla ya Adhuhuri
ANT.: Manabii walitabiri kwamba Mwokozi atazaliwa na bikira.

Adhuhuri
ANT.: Malaika Gabrieli alimwambia Maria, 'Furahi, wewe uliyependelewa sana! Bwana yu pamoja nawe. Umebarikiwa kuliko wanawake wote.'

Baada ya Adhuhuri
ANT.: Maria alihangaishwa sana na amkio hilo, akajiuliza: 'Salamu hii ina maana gani?' Akawaza: 'Nitamzaa Mfalme bila kupoteza ubikira!'

MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: Rom.13:13-14a
Mwenendo wetu uwe wa adabu kama inavyostahili wakati wa mwanga; tusiwe na ulafi na ulevi, uchafu na uasherati, ugomvi na wivu. Bwana Yesu Kristo awe vazi lenu.

K. Mataifa yatalicha jina lako, Bwana.
W. Na wafalme wote wa dunia watatukuza utukufu wako.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Adhuhuri: 1Tes.3:12-13
Bwana awawezeshe ninyi kupendana na kuwapenda watu wote zaidi na zaidi, kama vile sisi tunavyowapenda ninyi. Hivyo ataiimarisha mioyo yenu nanyi mtakuwa wakamilifu na watakatifu mbele ya Mungu na Baba yetu wakati Bwana wetu Yesu atakapokuja pamoja na wote walio wake.

K. Utukumbuke, Ee Bwana, kwa upendo wako ulio nao kwa watu wako.
W. Njoo utuokoe.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: 2Tes.1:6,7,10
Kwa kuwa ni haki, Mungu atawalipa mateso wale wawatesao ninyi, na kuwalipa ninyi mteswao leo pamoja na sisi, wakati wa kufunuliwa kwake Bwana Yesu kutoka mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake, siku hiyo atakapokuja ili kutukuzwa katika watakatifu wake na kustaajabiwa katika wote waliomsadiki.

K. Njoo, Ee Bwana, usikawie.
W. Uwafungue watu wako kutoka katika dhambi zao.

SALA:
Tuombe: Mungu Mwenyezi, mwenye huruma, usiruhusu kazi zetu za kila siku, wala shughuli za maisha haya, zitucheleweshe kwenda kukutana na Mwanao, bali kwa hekima yako utuangaze na kutuingiza katika ushirika wake. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.