DOMINIKA YA 2 MAJILIO

MASOMO MWAKA C

ANTIFONA YA KUINGIA: Isa.30:19,30
Enyi watu wa Sayuni, tazameni Bwana atakuja kuwaokoa mataifa; naye Bwana atawasikizisha sauti yake ya utukufu katika furaha ya mioyo yenu.

KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi na mwenye rehema, utujalie ili shughuli zozote za kidunia zisituzuie kufanya hima kumlaki Mwanao, bali mafundisho ya hekima ya mbinguni yatufanye tuwe washirika wake. Anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Bar.5:1-9
Ee Yerusalemu, vua nguo za matanga na huzuni, Uvae uzuri wa utukufu utokao kwa Mungu milele. Jifungie nguo ya haki itokayo kwa Mungu, Jipige kilemba kichwani cha utukufu wake aliye wa milele. Maana Mungu ataidhihirisha nuru yako duniani mwote, Na jina lako litaitwa na Mungu daima, Amani ya haki, na Utukufu wa utauwa. Ondoka, Ee Yerusalemu, usimame juu; Tazama upande wa mashariki, uangalie: Toka machweo ya jua hata maawio yake wanao wanakusanyika kwa neno lake Yeye Aliye Mtakatifu, Wakifurahi kwa kuwa Mungu amewakumbuka. Waliondoka kwako kwa miguu, wakikokotwa na adui zao. Lakini Mungu anawarejeza kwako wameinuliwa juu kwa heshima kama katika kiti cha enzi. Maana kwa maagizo ya Mungu kila kilima kirefu kitashushwa, na milima ya milele. Na mabonde yote yatajazwa, hata nchi iwe sawa, Ili Israeli aende salama katika utukufu wa Mungu. Nayo misitu, na miti yote itoayo harufu nzuri, Imemtia Israeli kivuli kwa amri ya Mungu; Kwa kuwa Mungu atamwongoza Israeli kwa furaha katika mwangaza wa utukufu wake, kwa ile rehema na haki itokayo kwake.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.126:1-6(K)3
1. Bwana alipowarejeza mateka wa Sayuni,
Tulikuwa kama waotao ndoto.
Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko,
Na ulimi wetu kelele za furaha.

(K) Bwana alitutendea mambo makuu, Tulikuwa tukifurahi.

2. Ndipo waliposema katika mataifa,
Bwana amewatendea mambo makuu.
Bwana alitutendea mambo makuu,
Tulikuwa tukifurahi. (K)

3. Ee Bwana, uwarejeze watu wetu waliofungwa,
Kama vijito vya Kusini,
Wapandao kwa machozi
Watavuna kwa kelele za furaha. (K)

4. Ingawa mtu anakwenda zake akilia,
Azichukuapo mbegu za kupanda
Hakika atarudi kwa kelele za furaha
Aichukuapo miganda yake. (K)

SOMO 2: Flp.1:3-6,8-11
Ndugu zangu: Namshukuru Mungu wangu kila wakati niwakumbukapo, siku zote kila niwaombeapo minyi nyote nikisema sala zangu kwa furaha kwa sababu ya ushirika wenu katika kuieneza Injili tangu siku ile ya kwanza hata leo hivi. Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu. Maana Mungu ni shahidi wangu, jinsi ninavyowaonea shauku ninyi nyote katika moyo wake Kristo Yesu. Na hii ndiyo dua yangu, kwamba pendo lenu lizidi kuwa jingi sana, katika hekima na ufahamu wote; mpate kuyakubali yaliyo mema; ili mpate kuwa na mioyo safi, bila kosa, mpaka siku ya Kristo; hali mmejazwa matunda ya haki, kwa njia ya Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa ya Mungu.

SHANGILIO: Lk.3:4,6
Aleluya, aleluya!
Itengenezeni njia ya Bwana, yanyosheni mapito yake, Na wote wenye mwili watauona wokovu wa Mungu,
Aleluya!

SOMO 3: INJILI: Lk.3:1-6
Mwaka wa kumi na tano wa kutawala kwake Kaisari Tiberio, Pontio Pilato alipokuwa liwali wa Uyahudi, na Herode mfalme wa Galilaya, na Filipo, ndugu yake mfalme wa Iturea na nchi ya Trakoniti, na Lisania mfalme wa Abilene, wakati wa ukuhani mkuu wa Anasi na Kayafa, neno la Mungu lilimfikia Yohane, mwana wa Zakaria, jangwani. Akafika nchi yote iliyo karibu na Yordani, akihubiri Ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi, kama ilivyoandikwa katika chuo cha maneno ya Nabii Isaya: Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake. Kila bonde litajazwa, Na kila mlima na kilima kitashushwa; Palipopotoka patakuwa pamenyoka, Na palipoparuza patalainishwa Na wote wenye mwili watauona wokovu wa Mungu.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Ee Mungu Baba, toka mwanzo uliwatuma duniani Manabii kama vile Yohane Mbatizaji, wawakusanye watu na kuwaongoza katika njia ya kukutana nawe, Mwokozi wao. Tunakuomba,

1. Utuamshe tukubali kuongozwa na Mitume na wajumbe wako ili tufikie wokovu wa mwili na wa roho.

2. Utusaidie kutambua wajibu wetu wa kuwaongoza wenzetu kwako wewe, Mungu Mwokozi wetu.

3. Uwasaidie wakubwa wa serikali kutambua kwamba wana wajibu wa kutayarisha hali ya taratibu na amani na kuwawezesha raia kuishi kwa amani na uelewano.

4. Utuangaze na kututayarisha kuondoa vikwazo vinavyoziba njia ya kufikia wokovu.

5. Uwapokee kwenye hali kamili ya wokovu marehemu wetu waliojibidisha kuwatayarishia wenzao njia ya wokovu.

Ee Baba wa mbinguni, bila msaada wako hatuwezi kitu, kwa hiyo usikilize maombi yetu tunayokupelekea kwa msaada wa Bwana wetu Yesu Kristo. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba sala na dhabihu zetu sisi wanyonge zikutulize; na kwa kuwa mastahili yetu hayatoshi kitu, ututie shime kwa rehema yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

1. UTANGULIZI WA MAJILIO:
MAJILIO I:

K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.

K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele, kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Yeye, katika ujio wake wa kwanza, alipokuja katika unyenyekevu wa mwili, aliutimiza mpango ulioandaliwa nawe tangu kale. Hivyo, akatufungulia njia ya wokovu wa milele, ili, atakapokuja tena katika utukufu wa enzi yake, hatimaye tupewe waziwazi mema yaliyoahidiwa, ambayo kwa sasa tunathubutu kuyatarajia, tukikesha.
Kwa sababu hiyo, sisi pamoja na Malaika na Malaika Wakuu, pamoja na Viti vya enzi na Milki, na majeshi yote ya Malaika wa mbinguni, twaimba utenzi wa utukufu wako, tukisema bila mwisho:

W. Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,
Bwana Mungu wa majeshi.
Mbingu na dunia zimejaa utukufu wako.
Hosana juu mbinguni.
Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.
Hosana juu mbinguni.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Bar.5:5;4:36
Ondoka, ee Yerusalemu, usimame juu; tazama uione furaha inayokujia kutoka kwa Mungu wako.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, baada ya kushibishwa kwa chakula cha kiroho, tunakuomba kwa unyenyekevu, ili kwa kushiriki fumbo hili, utufundishe kuyapima kwa hekima malimwengu na kuambatana na mambo ya mbinguni. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.